Tanga. Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Tanga limeazimia kuwa vituo vya mabasi ya mikoani vilivyopo katikati ya jiji vihamishiwe kwenda Kituo Kikuu cha Mabasi cha Kange kuanzia Julai mosi, 2026, licha ya upinzani uliotolewa awali na Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC).
Awali, mpango huo ulitarajiwa kuanza kutekelezwa Februari 30, 2026, lakini ulisimama kufuatia msimamo wa kikao cha RCC, uliopinga utekelezaji wake kwa wakati huo.
Katika kikao cha Baraza la Madiwani cha Mei 13, 2026, baadhi ya madiwani walisisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za haraka, wakieleza kuwa uwepo wa vituo vya mabasi katikati ya jiji umeendelea kusababisha msongamano mkubwa wa magari na usumbufu kwa wananchi.
Diwani wa Viti Maalumu kupitia CCM, Habiba Namalecha, amesema suala la kuhamia Kange limekuwa likicheleweshwa kwa muda mrefu licha ya baraza kuidhinisha mpango huo.
Meya wa jiji la Tanga, Mustapha Seleboss akitoa msisitizo wa mpango kuondoa vituo vya mabasi ya abiria wa mikoani katikati ya jiji la Tanga na kwenda kituo kikuu cha mabasi cha Kange.
“Vurugu zote za magari zipo mjini, hakuna hata mtaa wa kupita. Tulijenga stendi ya Kange kwa lengo la kuwa kitega uchumi cha Jiji la Tanga, lakini bado haitumiki ipasavyo,” amesema Namalecha.
Ameeleza kuwa kwa sasa kituo hicho kinatumiwa zaidi na magari madogo, huku mabasi makubwa yakiendelea kutoa huduma katikati ya jiji.
Kwa upande wake, Diwani wa Maweni, Joseph Colvas, amesema mjadala wa lini mabasi yahamie Kange umepitwa na wakati, na kinachohitajika sasa ni utekelezaji wa maamuzi ya baraza.
“Wenye Tanga ni sisi. Tunaitaka stendi ya Kange ianze kutumika sasa,” amesema Colvas.
Naye Diwani wa Mnyanjani, Thobias Haule, amewatuhumu baadhi ya wafanyabiashara kwa kukwamisha utekelezaji wa mpango huo.
“Wapo watu wanatamba mjini kwamba hawawezi kuondoka. Tunataka maamuzi ya halmashauri yaheshimiwe,” amesema Haule.
Akizungumzia suala hilo, Meya wa Jiji la Tanga, Mustapha Seleboss, amesema hakuna mamlaka yenye uwezo wa kubatilisha maamuzi ya Baraza la Madiwani isipokuwa madiwani wenyewe, kwa mujibu wa sheria.
“Tulipoelekeza mabasi makubwa yaanze kutoa huduma Kange, utekelezaji ulikwama kutokana na muingiliano wa mamlaka. Lakini msimamo wetu ni kwamba stendi ya Kange lazima itumike,” amesema Seleboss.
Aidha, amewataka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), pamoja na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura), kuhakikisha mabasi hayaendelei kupakia abiria katika maeneo yasiyo rasmi ndani ya jiji.
Seleboss amesema Serikali imewekeza zaidi ya Sh3 bilioni katika ujenzi wa stendi ya Kange, hivyo ni lazima ilete tija kwa wananchi na halmashauri.
“Tumetumia fedha nyingi kujenga kituo hiki. Hatuwezi kuendelea kuona hakifanyi kazi wakati mabasi yote yapo mjini,” amesema.
Ameongeza kuwa halmashauri imekuwa ikitarajia kukusanya zaidi ya Sh6 bilioni kutokana na shughuli za stendi hiyo, lakini mapato hayo hayawezi kupatikana ipasavyo ikiwa kituo hakitatumika kikamilifu.
Hata hivyo, hoja zilizowahi kuibuka na kusababisha kusitishwa kwa mpango huo ni pamoja na hofu ya kuongezeka kwa gharama za usafiri kwa wananchi, ambao watalazimika kwenda Kange badala ya kutumia vituo vilivyopo katikati ya jiji.
Pia, kulikuwa na wasiwasi kuhusu usafiri wa usiku kwa abiria wanaoingia na kutoka nje ya Mkoa wa Tanga, kutokana na ukosefu wa daladala zinazofanya kazi nyakati za usiku, tofauti na ilivyo katika miji mikubwa kama Dar es Salaam.
Wadau wamesisitiza umuhimu wa kuweka mazingira rafiki na salama kwa wasafiri kabla ya utekelezaji kamili wa mpango huo.
Licha ya changamoto hizo, kikao cha Baraza la Madiwani kimeridhia kuanza kwa utekelezaji wa mpango huo, huku kikao cha wadau wa usafirishaji kikitarajiwa kuitishwa kwa ajili ya kujadili suala hilo kwa kina zaidi.
Dereva wa daladala, Rashid Mtoi, amesema uamuzi huo una manufaa kwa halmashauri kwa kuwa utaongeza mapato na kuimarisha matumizi ya kituo hicho.
“Ahadi ya kuhamisha mabasi imekuwa ikitolewa kwa muda mrefu bila utekelezaji, sasa ngoja tuone,” amesema Mtoi.
Naye Ramadhan Abdalah wa Barabara ya 12 jijini Tanga amesema ni muhimu mamlaka kuzingatia mahitaji ya abiria wanaowasili nyakati za usiku kabla ya utekelezaji kamili wa agizo hilo.
“Ni lazima kuwe na daladala za kutosha kwa abiria wanaofika nyakati za usiku,” amesema.
Kwa upande wake, mdau wa usafirishaji, Shaibu Ramadhani, ameunga mkono mpango huo, lakini akasisitiza umuhimu wa kuimarisha usalama katika kituo hicho.
“Mazingira rafiki na usalama wa saa 24 ni jambo la msingi kwa abiria,” amesema.