WENGI hatukutegemea Yanga ipoteze mechi dhidi ya Dodoma Jiji FC juzi Jumatano kule Singida kwenye Uwanja wa Airtel.

Na hii ni kwa sababu ya utamaduni ambao tumekuwa nao kwamba timu kubwa hazitakiwi kupoteza mechi dhidi ya timu ndogo hata zikiwa hazipo vizuri.

Hii dhana ndio inafanya wakati mwingine hata marefa waharibu mechi kwa sababu tu ya kulazimisha timu kubwa kwenye ligi yetu zisiangushe pointi tatu kwenye mechi ambazo zinaonekana kabisa kuwa zinaweza kupoteza.

Lakini hii ni tofauti kwa wenzetu ambao wala sio jambo geni kwa timu kubwa kupoteza dhidi ya timu ndogo pale mambo yanapoigomea ndani ya dakika 90 kwa sababu wanafahamu kuwa hilo linaleta ushindani wa kweli.

Hapa Kijiweni tunaamini kwamba matokeo kama ya juzi baina ya Dodoma Jiji na Yanga ni jambo ambalo linapaswa kuonekana la kawaida badala ya kutazamwa kama moja ya maajabu kwenye soka letu.

Kuna namna fulani matokeo ya namna ile yanatoa fundisho kwa timu kuwa timu kubwa hakumaanishi kwamba unaweza kupata ushindi kirahisi hata kama hujacheza mechi vizuri na kuwa timu ndogo hakumaanishi kwamba utapoteza tu mechi dhidi ya timu kubwa hata ukicheza vizuri.

Kwa upande mwingine ni matokeo ambayo yamezidi kunogesha ligi yetu kwani yamefanya mbio za ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu kubaki kuwa wazi kwa timu tatu zilizo juu kwenye msimamo wa ligi. Kwa hali inavyoonekana, upo uwezekano ubingwa wa ligi msimu huu ukaamriwa katika dakika za jioooooni na sio bingwa kupatikana huku akiwa na mechi kibao mkononi.

Ni raundi saba za moto zimebaki kazi ipo kwa farasi watatu wa mbio za ubingwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *