#HABARI: Naibu Waziri wa Katiba na Sheria wa sasa ni Mhe. Zainab Athuman Katimba (Mb.), ameitaka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania kutekeleza mipango waliyojiwekea kwa kuzingatia matumizi yenye tija, nidhamu ya bajeti, uwajibikaji na kuendelea kuimarisha taswira nzuri ya Tume mbele ya Serikali na wadau wake.

Ameitaka Tume hiyo kutambua kuwa inao wajibu mkubwa kuhakikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inatekelezwa na kufikia matokeo yaliyotarajiwa, kama alivyoelekeza Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa uzinduzi wa Dira hiyo, kuwa Tume ina jukumu muhimu la kufanya tafiti, mapitio na tathmini za Sheria ili kubaini na kurekebisha Sheria zinazoweza kukwamisha utekelezaji wa Dira 2050.

Naibu Waziri Katimba ametoa maelekezo hayo wakati akifungua mkutano wa 24 wa baraza la wafanyakazi wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Utumishi wa Mahakama Jijini Dodoma leo tarehe 14 Mei 2026.

Amesema ni wazi kuwa bila sheria bora, zinazokwenda sambamba na mahitaji ya wakati, utekelezaji wa Dira hiyo hautafikia mafanikio yaliyokusudiwa, hivyo ni muhimu kushirikiana kwa nguvu zote kuisaidia Serikali na taasisi zake kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo
2050.

“Niwasihi tuongeze bidii na kutekeleza majukumu yetu ipasavyo ili ongezeko hili lionyeshe tija na kufikia malengo ya Serikali ya kuongeza wigo husika wa Bajeti kwa Tume hasa katika kipindi hiki tunachoanza kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” ameeleza Mhe. Katimba.

Ameongeza kuwa Wizara ya Katiba na Sheria inaridhishwa na utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Tume kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ambapo Tume imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa katika kuimarisha mfumo wa sheria nchini.

(Feed generated with FetchRSS)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *