Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero kwa kushirikiana na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo na Mamlaka ya Hali ya Hew…Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero kwa kushirikiana na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo na Mamlaka ya Hali ya Hew…

Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero kwa kushirikiana na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania wanatekeleza mradi wa kuimarisha ustahimilivu na uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa serikali za mitaa, wameanza hatua za utekelezaji wa mradi huo unaotarajiwa kudumu kwa miaka mitatu.

Akiwasilisha mada kwa wadau kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, mtafiti mkuu wa mradi huo Profesa Christopher Mahonge alisema mradi huo unalenga kuongeza uwezo wa watumishi wa serikali za mitaa katika kupanga na kutekeleza shughuli za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa ufanisi zaidi.

Profesa Mahonge alisema mradi huo unatumia mfumo wa utafiti shirikishi kwa vitendo (Participatory Action Research) ambao unahusisha tathmini ya hali halisi kwa kutumia hojaji, mahojiano na mijadala ya pamoja ili kubaini changamoto zilizopo pamoja na njia bora za kukabiliana nazo.

Alieleza kuwa mradi huo umejengwa katika dhana kwamba watumishi wa serikali za mitaa wakipewa maarifa, zana na uzoefu wa vitendo wataweza kupanga na kutumia taarifa zinazohusiana na mabadiliko ya tabianchi kwa ufanisi mkubwa zaidi.

“Tutafanya tathmini shirikishi ili kutambua mapungufu ya kitaalamu na kitaasisi, kisha kuandaa mafunzo yatakayosaidia kuongeza uwezo wa watumishi katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi,” alisema Profesa Mahonge.

Aidha alisema kutakuwa na mfumo wa kujifunza kwa pamoja kupitia mbinu ya “Walimu wa Walimu” (Training of Trainers – ToT) ili kuhakikisha uendelevu wa maarifa kwa kuwajengea uwezo washiriki ambao nao wataendelea kuwafundisha wengine katika jamii zao.

Kwa mujibu wa Profesa Mahonge, suluhisho zitakazopatikana kupitia mradi huo zitakuwa zimetokana na mazingira halisi ya eneo la Mvomero pamoja na ushirikiano wa karibu kati ya wataalamu, watafiti na jamii husika.

(Feed generated with FetchRSS)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *