Morogoro. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Andrew Kantimbo amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa dereva wa bodaboda aliyeuawa na watu wasiojulikana, Ally Kambi (24) alichomwa na kitu chenye makali juu ya jicho la kushoto na kuvuja damu nyingi kulikosababisha kifo chake.
Kwa mujibu wa taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari, Kamanda Kantimbo amesema baada ya kufanya mauaji, watu hao waliutelekeza mwili kwenye shamba la mkonge lililopo Kata ya Mkambarani Wilaya ya Morogoro.
Kamanda Kantimbo amesema kwa sasa Polisi wanafanya uchunguzi kubaini waliohusika na mauaji hayo ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria, hivyo amewaomba wananchi kushirikiana na jeshi hilo kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa watuhumiwa.
Kwa upande wake, mjomba wa marehemu, Ahmed Ramadani amesema tayari mwili wa marehemu umezikwa kwenye makaburi ya Sheikh Athuman na kwa sasa suala hilo wanaliachia Jeshi la Polisi.
“Sisi kama familia tuna imani kubwa na Jeshi la Polisi katika kuchunguza tukio hili, hivyo kwa sasa tunaliachia lifanye kazi hiyo na watatupa taarifa ya kila hatua watakayofikia,” amesema Ramadhani.
Awali, baba mdogo wa marehemu, Shukuru Msonga amesema kijana wao alitoweka nyumbani Mei 11, 2026 akiwa na pikipiki na hakuonekana hadi Mei 13, 2026 mwili wake ulipoonekana kwenye shamba la mkonge.
Msonga amesema kabla ya kuupata mwili huo, jitihada zilifanyika kumtafuta ambapo walitoa taarifa Polisi na kwenye vijiwe vya bodaboda.
“Taarifa tulizozipata kutoka kwa wenzake wanadai Kambi alikodiwa na mtu mmoja ampeleke Mkambarani na ndiyo ilikuwa mara ya mwisho kuonekana. Pamoja na kumuua, watu hao walipora pikipiki, simu na fedha alizokuwa nazo,” amesema Msonga.
Amesema marehemu alianza kazi hiyo miaka michache iliyopita na alikuwa akiendesha bodaboda aliyokabidhiwa na rafiki yake kwa mkataba.