Dar es Salaam. Baada ya shauri la usajili wa chama kipya cha siasa, The Independent People’s Party (IPP) kukwama mara mbili kuanza usikilizwaji katika hatua za awali kutokana na kutokupangiwa jaji, Hatimaye sasa shauri hilo limepangiwa jaji atakayelisikiliza.

Kwa sasa shauri hilo la mapitio ya kimahakama lililofunguliwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, limepangwa kusikilizwa na Jaji Arnold Kirekiano.

Shauri hilo lilifunguliwa Februari 4, 2026 na waanzilishi wa chama hicho, Vyonheaven Exaud Urima na Fadhili Andrew Bomani kwa msaada wa Kituo cha Msaada wa Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

Wamefungua shauri hilo dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), wakiiomba mahakama imlazimishe Msajili kushughulikia maombi ya usajili wa chama chao hicho.

Awali, lilipangwa kusikilizwa na Jaji aliyeruhusu lifunguliwe, Obadia Bwegoge na lilipangwa kutajwa kwa mara ya kwanza kwa ajili ya maelekezo maalumu Aprili 13, 2026.

Tarehe hiyo shauri hilo liliitwa kwa Naibu Msajili wa mahakama hiyo, ambaye aliwaeleza wadaawa kuwa Jaji Bwegoge aliyekuwa amepangiwa kusikiliza shauri hilo alikuwa amehamishwa. Hivyo lilipangwa kutajwa Mei 4, 2026.

Mei 4, 2026 shauri hilo lilipotajwa tena wadaawa waliarifiwa shauri halikuwa  limepangiwa Jaji mwingine, hivyo liliahirishwa tena hadi Mei 20, 2026 kusubiri kupangiwa jaji atakayelisikiliza.

Hata hivyo, wakili wa wadai hao, Rose Omuga kutoka LHRC, amelieleza Mwanachi leo Alhamisi, Mei 14, 2026 kuwa mfumo mahakama wa usajili na usimamizi wa mashauri, unaonyesha limepangwa kwa Jaji Kirekiano.

Chanzo cha shauri

Kwa mujibu wa nyaraka zilizowasilishwa mahakamani na wadai (hati ya maelezo na hati ya kiapo) mchakato wa usajili wa chama hicho kipya cha siasa cha IPP ulianza Mei 3, 2023, waombaji walipowasilisha fomu maombi ya usajili kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Juni 8, 2023, Msajili aliomba nyaraka za ziada, zikiwemo nakala laini za katiba ya chama, uthibitisho wa uraia wa waombaji wa awali, bendera ya chama na vyeti vya kuzaliwa vya waanzilishi wawili.

Nyaraka nyingine zilikuwa ni uthibitisho wa uraia wa mzazi mmoja wa kila mwanzilishi wa awali na vielelezo vya malipo ya ada ya usajili.

Licha ya kutekeleza maelekezo hayo, baadaye Novemba 2, 2023 na Machi 4, 2024, Msajili alitoa barua nyingine akiibua mahitaji mapya, mengi ambayo kwa mujibu wa waombaji yalikuwa tayari yametekelezwa.

Mahitaji hayo mapya yalihusisha sera ya chama, uthibitisho wa uraia, nakala zinazoonekana vizuri za vyeti vya kuzaliwa vya waombaji (Urima na Bomani) pamoja na fomu za maombi ya usajili (PP1 na PP2) zilizo wazi na zinazoonekana vizuri.

Pia alihitaji taarifa za ofisi za chama, maelezo kuhusu pengo lililoonekana katika wasifu (CV) wa mmoja wa waombaji pamoja na ufafanuzi wa tofauti za majina.

Licha ya kuendelea kutekeleza matakwa yote yaliyotolewa, waombaji wanadai kuwa tangu hapo Msajili amekuwa kimya bila kutoa mrejesho wowote wa ama kukubali au kukataa maombi yao.

Kutokana na hali hiyo, wadai kupitia LHRC waliandika barua tatu rasmi za ufuatiliaji Machi 6, Mei 18 na Septemba 4, 2024, zikifuatiwa na barua ya kumbusho la mwisho ya Novemba 13, 2024. Barua zote zilipokewa, lakini hakuna hata moja iliyojibiwa.

