Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Aristides Mbwasi, amesema sera madhubuti ya ushindani imekuwa muhimu katika kuhakikisha biashara zinashindana kwa haki,

Kadri uchumi wa Tanzania unavyoendelea kukua, nchi iko katika mchakato wa kuimarisha mfumo wa ushindani wa kibiashara ili kuongeza ufanisi katika masoko, uhamasisha ubunifu na kutengeneza mazingira bora zaidi kwa uwekezaji endelevu.

Akuzungumza katika ufunguzi wa kongamano la sheria za ushindani na wawekezaji lililofanyika jijini Dar es Salaam. Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Aristides Mbwasi, alisema sera madhubuti ya ushindani imekuwa muhimu katika kuhakikisha biashara zinashindana kwa haki, watumiaji wanapata thamani ya fedha zao, na fursa zinabaki wazi kwa wawekezaji wa ndani na kigeni.

“Sera ya ushindani si suala la kiufundi au la pembeni tena. Sasa iko katikati ya mabadiliko ya kiuchumi,” alisema Mbwasi ambaye amemwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Sylvia Kapinga.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Khadija Ngasongwa akizungumza katika ufunguzi wa kongamano la sheria za ushindani na wawekezaji lililofanyika jijini Dar es Salaam Mei14, 2026

Aidha aliongezea akieleza kuwa wakati uchumi wa Tanzania ukiendelea kupanuka na kuunganishwa zaidi na masoko ya kimataifa, ni muhimu kuhakikisha ukuaji huo haujikusanyi kwa namna inayowaweka katika hasara wafanyabiashara wadogo.

Mbwasi aliipongeza Fair Competition Commission (FCC) pamoja na washirika wake kwa kuandaa kongamano hilo, akieleza kuwa limefanyika kwa wakati muafaka, wakati Tanzania ikikabiliana na changamoto mpya zinazohusiana na masoko ya kidijitali pamoja na ushirikiano katika uchumi kimataifa.

Ameeleza kuwa Tanzania inalenga kuwa na sheria ya ushindani itakayotoa mazingira ya biashara yenye uwazi na wezeshi, itakayoweza kuvutia wawekezaji huku ikihakikisha haki inatendeka kwenye masoko.

“Tanzania inataka kuwa na sheria za ushindani zinazotoa mazingira ya biashara yenye uwazi na yanayotabirika, ili wawekezaji waweze kufanya maamuzi yao kwa kujiamini,” alisema.

Hata hivyo, Mbwasi alifichua kuwa tangu mwaka 2007, FCC imepokea maombi 843 ya miunganiko ya kampuni (mergers) na kuyafanyia uchambuzi. Kati ya hayo, maombi 794 yaliidhinishwa moja kwa moja, huku 91 yakipewa masharti maalumu kabla ya kuidhinishwa.

Tume hiyo ilichunguza miunganiko kadhaa ambayo haikuwasilishwa rasmi na kutoa maamuzi manane ya mwisho. Huku kampuni saba zikipewa adhabu kwa kukiuka sheria.

Naye, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Khadija Ngasongwa, alisema sheria ya ushindani sasa inaangazia moja kwa moja namna kampuni zinavyoingia sokoni, kupanua biashara, kupanga bei na kushindana.

“Sheria ya ushindani si suala la udhibiti tu. Inaamua jinsi biashara zinavyoingia sokoni, jinsi zinavyokua na namna zinavyoshindana,” alisema.

Alisisitiza kuwa ufuataji wa sheria usionekane kama kikwazo kwa uwekezaji, bali kama nyenzo inayojenga imani kwa wawekezaji na kupunguza hatari za kibiashara.

“Uzingatiaji wa sheria ya ushindani huongeza imani ya wawekezaji na kusaidia kampuni kutambua hatari kabla hatua za utekelezaji wa sheria hazijachukuliwa,” alisema.

FCC pia ilitangaza mpango wa kuweka huduma zake kadhaa katika mfumo wa kidijitali, ikiwemo kuanzisha mfumo wa mtandaoni wa kuwasilisha maombi ya muunganiko wa kampuni pamoja mfumo wa kupokea malalamiko ya watumiaji. Hatua inayolenga kuongeza ufanisi na kurahisisha upatikanaji wa huduma za usimamizi wa ushindani.

Ngasongwa alimalizia kwa kueleza kuwa kongamano hilo linapaswa kuwa mwanzo wa mazungumzo na ushirikiano endelevu kati ya wadhibiti na sekta binafsi katika kuimarisha mazingira ya ushindani na uwekezaji nchini Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *