
Katika taarifa ya pamoja, ya mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa lile la Chakula na Kilimo FAO na la Mpango wa Chakula Duniani WFP yamesema karibu mtu mmoja kati ya wanne nchini humo anakabiliwa na viwango vya njaa vya dharura, huku zaidi ya watu milioni 3.6 wakiwa tayari katika hali mbaya inayotishia maisha yao.
Mashirika hayo yameeleza hali hiyo kuwa moja ya migogoro mikubwa na mibaya zaidi ya njaa duniani. Yamesema mapigano yanayoendelea katika majimbo ya mashariki mwa DRC kama Kivu Kaskazini, Kivu Kusini, Ituri na Tanganyika yamesababisha familia kuhama makazi yao, kuharibu maisha yao na kuvuruga shughuli za kilimo.
Mamilioni wahama makazi huku bei za chakula zikipanda
Kwa mujibu wa mashirika hayo, zaidi ya watu milioni 7.8 wameyakimbia makazi yao ndani ya nchi, wengi wao wakipoteza mashamba, mifugo na vyanzo vya mapato.
Hali ya kibinadamu nchini humo imeendelea kuzorota kutokana na kupanda kwa bei za chakula, kuvurugika kwa usafirishaji wa bidhaa pamoja na milipuko ya mara kwa mara ya magonjwa ya kipindupindu, surua na Mpox.
Wahudumu wa misaada wameonya kuwa jamii ambazo tayari ni dhaifu zinakaribia maafa makubwa zaidi huku ukosefu wa usalama ukizuia upatikanaji wa misaada kwa wahitaji wengi.
Watoto na akina mama wakikabiliwa na utapiamlo wa kutisha
Ripoti hiyo pia imeonesha hali mbaya ya lishe, hasa kwa watoto na wanawake wajawazito pamoja na wanaonyonyesha. Takriban watoto milioni 4.18 walio chini ya umri wa miaka mitano wanatarajiwa kuhitaji matibabu ya utapiamlo mkali kati ya Januari na Juni mwaka 2026.
Kati yao, zaidi ya watoto milioni 1.3 wanatarajiwa kuugua unyafuzi ambao unaweza kusababisha vifo ndani ya wiki chache iwapo hautatibiwa. Aidha, zaidi ya wanawake milioni 1.5 wajawazito na wanaonyonyesha wanatarajiwa kukumbwa na utapiamlo mkali, hali inayoongeza hatari kwa afya ya mama na mtoto.
“Kila msimu wa kilimo unaopotea unaongeza utegemezi wa misaada ya kibinadamu,” amesema Athman Mravili Mratibu wa Kikanda wa FAO. “Familia zinapopata mbegu, zana na msaada wa haraka wa kujikimu, zinaweza kuzalisha chakula ndani ya wiki chache, kulinda heshima yao na kuepuka kuzama zaidi kwenye njaa. Lakini msaada huo lazima ufike kabla ya misimu ya upandaji kufungwa.”
Mashirika ya misaada yaonya kuhusu upungufu mkubwa wa fedha
FAO imesema tayari inasaidia zaidi ya familia 55,500 zilizoathiriwa na mgogoro mashariki mwa DRC kupitia dola milioni 10 kutoka Mfuko wa Kibinadamu wa DRC.
Msaada huo unajumuisha mbegu, vifaa vya kilimo, msaada wa kujikimu na fedha taslimu ili kusaidia familia kurejesha uzalishaji wa chakula na kupunguza utegemezi wa misaada ya chakula. Hata hivyo, shirika hilo limesema linahitaji haraka dola milioni 163 zaidi ili kupanua wigo wa msaada huo kabla ya misimu muhimu ya upandaji kupita.
Wakati huo huo, WFP imesema msaada wake wa chakula na fedha taslimu umefikia karibu watu milioni 1.3 tangu Januari 2026, idadi ambayo ni ndogo ikilinganishwa na mahitaji yaliyopo. Shirika hilo limeongeza kuwa watoto na akina mama 389,000 pekee walipata msaada wa lishe kati ya Januari na Machi, kiwango ambacho kiko chini sana ya mahitaji halisi.
Aidha, WFP inakabiliwa na pengo la ufadhili la dola milioni 214 hadi Oktoba mwaka huu, hali inayozuia zaidi juhudi za misaada.
Wito wa hatua za haraka za kimataifa
Mashirika ya misaada sasa yanatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza msaada wa haraka ili kuzuia mgogoro huo kuzidi kuwa mbaya zaidi. Yamesisitiza kuwa msaada wa dharura wa chakula pekee hautoshi bila uwekezaji wa muda mrefu katika kilimo, maisha ya wananchi na mifumo imara ya chakula.
“Badala ya kupungua, mgogoro huu umejikita zaidi na kuwa mgumu zaidi, ukinasa mamilioni ya kaya zilizo katika mazingira magumu kwenye mzunguko wa mahitaji ya kudumu,” amesema David Stevenson afisa wa WFP nchini DRC. “Misaada ya kibinadamu ni tegemeo muhimu la maisha, lakini lazima iongezwe haraka ili kukidhi ukubwa wa mahitaji. Zaidi ya msaada wa dharura, uwekezaji endelevu katika mifumo imara ya chakula na suluhisho jumuishi ni muhimu kusaidia jamii kukabiliana na mishtuko na kuelekea katika ahueni.”