Jeshi la Magereza Mkoa wa Morogoro limeendelea kuhamasishwa matumizi ya nishati safi ya kupikia ikiwa ni sehemu ya Mkakati wa Serikali kuhakikisha Asilimia 80 ya wanatumia wahamie kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua miradi ya nishati safi ya kupikia kwa Jeshi la Magereza mkoani Morogoro, Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali (Mstaafu), Jacob Kingu amesema kuwa lengo la taifa la kufikia matumizi makubwa ya nishati safi ya kupikia linawezekana kutokana na uwepo wa vyanzo mbalimbali vya nishati hiyo.
Amesema wananchi wana nafasi ya kuchagua aina ya nishati safi kulingana na mazingira wanayoishi, ikiwemo gesi, mkaa mbadala pamoja na matumizi ya umeme kwa ajili ya kupikia.
“Inawezekana ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya watanzania wanatumia nishati safi za kupikia maana zipo nyingi” amesema Mwenyekiti Kingu.
Aidha, ameeleza kuwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unaendelea kupeleka huduma ya umeme katika Vijiji na Vitongoji jambo litakalowezesha wananchi wengi zaidi kutumia umeme kama chanzo cha nishati safi ya kupikia.
Kwa upande wake, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza (SACP), Peter Anatory amesema mradi wa majiko ya nishati safi ya kupikia unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umewezesha magereza 12 ya Mkoa wa Morogoro kunufaika na huduma hiyo.
Amesema kupitia mradi huo, magereza hayo yamepata majiko 15 yanayotumia mkaa rafiki kwa mazingira pamoja na tani 236 za mkaa huo, hali iliyosaidia kuongeza matumizi ya nishati safi katika taasisi za magereza.
“Mradi huu umekuwa kichocheo kikubwa kwa magereza katika kuhakikisha tunatumia nishati safi ya kupikia,” amesema Anatory.
Naye Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Samuel Aron Mwakatika amesema matumizi ya nishati safi yana mchango mkubwa katika kuboresha maisha ya wananchi, kulinda mazingira pamoja na kukuza uchumi wa taifa.
(Feed generated with FetchRSS)
