DC Mtatiro: Kuandika wosia sio kujitabiria kifoDC Mtatiro: Kuandika wosia sio kujitabiria kifo

Shinyanga. Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro amewataka wananchi kuandika wosia mapema kwani unasaidia kupunguza migogoro ya mirathi ambayo mara nyingi husababisha ndugu kufarakana.

Mtatiro ameeleza hayo leo Mei 17, 2026 katika kituo cha Nguzonane mjini Shinyanga wakati wa ziara yake ya kutembelea utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria kwa wananchi wa Manispaa ya Shinyanga ulioanza Mei 6 na unatarajiwa kuhitimishwa Mei 20, 2026.

Amesema migogoro hiyo inaendelea kwa sababu wananchi bado wana uhitaji mkubwa wa elimu katika kuipunguza, pia, amewasihi wazazi kuandika wosia mapema.

“Kuandika wosia sio kujitabiria kifo, bali ni maandalizi mazuri kwa ajili ya kuweka familia katika amani hata kipindi ambacho unakuwa haupo. Pia, wale wanaosubiri siku za mwisho, wajitokeze kupata huduma ya kisheria kwani siku zimeisha, zimebaki siku tatu tu,” amesema Mtatiro.

Kwa upande wake, mratibu wa kampeni ya msaada wa kisheria, Laurent Bulilo amesema huduma hiyo imetolewa katika halmashauri zote sita, ambapo awamu ya pili ilianza    Mei 6, 2026, na huduma hiyo inatolewa bure, ikiwalenga wasiokuwa na uwezo wa kuwalipa mawakili.

“Toka tumeanza huduma hii katika Mkoa wa Shinyanga kesi za migogoro ya ardhi zimeongoza ambapo tumepokea kesi 2,370 na kutatua migogoro 331,” amesema Bulilo.

Kwa upande wao, watoa huduma ya msaada wa kisheria kutoka vitengo mbalimbali, wameeleza kesi walizopokea pamoja na utatuzi unaotolewa sambamba na utoaji elimu kwa wananchi na upatikanaji wa huduma hapo hapo hususani katika masuala ya kupata vyeti vya kuzaliwa.

Wakili wa Serikali kutoka Wakala wa Vizazi na Vifo (Rita), Nyanda Masunga amesema: “Katika kipindi hiki tumetoa vyeti 1,648, pia, tumekuwa tukishauri watu kuandika wosia kwa kuzingatia uhiari wake na muhimu ni kuwa na cheti cha kuzaliwa kwa sababu kwa sasa hata mtoto kuanza darasa la kwanza lazima uwe na cheti cha kuzaliwa,” amesema Nyanda.

Ofisa Usajili wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) Mkoa wa Shinyanga, Devotha Nchia ameeleza kuwa: “Hadi kufikia Mei 17 tumetoa vitambulisho 516 na tumepokea malalamiko 65, wananchi wakidai kuwa wanakaa mbali na ofisi, wakihitaji mwafaka wa kupata vitambulisho pindi huduma hii itakapokwisha. Kwa hili niwahakikishie kwamba baada ya vitambulisho kutoka, wataletewa katika kata zao,” amesema Devotha.

Kwa upande wake, Ofisa Ardhi mteule kutoka Ofisi ya Kamishna wa Ardhi, Halima Ramadhan amesema: “Tumefanikiwa kutoa hati 92 ndani ya muda mfupi tangu kuanza kwa huduma hii, pamoja na migogoro 16 ambayo tumeipokea na kuwaelekeza kwenda idara husika kwa sababu hapa kuna mawakili ambapo pia wanasaidia na kuwaelekeza cha kufanya ili kupata utatuzi,” amesema Halima.

Mkazi wa kata ya Ngokolo, Manispaa ya Shinyanga, Mshandete Charles ameeleza kufurahishwa na huduma zinazotolewa na timu ya huduma ya msaada wa kisheria, bila kuwa na changamoto yeyote, ambapo amefanikiwa kupata cheti cha kuzaliwa cha mtoto ndani ya muda mfupi.

“Nimefurahishwa na namna wanahudumia watu hapa, nilikuwa nafuatilia vyeti vya watoto wangu sita na leo nimepata cheti cha mwisho ndani ya muda mfupi, ukija leo kesho unapata cheti chako kwa wakati,” amesema Charles.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *