WHO: Mlipuko mpya wa Ebola DRC na Uganda sasa ni dharura ya kimataifa ya afya ya ummaWHO: Mlipuko mpya wa Ebola DRC na Uganda sasa ni dharura ya kimataifa ya afya ya umma

WHO imesema uamuzi huo umefanywa chini ya Kanuni za Afya za Kimataifa baada ya mashauriano na nchi hizo mbili pamoja na tathmini ya hatari ya kusambaa kwa ugonjwa huo kimataifa, ongezeko la maambukizi na hali tete ya kibinadamu katika maeneo yaliyoathirika.

Kuongezeka kwa wagonjwa na vifo kwazua hofu

Hadi jana Mei 16, mamlaka za afya zilikuwa zimeripoti wagonjwa wanane  waliothibitishwa maabara ya Ebola, wagonjwa wengine 246 vinaoshukiwa na vifo 80 vinavyoshukiwa katika jimbo la Ituri mashariki mwa DRC katika maeneo ya afya ya Bunia, Rwampara na Mongbwalu.

WHO pia imethibitisha wagonjwa wawili wa Ebola mjini Kampala nchini Uganda, na kifo kimoja kinachoshukiwa kuwa Ebola, kwa wasafiri waliowasili kutoka DRC ndani ya kipindi cha saa 24.

WHO imeonya kuwa mlipuko huo unaweza kuwa mkubwa zaidi kuliko unavyogunduliwa kwa sasa. “Kiwango kikubwa cha sampuli zilizopatikana kuwa na maambukizi, kuthibitishwa kwa wagonjwa mjini Kampala na Kinshasa, pamoja na ongezeko la makundi ya vifo, vinaashiria uwezekano wa mlipuko mkubwa zaidi kuliko unaoripotiwa sasa,” shirika hilo limesema.

Shirika hilo limeongeza kuwa ukosefu wa usalama, uhamaji mkubwa wa watu na udhaifu wa hatua za kudhibiti maambukizi vinaongeza hatari ya kusambaa zaidi kwa ugonjwa huo.

Wahudumu wa afya miongoni mwa waliopoteza maisha

Wasiwasi mkubwa pia umeibuka kuhusu maambukizi kwa wahudumu wa afya, huku angalau vifo vinne vya wahudumu hao vikihusishwa na mazingira yanayofanana na homa kali ya kuvuja damu inayosababishwa na virusi vya Ebola. WHO imesema hali hiyo inaibua hofu ya maambukizi ndani ya vituo vya afya pamoja na mapungufu katika mifumo ya kuzuia na kudhibiti maambukizi.

“Tukio hili ni la kipekee,” WHO imesema katika tamko lake, ikibainisha kuwa tofauti na milipuko ya awali ya Ebola iliyosababishwa na aina ya Zaire, kwa sasa hakuna chanjo wala tiba maalum zilizoidhinishwa kwa virusi vya Bundibugyo. Shirika hilo limesisitiza kuwa uelewa mdogo kuhusu uhusiano wa wagonjwa waliothibitishwa na wanaoshukiwa unatatiza juhudi za kufuatilia na kudhibiti mlipuko huo.

© WHO Mlipuko mpya wa Ebola wazuka Uganda

Kusambaa kikanda kwaibua wasiwasi wa kimataifa

WHO imesema kuthibitishwa kwa visa vya Ebola nchini Uganda kunaonesha kuwa ugonjwa huo tayari umeanza kusambaa kimataifa. Nchi jirani zinazopakana na DRC zinatajwa kuwa katika hatari kubwa kutokana na harakati kubwa za watu kuvuka mipaka, biashara na safari za mara kwa mara.

Shirika hilo limezipongeza serikali za DRC na Uganda kwa uwazi wao na hatua za haraka walizochukua. Mkurugenzi Mkuu wa WHO amezisifu nchi hizo “kwa kujitolea kuchukua hatua muhimu na madhubuti kudhibiti tukio hili,” akiongeza kuwa uwazi wao umewezesha jumuiya ya kimataifa kuanza maandalizi na hatua za kukabiliana na mlipuko huo kwa haraka.

WHO WHO yaongeza juhudi za kukabiliana na mlipuko moya wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (Maktaba)

Ushirikiano wa kimataifa wahitajika haraka

WHO imetangaza kuwa Kamati ya Dharura chini ya Kanuni za Afya za Kimataifa itaitishwa haraka iwezekanavyo kutoa ushauri kuhusu mapendekezo ya muda kwa nchi zinazokabiliana na mlipuko huo. Shirika hilo limesisitiza kuwa ushirikiano madhubuti wa kimataifa utahitajika ili kuimarisha ufuatiliaji, kinga, matibabu ya wagonjwa na operesheni za dharura.

WHO imeonya kuwa mchanganyiko wa migogoro ya usalama, majanga ya kibinadamu, hatari ya maambukizi mijini na mtandao mkubwa wa vituo vya afya visivyo rasmi unaweza kuongeza kasi ya kusambaa kwa ugonjwa huo iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.

“Tukio hili linahitaji uratibu na ushirikiano wa kimataifa,” WHO ilisema, ikitoa wito wa kuongeza juhudi za kuelewa ukubwa kamili wa mlipuko huo na kuzuia maambukizi zaidi kikanda na kimataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *