Viwango vipya vya kimataifa vyatakiwa ili plastiki zilizorejelezwa ziwe salama kwa matumiziViwango vipya vya kimataifa vyatakiwa ili plastiki zilizorejelezwa ziwe salama kwa matumizi

Unaweza kujiuliza kurejeleza au recycling kwa lugha ya kiingereza ni nini? Tunanukuu kamusi ya kiingereza ya Oxford inayoeleza kuwa ni mchakato wa kuwezesha bidhaa au kitu kilichokwishatumika, kiweze kutumika tena.

Ni katika muktadha huo wataalamu wa usalama wa chakula wanataka hatua zichukuliwe ili plastiki zinazorejelezwa na kutumika kama vifungashio vya chakula hazina madhara kwa afya ya binadamu, huku dunia ikiendelea kutafuta suluhisho la kudumu la kupunguza taka za plastiki.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO, Katika uchambuzi mpya wake mpya limeonya kuwa ingawa plastiki zilizorejelezwa pamoja na vifaa mbadala vya kufungashia chakula vinaweza kusaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira, lakini vinaweza pia kuongeza hatari ya kemikali hatari kuingia kwenye chakula iwapo mifumo ya urejelezaji haitabuniwa kwa umakini.

© Unsplash/Calvin Sihongo Plastiki hukusanywa kwa ajili ya kurejelewa katika jiji la Johannesburg, Afrika Kusini.

Kivipi kemikali kwenye chakula?

Vittorio Fattori, Afisa wa Usalama na Ubora wa Chakula wa FAO, amesema, “Taka za plastiki zimekuwa changamoto kubwa duniani na kwamba urejelezaji bora ni sehemu muhimu ya suluhisho.”

Hata hivyo, ameonya kuwa juhudi za kupunguza uchafuzi wa plastiki hazipaswi kusababisha matatizo mapya ya usalama wa chakula.

Kwa mujibu wa uchambuzi huo, vifungashio vya chakula vina mchango mkubwa katika mifumo ya kisasa ya chakula kwa kusaidia kuhifadhi ubora wa chakula, kuongeza muda wa matumizi na kupunguza upotevu wa chakula. Soko la vifungashio duniani linatarajiwa kuongezeka kutoka dola bilioni 505 mwaka 2024 hadi zaidi ya dola bilioni 815 ifikapo mwaka 2030.

Kemikali kwenye plastiki zilizorejelewa

FAO imeeleza kuwa tofauti na bidhaa nyingine zinazorejelewa, vifungashio vya chakula vinahitaji kufikia viwango vya juu zaidi vya usalama wa kemikali.

Plastiki zinazotumika kufungashia chakula huwa na maelfu ya kemikali zinazotumika wakati wa uzalishaji, mathalani:

  • Rangi, mipako, viimarishaji na vilainishi vya plastiki.
  • Wakati wa urejelezaji, uchafu mwingine unaweza kuingia kutokana na upangaji usio sahihi wa taka, mazingira au matumizi ya awali ya watumiaji.
  • Viwango vya juu vya metali nzito, kemikali za kuzuia moto na kemikali nyingine sugu kuliko plastiki mpya.

Hata hivyo, wataalamu wameeleza kuwa plastiki zilizorejelewa na kuidhinishwa kwa matumizi ya chakula zinaweza kuwa salama sawa na plastiki mpya iwapo zitafanyiwa usafishaji wa kina, kuondolewa uchafu na ukaguzi mkali wa kisheria.

Kwa mfano, katika Muungano wa Ulaya, (EU), plastiki zilizorejelewa zinazotumika moja kwa moja na  chakula zinatakiwa kukidhi viwango sawa vya usalama kama plastiki mpya.

Vifungashio mbadala navyo vyachunguzwa

Ripoti hiyo pia imeangazia vifaa mbadala vya kufungashia chakula kama bioplastiki, nyuzi za mimea na vifaa vinavyotokana na protini, ambavyo vinatajwa kama suluhisho rafiki kwa mazingira.

Hata hivyo, FAO imeonya kuwa kuwa na asili ya kibaolojia hakumaanishi moja kwa moja kuwa vifaa hivyo vinaweza kuoza kwa urahisi au kuwa salama kabisa.

© Unsplash/Arshad Pooloo Bidhaa nyingi za plastiki, kama vile chupa za vinywaji, zimetengenezwa kwa matumizi mara moja tu.

Mathalani zitengenwazo na miwa au mahindi

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, baadhi ya vifaa vinavyotokana na mahindi au miwa vina muundo wa kemikali unaofanana na plastiki zinazotokana na mafuta ya kisukuku. Aidha, vifungashio vya mimea vinaweza kuingiza mabaki ya viuatilifu, sumu za asili, fangasi sumu na metali nzito kwenye chakula.

Vifaa vinavyotokana na protini vinaweza pia kuongeza hatari ya vihatarishi vya mzio kama gluten kuingia kwenye chakula.

Wasiwasi kuhusu chembechembe ndogo za plastiki waongezeka

Uchambuzi huo umeeleza pia wasiwasi unaoongezeka kuhusu chembe ndogo za plastiki zinazojulikana kama chembechembe ndogo za plastiki au microplastics kwa lugha ya kiingereza, na chembechembe ndogo zaidi za  plastiki au nanoplastics kwa lugha ya kiingereza, katika chakula na vinywaji.

“Wanasayansi wamegundua chembe hizo katika damu ya binadamu, mapafu, maziwa ya mama na hata kondo la uzazi, hali inayodhihirisha kuwa watu wengi tayari wameathiriwa nazo.”

Hata hivyo, ripoti imebainisha kuwa bado hakuna mbinu zinazofanana kimataifa za kugundua na kupima chembe hizo kwa usahihi, jambo linalofanya iwe vigumu kubaini madhara yake halisi kwa afya ya binadamu.

Aidha, baadhi ya mitambo ya urejelezaji imetajwa kuwa inaweza kuchangia kuenea kwa microplastics wakati wa kuvunja plastiki katika vipande vidogo.

Wito wa viwango vya kimataifa

Matokeo ya uchambuzi huo yanatarajiwa kusaidia majadiliano ndani ya Kamisheni ya CAC (the Codex Alimentarius Commission), chombo cha kimataifa cha viwango vya chakula kilichoanzishwa na FAO pamoja na WHO.

FAO imeeleza kuwa tofauti za sheria kati ya nchi kuhusu plastiki zilizorejelewa na vifaa vinavyogusa chakula zinaweza kuleta changamoto katika biashara na ulinzi wa walaji.

Kwa mujibu wa shirika hilo, kuwepo kwa viwango vya kimataifa vinavyofanana kutasaidia kufanya tathmini bora za kisayansi kuhusu hatari za kiafya na kusaidia mataifa kupunguza taka za plastiki kwa njia salama zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *