Katika ujumbe wake alioutoa leo akiwa Geneva Uswisi, Dkt. Tedros amesema zaidi ya watu 120 kutoka mataifa 23 waliteremshwa salama kutoka melini na sasa wanapatiwa uangalizi wa afya katika nchi zao.
Mshikamano ndio kinga bora
Amesema hatua hiyo imeonesha namna sayansi na mshikamano vinavyoweza kufanya kazi pamoja wakati wa dharura. “Kinga bora zaidi tuliyonayo ni mshikamano, Tenerife imethibitisha hili, si kama kauli pekee bali kama namna ya kufanya kazi na kuishi.” Amesema Dkt. Tedros
Aidha amesema wananchi wa Tenerife walionesha “ujasiri wa kimaadili” kwa kuwakaribisha watu waliokuwa katika hofu na sintofahamu badala ya kuwageuka. “Hawa ni binadamu, na hatutawapuuza,” amesema akielezea msimamo wa jamii hiyo.
Mkuu huyo wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani pia ametuma salamu za rambirambi kwa familia za watu watatu waliofariki ndani ya meli ya Hondius pamoja na mwanausalama mmoja wa Tenerife aliyefariki kwa mshtuko wa moyo alipokuwa akihudumu katika operesheni hiyo.
Virusi vya hanta ugonjwa wa virusi unaosambazwa zaidi kupitia panya walioambukizwa na unaweza kusababisha matatizo makubwa ya mfumo wa upumuaji na figo.
Kufahamu zaidi kuhusu ugonjwa huo bofya hapa