
Dar es Salaam. Katika jitihada za kuongeza tija ya kilimo nchini Tanzania, watafiti wameendelea kubuni teknolojia mpya zinazolenga kupunguza hasara inayotokana na magonjwa na wadudu wanaoshambulia mazao.
Miongoni mwa ubunifu huo ni matumizi ya akili bandia (AI) kupitia programu ya simu ya mkononi inayojulikana Nuru, inayowasaidia wakulima kutambua magonjwa ya mazao moja kwa moja wakiwa shambani na kupata suluhisho.
Mtafiti kutoka Taasisi ya Kimataifa ya kilimo cha Kitropiki (IITA), Neema Mbilinyi anayefanya kazi katika kitengo cha udhibiti wa magonjwa na wadudu wanaoshambulia mazao, anasema teknolojia hiyo imeandaliwa kupitia ushirikiano kati ya IITA na Penn State University na shirika la Chakula na kilimo duniani (FAO).
Katika mahojiano yake na Mwananchi amesema lengo la kuanzishwa kwa programu hiyo ni kuwasaidia wakulima kupata suluhisho la haraka na la uhakika dhidi ya changamoto zinazopunguza mavuno.
Anasema wakulima wengi nchini hukumbwa na tatizo la kutotambua mapema dalili za magonjwa, jambo linalosababisha kuendelea kutumia mbegu zilizoathirika au kusambaza magonjwa kutoka shamba moja hadi jingine.
Hali hiyo imechangia kupunguza uzalishaji na mapato ya mkulima kushuka.
“Vipimo vya maabara vinaweza kutoa majibu sahihi zaidi lakini mara nyingi ni ghali, vinachukua muda mrefu na si rahisi kufikika kwa mkulima wa kawaida. Ndiyo maana tulihitaji suluhisho ambalo mkulima anaweza kuwa nalo mkononi muda wote,” anasema Neema.
Kupitia programu ya Plant Village Nuru, mkulima hupiga picha ya jani la mmea kwa kutumia simu yake ya mkononi (Android), kisha mfumo wa akili bandia huchambua picha hiyo na kubaini kama mmea una ugonjwa au una afya njema.
Mpaka sasa, programu hiyo imefundishwa kutambua magonjwa ya mhogo kama michirizi ya kahawia na batobato, ugonjwa wa migomba unaojulikana kama banana bunchy top virus pamoja na madhara ya viwavi jeshi vamizi kwenye mahindi.
“Faida kubwa ya teknolojia hiyo ni kwamba inafanya kazi hata bila mtandao wa intaneti, hivyo mkulima wa kijijini anaweza kuitumia akiwa shambani bila changamoto ya mawasiliano,” anasema.
Ili kuhakikisha teknolojia hiyo inaweza kutumiwa na watu wote, imewekwa katika lugha mbalimbali ikiwemo Kiswahili ili iwe rahisi kwa wakulima wengi zaidi kuitumia.
“Mbali na kutambua ugonjwa, programu hiyo pia humpa mkulima ushauri wa hatua za kuchukua. Kwa magonjwa mengi ya virusi ambayo hayana tiba, wakulima wanashauriwa kutumia mbegu bora, safi na zilizothibitishwa na TOSCI (Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania) ili kuzuia maambukizi mapya na kuongeza uzalishaji,” anasema.
Neema anasema tangu mradi huo uanze kutengenezwa mwaka 2017 na kuanza kutumika rasmi mwaka 2022, zaidi ya wakulima na wadau wa mbegu 3,000 wamepatiwa mafunzo ya matumizi yake.
“Hii ni hatua muhimu katika kuimarisha kilimo cha kisasa kinachotegemea maarifa na teknolojia,” anasema.
Kwa Tanzania ambayo uchumi wake unategemea kwa kiasi kikubwa sekta ya kilimo, matumizi ya ubunifu kama huu yanaweza kuwa mkombozi mkubwa kwani kupunguza magonjwa ya mazao kunamaanisha kuongeza mavuno, kuinua kipato cha mkulima, kuboresha usalama wa chakula na kukuza uchumi wa Taifa.
“Kadri teknolojia inavyoendelea kusambaa vijijini, matumaini ni kwamba wakulima wengi zaidi wataweza kulinda mashamba yao mapema, kufanya maamuzi sahihi na kuendesha kilimo chenye tija, ushindani na manufaa makubwa zaidi,” anasema.
Anasema programu hiyo ni bure kwa wakulima wote wanaotaka kuitumia baada ya kuipakua isipokuwa baadhi ya vitu au ushauri zaidi ndiyo unaweza kuwataka kuwa na huduma ya intaneti ili waweze kupata usaidizi mzuri.
Ili kubaini ugonjwa wa zao husika, mkulima hutakiwa kuchagua jani ambalo anaona halina afya, kisha anachukua simu yake na kuelekeza kamera juu ya jani ili iweze kuona jani lote kwenye kioo cha simu.
“Atakuwa anasogeza simu taratibu kuhakikisha jani linaonekana vizuri katika simu yake na hapo inakuwa inafanya uchunguzi, baada ya utambuzi programu ya Nuru itamuelekeza njia za kudhibiti ugonjwa huo,” anasema.
Licha ya faida yake na uwezo wa kusaidia wakulima, baadhi ya watembeleaji wa maonyesho hayo walisema bado haijafahamika vizuri na wakulima.
“Watu 3,000 bado ni wachache sana ukilingananisha na idadi ya wakulima waliopo Tanzania, jitangazeni zaidi ili kuhakikisha wengi wanasaidika kwa njia rahisi ukizingatia wakulima wengine wapo mbali na maabara au hawawezi kufikiwa kirahisi na wataalamu wa kilimo,” amesema Victor Tesha.
