Tanga. Wakulima wa zao la kakao wilayani Muheza wameeleza namna mfumo wa stakabadhi ghalani ulivyobadilisha maisha yao kwa kuwapa soko lenye uhakika na bei nzuri tofauti na zamani walipokuwa wakitegemea walanguzi.
Kupitia mfumo huo pamoja na kilimo hai, wakulima wa vijiji mbalimbali wameanza kuona matokeo ya jasho lao kwa kujenga nyumba za kisasa, kusomesha watoto na kupanua mashamba yao ya kakao.
Mkulima wa Kijiji cha Shembekeza, Ramadan Rugambwa, anasema alianza kulima kakao mwaka 1995 wakati ambao soko la zao hilo halikuwa na uhakika na wanunuzi walipanga bei kwa matakwa yao.
“Wakati huo tulianza kuuza kilo kwa Sh200, baadaye ikafika Sh500 hadi Sh700. Soko lilikuwa linayumba sana,” anasema Rugambwa.
Anasema hali ilianza kubadilika baada ya wakulima kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Muheza kuanzisha mfumo wa stakabadhi ghalani uliowapa nafasi ya kuuza mazao yao kwa ushindani wa bei kupitia minada rasmi.
Wakulima wa Kakao wakikagua mashamba yao wakiwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, DKT Jumaa Muhina mwenye kaunda suti. Picha na Mbonea Herman
Kwa mujibu wa Rugambwa, mfumo huo umemwezesha kuboresha maisha yake ikiwemo kujenga nyumba ya kisasa na kusomesha watoto wake.
“Msimu wa kwanza nilianza msingi wa nyumba yangu, wa pili nikafika hatua ya madirisha na sasa niko kwenye lenta. Kabla ya mfumo huu sikuwa na matumaini ya kufanya jambo kama hili,” anasema.
Anasema pia ameongeza uzalishaji kutoka ekari moja hadi kuvuna kakao yenye thamani ya kati ya Sh10 milioni na Sh12 milioni kwa msimu, tofauti na zamani alipokuwa akipata kati ya Sh2 milioni na Sh3 milioni kwa mwaka.
Kilimo cha Pilipilimanga kinachofanywa kwa wingi na wakulima katika tarafa ya Amani wilaya ya Muheza mkoani Tanga.
Hata hivyo, anataja changamoto za magonjwa ya mimea na mabadiliko ya tabianchi, akisema kutokana na mfumo wa kilimo hai hawaruhusiwi kutumia kemikali kali hivyo hulazimika kutumia njia za asili kudhibiti wadudu na magonjwa.
Mkulima mwingine, Zaina Kaniki, anasema zamani wakulima walikuwa wakikopa fedha kwa walanguzi na kulazimika kuuza kakao kwa bei ndogo wakati wa mavuno.
“Lakini sasa wakulima tunaweka hata akiba benki na tuna uwezo wa kupanga matumizi yetu,” anasema.
Kaniki anasema mafanikio ya zao hilo yamemwezesha kununua kiwanja na kuanza kujenga nyumba yake mwenyewe.
Kwa upande wake, Sofia Ngumulo anasema kilimo cha kakao sasa kina tija kubwa zaidi kuliko zamani kwani kimemwezesha kumsomesha mwanawe shule ya kulipia na kununua shamba jingine.
Mpango wa uuzaji wa mazao kwa njia ya Stakadhi Galani unaotajwa kuwanufaisha wakulima wa Kokoa katika wilaya ya Muheza Mkoani Tanga.Picha na Mbonea Herman.
Katibu Mtendaji wa Muka Amcos, Mwanahawa Seleman, anasema tofauti kubwa iliyopo sasa ni kwamba soko limesogezwa karibu na wakulima kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani.
Kaimu Ofisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Nyeza Adam, anasema kakao na mazao ya viungo yanazalishwa zaidi kwa mfumo wa kilimo hai unaohitajika katika soko la Ulaya na maeneo mengine duniani.
Aidha, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Jumaa Muhina, anasema Serikali kwa kushirikiana na wadau imetoa miche zaidi ya laki mbili ya kakao na mazao ya viungo katika misimu ya 2025 na 2026 ili kuongeza uzalishaji na kuinua uchumi wa wananchi.
