Katika adhuhuri moja yenye joto la wastani jijini Tanga, Eliza (si jina lake halisi) anaonekana akifungua kurasa moja baada ya nyingine ya kijitabu kidogo kilichopambwa kwa mwandiko wenye kuvutia akiwa ameketi kwenye meza ya mbao.
Akiwa ndani ya nyumba iliyokuwa haina pilika pilika za hapa na pale lakini iliyojaa uchangamfu, anaonekana mwenye amani akiingia ndani ya chumba kimoja baada ya kingine, akisaidia kazi za ndani, akisalimia watu waliomo ndani na kisha kupata muda kufurahi na watoto.
“Sijisikii mnyonge hata kidogo kama ilivyokuwa hapo awali,” anajisemea chinichini. “Namchukulia mama huyu kama mzazi wangu na tunaishi naye kwa maelewano makubwa.”
Kauli hii ni kielelezo cha mabadiliko makubwa ya kisaikolojia kwa binti huyu. Hapo awali, Eliza hakuwa mtu wa kutabasamu au kuzungumza na watu hata kidogo, lakini leo hii amevaa vazi la ujasiri kuzungumzia kesho yake.
“Ndoto yangu ni kuwa mpishi mkubwa na kumiliki hoteli kubwa,” anasema Eliza kwa msisitizo.
Mwanzo wa safari ya matumaini ya Eliza ulionekana kupitia mradi wa Pamoja Tuwalinde, ambao ni sehemu ya programu ya TangaYetu unaotekelezwa na Shirika la TAYOTA.
Programu hii inalenga kuimarisha mifumo ya ulinzi na kukabiliana na ukatili dhdi ya watoto na vijana kupitia tafiti, ujengaji uwezo na ushirikishwaji wa jamii.
Kutokana na vitendo vya unyanyasaji alivyokuwa anapitia, Eliza alipendelea zaidi kukaa peke yake muda mwingi.
Mapito ya Eliza
Licha ya Eliza kupenda shule, hususani somo la Kiswahili, lakini majukumu ya nyumbani yalikuwa mwiba mchungu kwenye masomo yake kwa ujumla.
Baada ya shule, alilazimika kuosha vyombo, kupika na kulea watoto akimsaidia mama yake aliyekuwa akiuza samaki, hali iliyomnyima fursa ya kujisomea.
Hali ilizidi kuwa mbaya alipofika darasa la tano, ambapo alianza kufanyiwa ukatili na mwanaume aliyekuwa akimlea tangu utoto, ingawa hakuwa baba yake mzazi.
Licha ya Eliza kutoa taarifa mara kadhaa, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa, jambo lililomfanya aanze kujitenga na hata kutoroka nyumbani kutafuta ulinzi.
Baada ya kutoroka, Eliza alipata msaada kutoka kwa mwenyekiti wa mtaa ambaye alimuunganisha na viongozi wa jamii na hatimaye suala hilo kufikishwa kwa Mkurugenzi Mtendaji wa TAYOTA, George Bwire.
Mapambano yaliyoratibiwa kwa pamoja Bwire anafafanua kuwa, kisa hicho kiligundulika kupitia mtandao wa siri wa watoa taarifa wa kijamii ulioundwa chini ya mradi wa Pamoja Tuwalinde.
“Tulipata taarifa kutoka kwa mwenyekiti,” anaeleza. “Tumewapatia mafunzo watu mbalimbali katika kila kata ambao jukumu lao ni kutoa taarifa za siri kuhusu visa vye sura hii.”
Kutokana na mfumo huo thabiti unaohusisha viongozi wa mitaa, vijana na wakazi waliopatiwa mafunzo, hatua za haraka zilichukuliwa kwa kuwahusisha
Maofisa Ustawi wa Jamii na Jeshi la Polisi. Ili kuhakikisha usalama wake wakati taratibu za kisheria zikiendelea, Eliza alikabidhiwa kwa muda chini ya uangalizi wa Bwire.
Safari ya uponyaji
Safari ya uponyaji haikuwa rahisi. “Mara tu baada ya kufanyiwa vipimo vya kitabibu, Eliza alilia sana,” anasema Bwire.
Alipatiwa huduma za ushauri kutoka kwa mtaalamu wa saikolojia na mwongozo wa kiroho kutoka kwa kiongozi wa dini.
“Mwanzoni ilikuwa ngumu kuona tabasamu lake. Alikuwa mtu wa kujifungia ndani mwenyewe na kujiweka mbali na watu,” anaeleza Mkurugenzi huyo huku akisema kuwa hivi sasa amebadilika.
“Hivi sasa ni mchangamfu. Anaweza kuchangamana na watu, kwa kweli.” Eliza anakumbuka vizuri namna alivyopata msaada na anakiri kuwa kwa sasa anajisikia amani.
Wakati huohuo, taratibu za kisheria ziliendelea ambapo Eliza alifanikiwa kumtambua mtuhumiwa mbele ya mamlaka. Mtuhumiwa alikamatwa na kesi ikapelekwa mahakamani.
Vitendo vya unyanyasaji vilisababisha Eliza kukimbia nyumbani kwao ili kutafuta usalama.
Kujenga kesho iliyo bora
Mbali na ulinzi, zilifanyika jitihada nyingine za kumtafutia fursa Eliza za kukabiliana na maisha. Baada ya kutofanya vizuri katika mtihani wake wa Darasa la Saba, hakudhani kama bado ana fursa tena ya kuendelea na elimu.
Jambo pekee lililokuwa linazunguka kichwani mwake ni kugeukia mafunzo ya ufundi stadi.
Kupitia ufadhili wa mfuko wa kisaikolojia wa TangaYetu, sasa Eliza anasoma masuala ya upishi (catering) katika Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).
“Nataka kuishi kwa uhuru na kujitegemea na pia kuwasaidia wengine wanaopitia changamoto kama nilizopitia mimi,” anasema Eliza kwa matumaini.
Somo endelevu
Mkasa wa Eliza ni fundisho kuhusu umuhimu wa mifumo ya jamii iliyoratibiwa vizuri katika kupambana na ukatili dhidi ya watoto.
Ingawa bado kuna changamoto kama shinikizo la familia kunyamaza na ucheleweshaji wa kesi, kama anavyosema Bwire, mradi wa Pamoja Tuwalinde unaendelea kuimarisha ushirikiano kati ya jamii, vyombo vya dola na maofisa ustawi.
Eliza anatoa wito kwa wazazi kuwa na utamaduni wa kuwasikiliza watoto wao. Leo hii, Eliza anatumia muda wake mwingi jikoni akijifunza fani aipendayo, huku akifurahi na wale wanaomzunguka bila wasiwasi wowote.
Na hili ndilo lengo kuu la mradi: kuzuia ukatili inapowezekana, kupaza sauti haraka pale tatizo linapojitokeza, na kutoa msaada endelevu kwa wahanga kujenga upya maisha yao kwa kulinda utu wao.
Programu ya TangaYetu inafadhiliwa na Fondation Botnar na kusimamiwa na INNOVEX Development Consulting Limited kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Tanga, ikiwa na lengo la kuifanya Tanga kuwa mji ambapo vijana wanaweza kustawi.