Hivyo Aprili 11, 2025, wadai (waombaji) hao walifungua shauri wakiomba ridhaa kufungua shauri la mapitio ya mahakama, kutokana na mwenendo huo wa Msajili na Januari 22, 2026 Mahakama hiyo iliridhia maoambi hayo na ikawaruhusu kufungua shauri hilo ndani ya siku 14.

Misingi ya kisheria ya madai

Wadai wanadai kuwa mwenendo wa Msajili unakiuka wajibu wake kisheria kikatiba na kanuni za haki za asili.

Kisheria wanabainisha kuwa msajili amekiuka vifungu vya 8 na 9 vya Sheria ya Vyama vya Siasa [Sura ya 258 Marejeo ya 2023].

Kikanuni wanadai kuwa amekiuka kanuni ya 4(c) ya Kanuni za Vyama vya Siasa (Usajili na Ufuatiliaji), 2019 (Tangazo la Serikali Na. 953 la mwaka 2019) inayomtaka Msajili kutoa uamuzi kuhusu usajili wa muda ndani ya siku 30 tangu kupokea ombi lililokamilika.

Kikatiba ni ibara za 20(1), haki ya uhuru wa kujiunga na vyama, kuunda chama cha siasa; 21(1), kushiriki katika shughuli za umma moja kwa moja au kupitia wawakilishi waliochaguliwa kwa hiari na 13(6)(a), kupata utekelezaji wa hatua za kiutawala zilizo za haki na uwazi.

Wanadai kuwa kwa kushindwa kutoa sababu za kucheleweshwa kwa muda mrefu au kutoa uamuzi rasmi, Msajili anakwenda kinyume na kanuni za haki asilia, anAkiuka matarajio yao na kuwanyima haki ya usikilizwaji wa haki.

Waombaji hao wanadai kuwa jambo hilo limewaathiri kwa kuwazuia kufurahia kikamilifu haki zao za kisiasa kama zinavyotolewa chini ya Ibara ya 13(6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba wamepata madhila makubwa na mateso ya kiakili.                                         

Hivyo, wanadai kuwa hakuna chombo kingine cha kiutawala au kisheria ambacho wanaweza kuwasilisha malalamiko yao, na kwamba mapitio ya kimahakama ndiyo njia pekee inayopatikana kurekebisha kutotekelezwa kwa wajibu na Msajili.

Wanadai kuwa maombi yao yasipokubaliwa, watapoteza haki yao ya kushiriki kikamilifu katika siasa za nchi; hasara isiyorekebishika ikilinganishwa na hasara ambayo walalamikiwa wataipata iwapo maombi haya yatatolewa.

Majibu ya wajibu maombi

Wadaiwa katika majibu yao ya maandishi wamedai kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kutoa amri inayoombwa, kumlazimisha Msajili kutoa cheti cha usajili wa muda kwa chama hicho.

Wanadai kuwa wadai hawajatimiza masharti na vigezo vya usajili huo vilivyowekwa katika Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 Marejeo ya 2023, na Kanuni za Vyama vya Siasa (Usajili na Ufuatiliaji) za mwaka 2019, Tangazo la Serikali Na. 953 la mwaka 2019.

Hivyo, wanadai kuwa Msajili hajafanya kitendo chochote kinachokiuka kanuni za haki za asili, Sheria na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wala hajawanyima waombaji haki zao kama zilivyoainishwa katika ibara ya 13(6) ya Katiba.

Pia wanadai kuwa Msajili hajatoa uamuzi wowote wenye maana kwamba chama chao hakiwezi kusajiliwa, huku wakidai kuwa chama hicho kinaweza kusajiliwa tu pale maombi husika yatakapokidhi masharti na vigezo vya sheria zinazosimamia usajili wa vyama vya siasa nchini.

Katika mbadala wake, wanadai kuwa waombaji hawajaambatisha ushahidi wowote kuthibitisha kwamba wamepata madhila makubwa yasiyoelezeka wala maumivu ya kiakili.

Kwa sababu hizo wanadai kuwa hakuna sababu za msingi zilizotolewa kuiwezesha Mahakama kutoa amri zinazo ombwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *