Dar es Salaam. Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imeandika historia mpya katika huduma za afya nchini baada ya madaktari bingwa wa hospitali hiyo kufanikiwa kufanya upandikizaji wa figo kwa wagonjwa wanne kwa kutumia teknolojia ya upasuaji wa njia ya tundu dogo, maarufu laparoscopic surgery.

Dk Emanuel Minja, Mtanzania anayefanya kazi nchini Marekani na mtaalamu bingwa wa upasuaji wa upandikizaji figo kwa njia ya tundu dogo, ndiye aliyeongoza jopo la madaktari wa Muhimbili katika utekelezaji wa upasuaji huo.

Mafanikio hayo yanatajwa kuwa hatua kubwa katika maendeleo ya tiba za kibingwa nchini kutokana na uwezo wa teknolojia hiyo kupunguza madhara ya upasuaji kwa wagonjwa na wachangiaji wa figo, huku ikiongeza ufanisi wa huduma za matibabu.

Kwa kutumia vifaa maalumu vya kisasa, madaktari walifanya upasuaji huo kwa usahihi mkubwa bila kufungua sehemu kubwa ya mwili kama ilivyo katika upasuaji wa kawaida.

Mbinu hiyo imeelezwa kusaidia kupunguza maumivu baada ya upasuaji, kupunguza kiwango cha damu kinachopotea pamoja na kufupisha muda wa mgonjwa kukaa hospitalini.

Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, leo Mei 14, 2026 daktari bingwa wa upandikizaji figo wa MNH, Dk Jonathan Mgumi, amesema matumizi ya teknolojia hiyo ni hatua muhimu katika kuimarisha huduma za upandikizaji figo nchini.

Amesema wagonjwa pamoja na wachangiaji wa figo wanaofanyiwa upasuaji kwa njia hiyo hupata nafuu kwa haraka zaidi ikilinganishwa na upasuaji wa kawaida unaohusisha kufungua sehemu kubwa ya mwili.

“Teknolojia hii imeongeza usalama kwa wachangiaji wa figo kwa sababu wanapona mapema na kurejea katika shughuli zao za kila siku kwa muda mfupi zaidi. Hii ni hatua kubwa katika kuboresha huduma za kibingwa hapa nchini,” amesema Dk Mgumi.

Ameongeza kuwa Muhimbili itaendelea kuwekeza katika matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ndani ya nchi badala ya kusafiri nje kutafuta matibabu ya gharama kubwa.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, ongezeko la wagonjwa wa figo nchini linahitaji uwekezaji mkubwa katika huduma za kibingwa na vifaa tiba vya kisasa ili kukabiliana na changamoto hiyo inayoongezeka kila mwaka.

Kwa upande wa Dk Minjua amesema  “Njia hii inasaidia kupunguza maumivu, kupunguza muda wa kupona na pia inapunguza uwezekano wa madhara yanayoweza kujitokeza baada ya upasuaji. Hii ni teknolojia inayotumika katika hospitali kubwa duniani na sasa Watanzania wanaanza kunufaika nayo hapahapa nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *