Kinyume na madai ya maafisa wa serikali ya Marekani wanaochochea vita, akiwemo Rais Donald Trump, vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti, vikinukuu tathmini za siri, kwamba Iran bado ina uwezo mkubwa wa makombora.

New York Times imeandika kwamba madai ya Donald Trump kuhusu kudhoofisha vikosi vya jeshi vya Iran si sahihi kabisa, kwa mujibu wa tathmini za siri za Marekani zilizotolewa mapema mwezi huu.

Tathmini hizo zinaonyesha kwamba, kiutendaji, Iran ina maeneo 30 kati ya 33 ya makombora kando ya Mlango Bahari wa Hormuz, ambayo yanaweza kuwa tishio kwa meli za kivita za Marekani na meli za mafuta zinazopita kwenye njia hiyo nyembamba ya majini.

Tathmini hizo za siri zinasema, Iran bado ina takriban asilimia 70 ya mitambo tamba ya kurushia makombora iliyosambazwa kote nchini na imehifadhi takriban asilimia 70 ya akiba yake ya makombora kabla ya vita.

Wakati huo huo, wataalamu wenye maarifa na masuala hayo wanasema kwamba, kwa mujibu wa taarifa kutoka vyanzo vingi, ikiwa ni pamoja na picha za satalaiti na teknolojia zingine za ufuatiliaji, Iran bado ina takriban asilimia 90 ya vituo vyake vya kuhifadhi na kurusha makombora ya chini ya ardhi kote nchini, ambavyo vinafanya kazi kikamilifu.

Wakati huo huo, CNN imeripoti kwamba kuendelea kufungwa Mlango-Bahari wa Hormuz kumesababisha kupungua kwa kasi akiba ya mafuta ya dharura ya Marekani.

Ripoti hiyo inasema, utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump unapunguza akiba ya mafuta ya dharura ya nchi hiyo kwa kiwango kisicho cha kawaida. Kwa mujibu wa data iliyotolewa Jumatano, Hifadhi ya Mafuta ya Kimkakati ya Marekani ilishuka kwa mapipa milioni 8.6 wiki iliyopita, ikiwa ni kupungua kwa kiwango kikubwa zaidi tangu miaka ya 1980.

Sambamba na hayo, Kiongozi wa Wachache katika Seneti ya Marekani, Chuck Schumer pia ametangaza kwamba Rais Donald Trump amepoteza dola bilioni 29 pesa za nchi hiyo katika vita visivyo na maana dhidi ya Iran.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *