
Meneja wa Programu ya Usimamizi wa Maliasili wa FAO, Philip Kisoyan, amesema kuwa mpango huo unasaidia jamii kutambua thamani ya kiuchumi ya misitu huku ukilinda mifumo muhimu ya ikolojia.
“Mpango wa Forest and Farm Facility ni mpango wa ruzuku unaosaidia mashirika ya wazalishaji wadogo wadogo, ikiwemo vyama vya misitu vya kijamii.”
Mwaka huu, moja ya wanufaika wa mpango huo, Chama cha Misitu cha Jamii cha Maragoli katika Kaunti ya Vihiga, kiliandaa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya misitu chini ya kaulimbiu Misitu na Uchumi.
Wakati wa maadhimisho hayo, takriban miti elfu ishirini ilipandwa katika kilima cha Maragoli kama sehemu ya juhudi zinazoendelea za kurejesha mfumo wa ikolojia katika kaunti hiyo.
Kisoyan amesema mpango wa FFF tayari umeleta mafanikio makubwa kote nchini.
“Kupitia mpango wa Forest and Farm Facility, tumesaidia zaidi ya misitu tisa katika kaunti nane na kufanikisha zaidi ya hekta 160,000 kuwa chini ya usimamizi endelevu wa misitu.”
Mpango huo pia umechangia maendeleo ya minyororo ya thamani pamoja na kusaidia maisha ya jamii zinazotegemea misitu kwa kipato na maisha yao ya kila siku.
FAO imesema mpango huo utaendelea kusaidia urejeshaji wa mandhari, shughuli za uhifadhi, pamoja na kuwawezesha wakulima wadogo wadogo na jamii za misituni kiuchumi.
“FFF itaendelea kutoa msaada kwa jamii na wakulima wadogo wadogo katika urejeshaji wa mandhari, maendeleo ya minyororo ya thamani na kuboresha maisha yao.”
Hafla iliwaleta pamoja viongozi waandamizi wa serikali ya Kenya pamoja na Mwakilishi wa FAO nchini humo Farai Zemoudzi.