Dar es Salaam. Wakati Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ikikitaka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kujieleza kwa nini kisisimamishiwe usajili kufuatia kauli za viongozi wake, wadau wa demokrasia wameishukia ofisi hiyo wakieleza kwamba hatua hiyo ni tishio dhidi ya demokrasia nchini.

Barua ya Msajili iliyosainiwa na Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza kwenda kwa Katibu Mkuu wa Chadema Mei 7, 2026, inaeleza kwamba Chadema imekiuka Katiba na sheria kwa viongozi wake kutoa maoni kwa lugha za kashfa, dhihaka na uchochezi.

Msajili ameeleza katika barua hiyo kwamba Ibara ya 20 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inaruhusu Watanzania kuanzisha vyama vya siasa na kutoa maoni yao bila kukiuka sheria za nchi.

Hata hivyo, amesema chama cha siasa kutoa maoni kwa lugha za kashfa, dhihaka na uchochezi ni ukiukwaji wa Katiba na sheria za nchi ambao haupaswi kuwepo, kwa sababu chama cha siasa kina uwezo wa kuwasilisha ujumbe wake bila ya kukiuka sheria.

Msajili amezingatia kifungu cha 7 cha Sheria ya Vyama vya Siasa, kifungu cha 39(2)(a) cha Sheria ya Vyama vya Siasa kama kilivyorekebishwa na kifungu cha 19 cha Sheria Namba 3 ya mwaka 2024 na kifungu cha 45 cha Sheria ya Vyama vya Siasa kama kilivyorekebishwa na kifungu cha 21 cha sheria hiyo.

“Msajili wa Vyama vya Siasa anawataka Chadema muwasilishe maelezo kwa nini usajili wa chama chenu usisimamishwe au chama chenu kutozwa faini kwa kukiuka masharti ya Sheria ya Vyama vya Siasa, ikiwemo masharti ya usajili.

“Maelezo yenu yawasilishwe Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa si zaidi ya Mei 20, 2026 saa tisa na nusu alasiri. Nimekutumia video hizo kwa njia ya barua pepe ya chama na yako binafsi na WhatsApp,” inasomeka sehemu ya barua hiyo kwenda kwa Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika.

Katika barua hiyo, Msajili amenukuu kauli mbalimbali zilizotolewa na viongozi wa Chadema akiwamo Makamu Mwenyekiti Bara, John Heche, Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Korogwe Mkoa wa Tanga, Oliver Kisaka pamoja na sehemu za taarifa iliyotolewa baada ya kikao cha Kamati Kuu, akidai zimekiuka Katiba na sheria.

Alipotafutwa kuzungumzia barua hiyo, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika hakuwa tayari kuzungumzia barua hiyo ya msajili akielekeza atafutwe Msajili mwenyewe, kauli inayofanana na aliyoitoa jana, alipodokeza kuhusu jambo hilo.

Wadau wamshukia

Kutokana na barua hiyo, wadau mbalimbali wa demokrasia wamejitokeza na kulaani hatua hiyo ya Msajili, wakieleza kuwa ni njama ya kutaka kukifuta chama hicho, jambo ambalo ni tishio kwa demokrasia nchini Tanzania.

Kiongozi wa zamani wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amesema zama za Ofisi ya Msajili wa Vyama kuwa mchezaji namba 12 wa Chama cha Mapinduzi (CCM) zimekwisha, hivyo asijaribu kukifuta chama hicho.

“Tume ya Chande iliyoundwa na Rais imetoa taarifa inayosema wananchi wanailalamikia Ofisi ya Msajili kutokutenda haki kwenye kusimamia shughuli za vyama vya siasa. Badala ya Msajili kuchutama, kuwajibika na kubadilika, anarudia makosa yaleyale yaliyopelekea mauaji yaliyoanza Oktoba 29, 2025.

“Ofisi ya Msajili ijue Watanzania sio mabwege. Tunachukulia tishio lolote dhidi ya Chadema ni tishio dhidi ya demokrasia. An attack to one, is an attack to all (shambulizi dhidi ya mmoja ni shambulizi kwa wote),” ameandika Zitto kwenye ukurasa wake wa X.

Zitto ameitaka Ofisi ya Msajili pamoja na vyombo vingine vya dola kuacha kukibeba chama tawala, badala yake waache siasa zifanyike kwa mujibu wa Katiba na sheria.

Ameongeza kuwa wakiendelea kufanya hivyo nao wataanguka.

Maoni ya Zitto hayako mbali na ya Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi ambaye amesema Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa idhibitiwe kabla haijasababisha maafa kwa mara ya pili.

Amesema Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ndiyo chemichemi ya vurugu za kidemokrasia ndani ya vyama vya upinzani na ina mchango mkubwa katika vurugu za Oktoba 29.

“Kimsingi Tume ya Uchaguzi na Ofisi ya Msajili kwa matendo au kutowajibika kwao, zimesababisha kwa asilimia zaidi ya 60 mauaji ya Oktoba 29, 2025.

“Baadhi ya maofisa wake kwa makusudi, kujipendekeza au kutumika wana mchango mkubwa katika kuharibu haki, amani, umoja, utulivu wa kidemokrasia ndani ya vyama vya siasa na ustahimilivu wa kidemokrasia,” ameandika Mwabukusi katika ukurasa wake wa X.

