
Maadhimisho hayo pia yanasisitiza kuwa michezo inaweza kuwa daraja la kuleta amani na mshikamano duniani.
Mambo matano ya kufahamu kuhusu siku hii:
- Kuanzishwa kwake – Siku hii ilianzishwa rasmi na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2024. Umoja wa Mataifa ulipitisha azimio namba A/RES/78/310 bila kupingwa na kutangaza rasmi Mei 19 kuwa World Fair Play Day. Maadhimisho rasmi ya kwanza duniani yalianza mwaka 2025.
- Lengo lake – Ni kuhamasisha michezo yenye heshima na usawa. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, haki kwenye michezo si kushinda pekee, bali ni kucheza kwa kuheshimu sheria, wapinzani, waamuzi na kuzingatia uadilifu. Siku hii pia inapinga ubaguzi, vurugu na vitendo visivyo vya haki michezoni.
- Kuleta mabadiliko ya kijamii – Umoja wa Mataifa unaamini kuwa michezo inayozingatia haki inaweza kusaidia kujenga jamii zenye mshikamano, kuvuka tofauti za tamaduni na kuwapa vijana nafasi ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii zao.
- Kujengwa kwenye misingi ya maadili ya Olimpiki – Umoja wa Mataifa unaeleza kuwa dhana ya haki kwenye michezo imejikita katika maadili ya Olimpiki yanayosisitiza urafiki, mshikamano, uvumilivu na kuheshimiana. Hivyo siku hii inalenga kuendeleza roho hiyo ndani na nje ya viwanja vya michezo.
- Ujumbe mkuu wa Umoja wa Mataifa – Kupitia maadhimisho hayo, Umoja wa Mataifa unatoa wito kwa dunia kukumbatia roho ya haki kwenye michezo kwa sababu haki kwenye michezo au fair play “hujenga heshima miongoni mwa washiriki” na kusaidia kuunganisha watu bila kujali tofauti zao.
Zaidi kuhusu siku hii tembelea ukurasa wake maalum katika wavuti wa Umoja wa Mataifa kwa kubofya hapa.
