Tulee hivi watoto kukabiliana na changamotoTulee hivi watoto kukabiliana na changamoto

Dodoma. Fikiria baba na mwanawe wa miaka mitano wako kwenye bustani jioni. Ghafla suruali ya mtoto inanasa kwenye miiba.

Mtoto akiwa kakaa chini analia, “Baba, nisaidie! Baba!” Baba akiwa mbali anampa mwanawe pole na kumwambia, “Hebu itoe hiyo miiba polepole. Usiogope unaweza.” Mama anawaona kwa mbali. Haelewi kwa nini baba hamsaidii mtoto kuchambua miiba kwenye suruali.

“Baba Junia kweli? Mtoto analia na wewe unamwangalia tu?” Mama anatimua mbio kwenda kuokoa jahazi. “Usimtese mtoto bwana.” Mama analalamika lakini anafika tayari mtoto ameshachambua miiba yote.

Je, nani yuko sahihi kati ya baba na mama? Kumsaidia mtoto mapema kama anavyofanya mama hapa ni sawa au kumwacha apambane na tatizo?

Malezi, kwa hakika, yana nafasi kubwa kumsaidia mtoto kutatua matatizo, kwa maana ya uwezo wa kulibaini tatizo na kulikabili kwa kufikiria namna bora ya kuliondosha.

Utatizo wa matatizo ni stadi muhimu inayowawezesha watoto kukabiliana na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo kila siku kuanzia kwenye masuala madogo kama nini cha kufanya wenzake wanapokataa kucheza naye hadi kufanya maamuzi makubwa yanayoamua mustakabali wa maisha yake ya baadaye.

Malezi yanayokuza uwezo wa kukabiliana na changamoto humwekea mtoto mazingira salama ya kujaribu, kukosea na kujifunza kutokana na makosa. Kinyume chake ni kumuandaa kuwa tegemezi wa watu wengine, kulalamikia wengine kwa matatizo yake na hata kubaki akijihurumia katikati ya tatizo alilojisababishia mwenyewe badala ya kulitafutia ufumbuzi.

Mtoto mwenye uwezo wa kufumbua changamoto kwanza hujiamini, hana ule uoga wa kukabiliana na maumivu ya awali anapoanza kulibaini na kulikabili tatizo.

Mtoto muoga hughairi mapema hasa anapohisi kuna maumivu anapoanza kuchukua hatua za kulitafutia ufumbuzi tatizo. Pili, mtoto mfumbuzi huwa na mtazamo chanya unaomfanya awe tayari kujitegemea badala ya kulia lia akiomba msaada wakati mwingine kabla hata hajajaribu mwenyewe. Lakini pia, mtoto huyu huwa na ustahimilivu unaomfanya aendelee kujaribu hata pale matokeo yanapoonesha kuwa hajapata matokeo aliyoyatarajia.

Jaribio la kwanza linapokwama, mathalani, mtoto mfumbuzi hufikiri namna nyingine bora zaidi hata ikibidi kwa kushirikiana na wengine.

Malezi ya asili
Ufumbuzi wa matatizo umekuwa sehemu ya malezi yetu ya asili. Mazingira ya kimakuzi yaliwalazimisha watoto kuwa wanyumbulifu katika kutatua matatizo tangu wakiwa wadogo.

Kushiriki majukumu ya nyumbani, kwa mfano, ilikuwa ni jambo lisilo na mjadala. Ukosefu wa raslimali muhimu za kusafisha kinywa, ziliwachochea watoto kugeuza miti kuwa miswaki na mkaa kuwa dawa ya kung’arishia meno.

Kadhalika, katika mazingira ambayo shule zilikuwa mbali, watoto walilazimika kutembea umbali mrefu bila kushurutishwa na wazazi.

Hadithi za jioni pia zilifundisha kutatua matatizo kupitia mifano ya maadili, ambapo wahusika walikabiliwa na matokeo ya uamuzi wao na kujifunza kuchukua hatua mapema. Malezi haya yaliwafanya watoto wa Kiafrika wawe na mtazamo madhubuti wa  kutatua matatizo pengine kuliko ilivyo hivi sasa.

Malezi ya kizazi kipya
Kimeibuka kizazi kipya hapa katikati kinachoamini kumwacha mtoto kukabiliana na changamoto ni uonevu. Tabia yetu ya kutafsiri maendeleo kwa papara inawafanya wazazi waliofanikiwa kuzitazama shida kamma kiashiria cha umasikini.

Leo hii mzazi anapokuwa na maisha bora anaanza kuwaza zaidi namna ya kuwaepusha watoto wake na changamoto zozote ambazo kimsingi wanazihitaji ili kukuza unyumbulifu wao katika kutatua matatizo.

Wazazi wangapi leo wanawazuia watoto kucheza? Sikiliza namna tunavyozungumzia michezo kama upotevu wa muda. Tunasahau kuwa michezo ni fursa kwa mtoto kujifunza maisha katika uhalisia wake ikiwa ni pamoja na kutatua matatizo.

Ingawa hatuwezi tena kurudi moja kwa moja kwenye shida zilezile tulizokutana nazo tulipokulia kwenye umasikini, lakini bado tunaweza kuwatengenezea watoto mazingira ya kuona kumbe si kila wanachokihitaji kinapatikana kirahisi. Tunaweza kuwalea watoto kwenye mazingira yanayowafanya waone haja ya kufikiri, kujiongeza na kuyatazama maisha kama safari inayohitaji uwezo wa mtu kujifunza, kukosea, kujirekebisha na kujipa nafasi ya kurudia tena na tena na tena.  

Ushauri
Hata katika mazingira ambayo una rasilimali za kutosha na mtoto anaweza kupata kila anachokihitaji, bado unaweza kubana kidogo na hata kuchelewesha upatikanaji wake ili mtoto aone haja ya kujiongeza.

Kuna wakati mazungumzo ya moja kwa moja pia yanasaidia. Mshirikishe kwenye mazungumzo ya wazi kuhusu tatizo lililopo na kwa pamoja msaidiane kutafuta ufumbuzi kulingana na umri wake. Tengeneza mazingira rafiki yanayomruhusu mtoto kukabiliana na matatizo madogo peke yake chini ya mwongozo wako, ili ufumbuzi wa matatizo uwe sehemu ya maisha ya kawaida.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *