
Dar es Salaam. Chama cha Sekta ya Ulinzi Tanzania (TSIA) kimelaani matumizi ya mabaunsa kwa shughuli za ulinzi, pamoja na kufanya fujo na kusababisha madhara kwa watu na mali zao.
Chama hicho kinaibuka na tamko hilo siku moja tangu Gazeti la Mwananchi lilipochapisha habari kuhusu matumizi ya mabaunsa kama walinzi na athari zinazosababishwa.
Katika habari hiyo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Ayoub Mohamed Mahmoud, aliliambia Mwananchi kuwa hakuna sheria inayowatambua mabaunsa nchini, na kwamba kutumika kama walinzi ni kinyume cha sheria.
Taarifa ya TSIA imetolewa leo Ijumaa, Mei 15, 2026 na Mwenyekiti wake, Felix Kagisa, ikirejea habari iliyochapishwa katika Gazeti la Mwananchi, toleo namba 9405 la Mei 14 mwaka huu.
“Taarifa hii inatolewa na TSIA baada ya taarifa iliyoachapishwa kwenye Gazeti la Mwananchi, toleo namba 9405 la tarehe 14 Mei 2026,” imeeleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, chama hicho kinaungana na Serikali kulaani matumizi ya mabaunsa kwa shughuli za ulinzi, kufanya fujo na kuleta madhara kwa watu na mali zao.
Sambamba na hilo, TSIA kupitia taarifa hiyo imefafanua kuhusu kazi za mabaunsa, kikisema kitaalamu hutumika kwenye milango ya kuingilia matamasha au sherehe maalumu.
“Hawa huwa ni kama maofisa wa usalama wenye jukumu la kudhibiti uingiaji wa wageni au waalikwa kwenye sherehe au matamasha, kuhakikisha usalama na kudumisha utulivu hasa kwa kuangalia vitambulisho,” imeeleza.
Katika milango hiyo, mabaunsa hudhibiti idadi ya watu ukumbini au kwenye eneo la sherehe, kupunguza migogoro na kuwaondoa wasiotii kama ni eneo la kibiashara.
“Wanafanya kama safu ya kwanza ya ulinzi kuwaweka salama wageni wanaoshiriki au waalikwa kwenye tamasha,” imeeleza taarifa hiyo.
Taarifa imesisitiza kuwa mabaunsa hawawezi kutumika kama walinzi wa mali za watu.
Imeeleza kuwa kampuni za ulinzi zilizosajiliwa na kuwa wanachama wa TSIA hutoa mafunzo maalumu kwa walinzi wake na kuhakikisha wanaotumika kwenye ulinzi ni wale waliofuzu mafunzo hayo.
“Tunahakikisha kuwa wanaotumika kwenye ulinzi ni wale waliofuzu mafunzo na wanafanya kazi kwa weledi, uaminifu na kuzingatia sheria za nchi,” imeeleza taarifa hiyo.
Chama hicho kimewasihi Watanzania wote na wale wanaohitaji huduma ya ulinzi wa watu na mali zao kuhakikisha wanatumia walinzi wa kampuni zilizosajiliwa kisheria na wanachama wa TSIA.