Mwabukusi ameongeza kwamba ofisi hiyo inafanya na kutenda kwa kuzingita uonevu, ubaguzi, hila na inaongoza kwa matumizi mabaya ya mamlaka.

“Tunaweza tukalaumu vyombo vingine vya kusimamia sheria kama Polisi, Jeshi, Mahakama na vyombo vingine vya ulinzi, ila tusisahu kuwa kinu kinachofua na kuandaa hila, fitina na machafuko ni Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambayo imeacha kazi ya kusajili vyama na imejigeuza ofisi ya kuvuruga utulivu ndani ya vyama na kuminya uhuru wa kidemokrasia na ushiriki mpana wa vyama vya siasa,” amesema.

Makamu Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi Bara, Joseph Selasini amedai ofisi ya Msajili ni ofisa wa Serikali na uamuzi huo ameagizwa na wakubwa ili kukidhibiti Chadema.

Amesema Serikali inaimba habari za maridhiano, lakini huwezi kufanya maridhiano na mtu ambaye anakuchekea usoni lakini moyoni amejaa chuki.

“Msajili ambaye anatakiwa kuwa mlezi wa vyama, ndiye anavibomoa. Maandamano ni haki ya vyama vya siasa, yameruhusiwa kikatiba na kisheria, kwa hiyo sioni kama ni kosa kwa kiongozi wa Chadema kusema wataitisha maandamano.

“Suala la kushikiliwa kwa Tundu Lissu (Mwenyekiti wa Chadema) linamkera kila mtu. Msajili anataka Chadema wasiwe na uchungu kwa mwenyekiti wao kushikiliwa kwa siku 399. Msajili anataka watu wote wanaompenda Lissu wawe wanachekelea Mahakama inavyomzungusha?” amehoji.

Ameongeza. “nadhani bado Serikali haijajifunza kwa kile kilichotokea mwaka jana, mimi nashauri waachane na Chadema kifanye kazi yake.

“Kuitikisa Chadema ni kuitikisa nchi. Tumechoka kuona damu za watu zikimwagika. Chadema imetoa kauli tu, amewaandikia barua, kwanini asisubiri aone, maandamano yana taratibu zake,” amesema.

Mbali na hao, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Conrad Masabo amesema suala la Msajili kuvitaka vyama kujieleza ni utamaduni uliozoeleka kwa vyama vya upinzani, lakini ofisi hiyo hajawahi kuitaka CCM kujieleza kama ambavyo amekuwa akifanya kwa vyama vya upinzani.

Dk Masabo amesema katika nadharia ya udhibiti wa vyama, Msajili amechukua hatua hiyo ili kukidhibiti chama hicho ambacho kilikuwa kifungoni kwa muda mrefu na sasa kimeanza kufanya siasa zake.

“Chama kilichokuwa kifungoni kikija na makeke, lazima watawala watikisike, na ndiyo hao wanaitumia Ofisi ya Msajili kukipunguza makali,” amesema mwanzuoni huyo.

Katika nadharia nyingine, amesema imezoeleka kwamba Ofisi ya Msajili imekuwa ikivikandamiza vyama vya upinzani hasa vile vikubwa vinavyokubalika kwa wananchi, ili kupunguza nguvu yao.

“Hii barua ni mwendelezo wa uonevu wa Ofisi ya Msajili dhidi ya vyama vya upinzani. Sidhani kama wamefanya jinai kwa sababu kama ingekuwa ni jinai, polisi wangekuwa wamewakamata,” amesema Dk Masabo.

Hata hivyo, amesema anaamini Chadema wakitoa maelezo yao, Msajili atafanya uamuzi na kisha atatoa adhabu kulingana na kosa husika.

MsajiIi afafanua

Msajili Msaidizi, Sisty Nyahoza amefafanua kwamba ni kweli waliwaandikia Chadema barua Mei 7, 2026 kwa sababu kauli za viongozi wao hususani Heche kutaka kuitisha maandamano kushinikiza Lissu kutolewa, zinakiuka sheria.

“Mtu akiwa mahakamani, unachotakiwa ni kufuata utaratibu wa kimahakama ili mahakama itoe uamuzi, huwezi ukakaa barabarani unaishinikiza mahakama itoe uamuzi in your favor (kwa kukupendelea), hiyo ni ukiukwaji wa sheria,” amesema Nyahoza.

Ameongeza kwamba Mwenyekiti wa Chadema Korogwe naye alinukuliwa akiwapongeza watu waliofanya vurugu Oktoba 29 wakipigania haki zao, jambo ambalo amesema ni uchochezi kwani haki inatafutwa kwa njia za mazungumzo.

“Sheria yetu inakataza kutumia lugha za matusi, dhihaka, kashfa na kuchochea watu kufanya vurugu katika kutafuta haki zao. Kwa hiyo, tumewaambia hilo tamko lao limetumia lugha mbaya zinazokiuka sheria,” amesema.

Nyahoza ameongeza kwamba wamekitaka chama hicho kujieleza kabla ya mei 20, wakiona maelezo yao hayajitoshelezi watachukua hatua kwa mujibu wa sheria.

“Kwenye barua yetu tumewaambia kwamba kwa uzito wa kosa hili, tusiporidhika na maelezo yao tutawasimamishia usajili kwa muda tutakaoona unaofaa, au kuwatoza faini au vyote viwili,” amesema Nyahoza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *