Israel ilianzisha vipi vituo vya kijeshi nchini Iraq na madhara yake ni yapi?Israel ilianzisha vipi vituo vya kijeshi nchini Iraq na madhara yake ni yapi?

Gazeti la Marekani la New York Times limeandika katika ripoti yake kwamba, Israel imeanzisha vituo viwili vya kijeshi vya siri ndani ya ardhi ya Iraq kwa ajili ya kusaidia operesheni zake dhidi ya Iran.

Swali ni kwamba, utawala wa Kizayuni wa Israel umewezaje kuanzisha kituo cha kijeshi ndani ya nchi ambayo hata haina uhusiano wa siri na Tel Aviv? Madhara ya kitendo kama hiki ni yapi?

Hatua ya Israel ya kuanzisha vituo vya kijeshi nchini Iraq ilifanywa kwa msaada na uratibu wa Marekani. Ushawishi na uwepo wa kiusalama wa Marekani nchini Iraq — ambao mara nyingi umekabiliwa na maandamano na upinzani wa wananchi — uligeuka kuwa nyenzo mikononi mwa Washington, na Israel ikaweza kuanzisha kituo cha siri ndani ya ardhi ya Iraq. Gazeti la New York Times liliripoti kwamba, Marekani ilikuwa na taarifa kuhusu uwepo wa kituo hiki cha Israel. Inaonekana Washington ilificha ukweli huu kwa Iraq, kwamba vikosi vya adui vilikuwa vipo ndani ya ardhi ya nchi hiyo.

Ili jeshi, vikosi vya usalama na makundi ya muqawama nchini Iraq yasigundue kuanzishwa kituo cha kijeshi, kituo hicho kilijengwa katika eneo la jangwani lenye upana mkubwa.

Gazeti la Marekani la Wall Street Journal pia liliandika kwamba, kituo hiki cha siri kilikuwa katika jangwa la magharibi mwa Iraq, ndani ya eneo la Sahara ya Najaf, na vikosi maalum vya Israel vilikuwa vimepangwa humo; eneo kubwa na lenye watu wachache ambalo, kwa mujibu wa wachambuzi, linachukuliwa kama mazingira mazuri kwa shughuli za siri. Utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kutumia vibaya upana na ugumu wa kupitika kwa maeneo ya jangwani ya Iraq, ulijaribu kuanzisha kituo cha kisasa kati ya mikoa ya Karbala, Anbar na Najaf kwa ajili ya msaada wa vifaa na operesheni za ndege za kijeshi.

Jambo jingine ni kwamba vituo hivi vilianzishwa kwa vipindi viwili tofauti: kabla ya vita vya siku 12 na kabla ya vita vya siku 40 dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kituo kimoja kilijengwa mwishoni mwa mwaka 2024 magharibi mwa Iraq, na kituo kingine pia kilianzishwa mwaka huu. Kwa maneno mengine ni kuwa, Marekani kwa zaidi ya mwaka mmoja imeficha uwepo wa vituo hivi kwa viongozi wa Iraq, na hadi sasa haijaonyesha radiamali na mjibizo wowote kuhusu suala hili.

Maudhui nyingine pia inahusu lengo na jukumu la vituo hivi. Vyanzo vya Marekani vilitangaza kwamba, jukumu kuu la kituo hiki ni kusaidia mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya malengo yanayohusiana na Iran; ikiwemo kutoa njia za dharura kwa ajili ya kutua au kuokoa marubani iwapo ndege zao za kivita zingetunguliwa. Baadhi ya vyanzo pia vilisema kwamba, lengo la kuanzishwa vituo hivi ni kupunguza muda wa safari za ndege kwa mashambulizi dhidi ya Iran, kutoa msaada wa vifaa, kuweka vikosi maalum na kuandaa operesheni za uokoaji iwapo ndege za kivita za Israeli zingeangushwa.

Hatua ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuanzisha vituo hivi ina madhara makubwa. Hii ni mara ya kwanza ambapo Israel imeanzisha miundombinu ya operesheni amilifu ndani ya ardhi ya Iraq. Hatua kama hii, kwa kuzingatia ushawishi na uwepo wa kijeshi wa Marekani nchini Iraq, inaweza kukaririwa tena.

Aidha, kitendo hiki, mbali na kuthibitisha kushindwa serikali ya Iraq katika kulinda mamlaka ya nchi, pia kinaonyesha kwamba, utawala wa kimabavu wa Marekani unatumia vibaya jiografia ya Iraq na kukiuka makubaliano ya kiusalama na nchi hiyo. Kutumia vibaya Marekani na Israel udhaifu wa serikali ya Iraq katika kulinda mamlaka yake ya kujitawala, kunaipa haki Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kulenga vituo vya kijeshi vya utawala ghasibu Israel vilivyoko Iraq kwa minajili ya kujihami na kudhamini usalama wake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *