Siku ya Familia Duniani, huadhimishwa Mei 15 kila mwaka.
Familia ndiyo taasisi ya msingi katika ujenzi wa taifa, uchumi na maendeleo ya nchi yoyote duniani.

Akizungumza kupitia Mtandao wake wa kijamii wa X, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta binafsi (PPP-CENTRE) David Kafulila amesema moja ya changamoto zinazokabili familia nyingi nchini ni suala la uzazi wa mpango na ukubwa wa familia usioendana na uwezo wa kiuchumi wa wazazi. Hali ambayo husababisha ugumu wa kuwalea watoto katika mazingira bora yatakayowafanya kuwa rasilimali watu yenye ubora, uwezo wa kutimiza ndoto zao na kuchangia maendeleo ya taifa bila kutegemea Serikali kwa kiwango kikubwa.

Kwa sasa, Tanzania ina kiwango cha ongezeko la watu kinachozidi asilimia 3 kwa mwaka, kiwango ambacho ni kikubwa kuliko wastani wa Bara la Afrika wa asilimia 2, pamoja na wastani wa dunia wa asilimia 1.

Takwimu zinaonesha kuwa Tanzania ipo nafasi ya 81 kwa ukubwa wa uchumi duniani na nafasi ya 165 kwa pato la mtu mmoja mmoja kati ya nchi 193 duniani.

Hata hivyo, kwa idadi ya watu, Tanzania ipo nafasi ya 20 duniani, na ikiwa kasi ya ukuaji wa watu itaendelea hivi sasa, mwaka 2050 nchi inaweza kufikia nafasi ya 14 duniani kwa idadi ya watu.

Aidha, makadirio yanaonesha kuwa ifikapo mwaka 2100 Tanzania inaweza kuwa miongoni mwa nchi tisa zenye idadi kubwa zaidi ya watu duniani. Mifano ya mataifa kama China na India inaonesha umuhimu wa kupanga ukuaji wa watu sambamba na maendeleo ya uchumi. China, pamoja na kuwa moja ya nchi zenye uchumi mkubwa duniani, ilifanikiwa kwa kiasi kikubwa kupitia sera ya kudhibiti ongezeko la watu ya “One Child Policy” iliyoanza mwaka 1979/1980. Kwa sasa China ina ukuaji hasi wa watu.

Kwa upande wa India, licha ya kuwa taifa lenye watu wengi zaidi duniani na uchumi wa tano kwa ukubwa, bado pato la mtu mmoja mmoja linaendelea kuwa la chini ukilinganisha na mataifa yaliyoendelea kama Uingereza.

(Feed generated with FetchRSS)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *