
Mbeya. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, linawashikilia watu saba kwa tuhuma za kujipatia Sh81 milioni kwa njia za udanganyifu wa kutoa ajira kwa vijana 80, kupitia kampuni ya Q Net na Global Alliance.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema watuhumiwa hao wamekamatwa leo Alhamisi Mei 14,2026, kwenye msako uliofanywa katika maeneo mbalimbali jijini hapa.
Amesema watuhumiwa walikuwa wakijipatia fedha kwa njia za udanganyifu na kuwarubuni vijana kuwapa ajira kupitia Kampuni ya Q Net na Global Alliance.
“Watuhumiwa walikuwa wakiwashawishi vijana watoe kiasi cha Sh40,000 hadi Sh5 milioni kwa lengo la kuwapatia ajira katika kampuni hiyo,”amesema.
Amesema kufuatia udanganyifu huo zaidi ya vijana 80 waliingia kwenye mtego na kukusanywa katika nyumba tofauti maeneo ya Iwambi, Shewa, Isyesye na Iyunga halmashauri ya Jiji la Mbeya.
Kuzaga amewataja watuhumiwa hao ni Willam Hamis, Tyson Lubida, Onesmo Haldphonce, Charles Masanja, Chemka Mwanyanga, Gracia Ephrahim, wote wakati wa jijini hapa na Ezekiel Mgogo mkazi wa Igunga Mkoa wa Tabora.
“Watuhumiwa walitumia mbinu ya kuwarubuni vijana kutoka mikoa mbalimbali kuwaleta mkoani hapa kwa lengo kuwapatia ajira jambo ambalo sio sahihi na kupelekea kuishi maisha ya shida kwa kukosa huduma,” amesema.
Wakati huohuo, Kamanda Kuzaga amewaonya vijana kuepuka kutafuta ajira kwa kutakiwa kutanguliza fedha na badala yake watumie mifumo rasmi .
“Vijana mnaotafuta ajira msikubali kutoa fedha ili kupata ajira kwani hakuna utaratibu huo na badala yake kutoa taarifa kwa vyombo vya dola ili kujinasua kwenye mitego,” amesema.
Kauli za wananchi
Mkazi wa Ituha jijini hapa, Aminael Petro amesema tabia hizo hazijaanza leo vijana wamekuwa wakizagaa mitaani kwa kukosa mahitaji muhimu.
“Tumeona hii kampuni ni shida wanaita vijana kutoka mikoa mbalimbali kwa madai ya kuwapa ajira, lakini mwisho wa siku ni changamoto kwani wanazagaa mitaani, “amesema.