
Unguja. Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar (WEMA), kwa mwaka wa fedha 2026/27, inahitaji Sh1.1 trilioni katika kutekeleza mpango wa maendeleo wa sekta ya elimu, huku ikija na vipaumbele sita vya matumizi kwa wizara na taasisi zake.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya wizara hiyo katika mkutano wa Baraza la Wawakilishi, leo Mei 15, 2026, waziri mwenye dhamana, Lela Mohamed Mussa, amesema kati ya fedha hizo, Sh849.179 bilioni zinatokana na mapato ya ndani, na Sh251.446 bilioni ni kutoka kwa wahisani. Katika fedha zinazotokana na mapato ya ndani, Sh466 bilioni ni za miradi ya maendeleo.
Akitaja vipaumbele hivyo, Waziri Lela amesema katika kuimarisha upatikanaji wa elimu bora katika ngazi ya elimu ya lazima, wizara itajenga madarasa 1,600 ya maandalizi, msingi na sekondari.
“Madarasa hayo yanajumuisha shule 20 za kisasa za maandalizi, shule tano za ghorofa za msingi, 10 za ghorofa za sekondari, shule mbili za sekondari za wasichana, shule tano za sekondari za amali, ujenzi wa madarasa mapya pamoja na ukamilishaji wa madarasa yaliyoanzishwa na wananchi,” amesema Waziri Lela.
Vilevile, wizara itafanya ukarabati wa madarasa chakavu, kujenga vyoo 800 na sehemu za kunawia mikono kwa skuli za maandalizi, msingi na sekondari.
Katika kuimarisha ubora wa ufundishaji na ujifunzaji, wizara itasambaza vifaa vya kufundishia na kujifunzia katika shule zote, kutayarisha na kuchapisha vitabu vya mtalaa mpya kwa madarasa ya kidato cha tatu, nne na sita, pamoja na kununua vitabu vya maktaba.
Aidha, walimu 64 watajengewa uwezo juu ya matumizi ya mtaala mpya kwa kidato cha tatu, nne na sita, na vifaa vya utekelezaji wa mtaala rekebifu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu vitaandaliwa.
Vilevile, mfumo wa tathmini ya kitaifa utaanzishwa na tathmini kufanyika katika darasa la pili, tatu na kidato cha pili. Katika kuendeleza ujifunzaji wa kina, huduma za maktaba mtandao na hifadhi ya taifa ya taarifa zitaanzishwa, gari la maktaba-tembezi litanunuliwa, na viwanja vya kisasa vya michezo katika shule zenye michepuo ya michezo vitajengwa Unguja na Pemba, pamoja na kuzipatia shule vifaa vya michezo.
Kipaumbele kingine ni kutanua na kuimarisha elimu ya mafunzo ya amali na ufundi kwa kuzingatia soko la ajira. Wizara itajenga skuli mbili za ufundi, karakana moja kwa kila wilaya kwa ajili ya mafunzo ya amali na ufundi kwa wanafunzi wa sekondari, na kuanza ujenzi wa skuli tano za mafunzo ya amali.
Vilevile, shule za mafunzo ya amali zitapatiwa vifaa ili kuimarisha utoaji wa mafunzo hayo.
“Wizara itajenga jengo la ofisi ya Mamlaka ya Mafunzo ya Amali pamoja na kujenga vyuo viwili vya mafunzo ya amali, Bweleo na Chambani, sambamba na ununuzi wa samani na vifaa vya mafunzo ya amali. Karakana za kufundishia na kujifunzia pia zitaimarishwa kwa kuzipatia vifaa na mashine za kisasa,” amesema Waziri Lela.
Katika uimarishaji wa matumizi ya Tehama na mifumo ya kidijitali, Wizara itasambaza vifaa vya Tehama kwa ajili ya kufundishia na kujifunzia katika shule na kuunganisha shule za msingi na sekondari na mkongo wa taifa.
Kwa mujibu wa wizara, hatua hii inalenga kuongeza matumizi ya teknolojia katika ujifunzaji, ufundishaji na usimamizi wa elimu, sambamba na kuimarisha upatikanaji wa huduma za kidijitali katika sekta hiyo.
Kipaumbele kingine ni kuimarisha upatikanaji wa fursa za elimu ya juu, ambapo Wizara itatanua miundombinu ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (Suza) kwa kuendelea na ujenzi wa mabweni ya wanafunzi wa kike na kiume, ujenzi wa Chuo cha Ubaharia pamoja na miundombinu ya elimu katika Kampasi ya Tunguu, ikiwemo jengo jipya la utawala, jengo la Shule ya Elimu na Lugha, na Kituo cha Huduma kwa wanafunzi.
Pia, wizara itaimarisha Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume (KIST) kwa kujenga hosteli ya wanawake pamoja na tawi la Pemba, na kuendelea na ujenzi wa ukumbi wa taasisi hiyo.
Aidha, Chuo cha Teknolojia cha India (IIT Madras) kitatanuliwa kwa awamu ya pili itakayojumuisha majengo ya utawala, madarasa, maabara, nyumba za walimu na migahawa. Sambamba na hatua hizo, idadi ya wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu itaongezwa.
Akieleza kipaumbele cha kuimarisha usimamizi na uongozi wa sekta ya elimu, Waziri Lela amesema wizara itajenga ofisi mbili za elimu na ukaguzi za mikoa, kuendelea na ujenzi wa jengo la ofisi Unguja, kukamilisha jengo la Wizara Ofisi ya Pemba, na kununua samani za ofisi.
Aidha, ukarabati wa jengo la ofisi Unguja utafanyika, pamoja na ujenzi wa ghala la wizara Unguja.
“Vilevile, nyumba za walimu zitajengwa ili kuboresha mazingira ya kazi na huduma kwa walimu, sambamba na ununuzi wa viti na meza za shule kwa ajili ya kuimarisha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji,” amesema Waziri Lela.
Kwa upande wa maoni ya Kamati ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi kuhusu bajeti hiyo, imeipongeza wizara kwa kufanikisha uandikishaji wa wanafunzi wa maandalizi kwa asilimia 94.7 ya shabaha ya utekelezaji na asilimia 106.1 kwa wanafunzi wa msingi.
Akisoma hotuba ya kamati, mjumbe wa kamati hiyo, Issa Ussi Haji (Gavu), amesema kamati inaishauri wizara kutoa taaluma sahihi kwa wanafunzi hao huku wakizingatia mtaala na mitasari ya masomo husika ili kuwajengea msingi mzuri wa kujifunza stadi zote za kusoma, kuandika na kuhesabu.