
Timu ya Taifa ya Tanzania ya Wanawake chini ya umri wa miaka 20 ‘Tanzanite Queens’ imeangukia katika kundi la ‘vigogo’ katika fainali za Kombe la Dunia kwa Wanawake wa umri huo zitakazofanyika Poland, Septemba Mwaka huu.
Katika droo iliyopangwa leo, Tanzanite Queens imewekwa katika kundi B lenye timu za Brazil, Canada na England.
Ukiondoa Tanzanite Queens, Brazil, Canada na England zote zina historia ya kufanya vizuri katika mashindano hayo hapo nyuma.
Brazil imewahi kumaliza katika nafasi ya tatu mara mbili katika mashindano hayo ambazo ni 2006 na 2022 huku pia ikimaliza katika nafasi ya nne mara mbili.
Canada mafanikio yao makubwa ni kumaliza katika nafasi ya pili katika mashindano hayo yalipofanyika mwaka 2002.
Kwa upande wa England, mafanikio yao makubwa ni kumaliza mara moja katika nafasi ya tatu ya fainali hizo.
Tanzanite Queens itashiriki kwa mara ya kwanza fainali hizo baada ya kufuzu kufuatia kuitupa nje Cameroon katika raundi ya mwisho ya kuwania kufuzu kwa faida ya bao la ugenini.
Timu hizo zilimaliza mechi mbili baina yao kwa sare ya mabao 3-3 ambapo Cameroon ilishinda kwa mabao 3-1 katika mechi ya kwanza na mechi ya marudiano, Tanzanite Queens ikapata ushindi wa mabao 2-0 nyumbani.
Fainali za Kombe la Dunia kwa Wanawake chini ya umri wa miaka 20 mwaka huu zitafanyika Poland kuanzia Septemba 5 hadi 27.