Wakati wengi huamini uzee ni mwisho wa kutimiza ndoto kubwa maishani, kwa Richard Eitel (Dick) hali ilikuwa tofauti baada ya kutimiza ndoto aliyoiwaza tangu ujana wake ya kufika Ncha ya Kaskazini duniani (North Pole).

Dick, ambaye kwa sasa ana miaka 95, ameweka rekodi mpya ya Kitabu cha Guinness baada ya kuwa mtu mwenye umri mkubwa zaidi kuwahi kufika eneo hilo maarufu la 90°N.

Rekodi hiyo ilithibitishwa Agosti 10 mwaka huu, Dick alikuwa na umri wa miaka 95 na siku 236 alipofika North Pole kupitia safari ya maelfu ya kilomita kwa kutumia meli ya Le Commandant Charcot.

Richard Eitel (katikati) ameweka rekodi mpya ya Kitabu cha Guinness baada ya kuwa mtu mwenye umri mkubwa zaidi kufika eneo la ncha ya Kaskazini maarufu 90°N. Picha na Mtandao

Kwa mafanikio hayo, Dick alivunja rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na Mmarekani mwingine, Edward Stahl, aliyefika North Pole mwaka 2022 akiwa na miaka 90 na siku 334.

Licha ya umri wake mkubwa, Dick bado ni mwanamichezo mwenye nguvu anayependa tenisi, kuteleza kwenye theluji na kutumia muda na familia yake.

Hata hivyo, kwa miaka mingi alikuwa hajapata nafasi ya kutimiza ndoto yake ya kufika eneo hilo lenye barafu kali duniani.

Ndoto hiyo ilitimia baada ya familia yake kuamua kumuandalia safari maalumu kama sehemu ya kumsaidia kutimiza azma yake ya maisha.

Miongoni mwa walioambatana naye ni wajukuu zake watano, akiwamo Alexandra aliyesaidia kupanga safari hiyo, hatua za usalama na maandalizi yote yaliyohitajika hadi kuthibitishwa rasmi na Kitabu cha Guinness.

Richard Eitel (Dick) ameweka rekodi mpya ya Kitabu cha Guinness baada ya kuwa mtu mwenye umri mkubwa zaidi kufika eneo la ncha ya Kaskazini maarufu 90°N. Picha na Mtandao

Walipofika North Pole, Dick alisherehekea mafanikio hayo akiwa pamoja na nahodha wa meli hiyo, Patrick Marchesseau pamoja na familia yake iliyokuwa na furaha kubwa kumuona akitimiza ndoto yake ya muda mrefu.

Baada ya kushuka katika eneo hilo lenye barafu nzito na hali kali ya hewa, Dick alivaa mavazi maalumu ya baridi kabla ya kufanya mchezo wa kuteleza kwenye theluji katika eneo la juu kabisa duniani.

Imeandikwa na Elizabeth Edward kwa msaada wa mtandao

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *