
Dar es Salaam. Chozi la maumivu limetawala uso wa mwalimu mstaafu, Magreth Jacob aliyelalamika kuibiwa Sh46 milioni baada ya kadi yake ya benki kunasa kwenye mashine ya kutolea fedha (ATM) huku akigharamia Sh12 milioni kwa askari polisi kumsaka mhusika wa wizi huo.
Magreth, mkazi wa Babati mkoani Manyara ametoa malalamiko hayo mbele ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba Jumapili ya Mei 17, 2026 aliyekuwa ziarani Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma kuzungumza na kusikiliza kero za wananchi.
Mama huyo aliyesafiri kutoka mkoani Manyara hadi Dodoma kuwasilisha kero yake kwa Waziri Mkuu, amesema baada ya kustaafu Januari 2020, Oktoba mwaka huo alipata mafao yake ya kustaafu kazini.
Amesema baada ya kupokea fedha hizo kupitia akaunti ya benki alifunga safari kwenda kuchukua fedha kidogo kwa ajili ya kujikimu.
“Nilikwenda Benki ATM, baada ya kuweka kadi ilimezwa na ilikuwa siku ya upigaji kura Oktoba 28, 2020 hivyo benki ilikuwa imefungwa niliwaeleza polisi wakaniambia hadi siku ya kazi.
“Siku iliyofuata ilikuwa ni sherehe za Maulid kwa hiyo, siku ya tatu ndio nilikwenda benki na nilipofika na kuwaeleza walitafuta kadi na hawakupata,” amesimulia mama huyo.
Magreth ambaye sasa ni mjane, amesema baada ya maofisa wa benki kubaini kadi hiyo haipo aliulizwa kama anafahamu namba ya akaunti ya kadi yake na alipotaja na kuangaliwa akaunti yake ilibainika fedha zilishatolewa kupitia mawakala mbalimbali.
Amedai kuwa, mawakala ambao wametumika kutoa fedha zake ni kutoka mkoani Arusha na Dar es Salaam.
Mama huyo amesema baada ya kuelezwa fedha zake zimetolewa, alianguka kwa shinikizo la damu na kupoteza fahamu.
Amesimulia wakati huo mumewe alikuwa hai na ndiye aliyepewa taarifa na kufika haraka eneo la tukio na kupashwa habari hizo na hapo alishauri taarifa itolewe polisi.
“Tulikwenda polisi Wilaya ya Babati na tukaandikisha maelezo, baada ya kuandikisha walisema twende Polisi Mkoa wa Manyara ambao walichukua jukumu la kwenda kuwasaka hao mawakala.
“Nimetoa gharama yangu mimi, gari aina ya Noah imetoka Wilaya ya Babati wamechukua fedha za mafuta juu yangu, askari watatu, wamekwenda kulala nyumba za wageni za maana Dar es Salaa juu yangu na ni fedha zangu nilizokopa,” amesema.
Magreth amesema kwa takribani wiki nzima walifanya kazi ya kuwasaka wezi, baadaye walitoa taarifa wezi wale hawaonekani, lakini watawachukua mawakala ambao miamala imefanyika kwao na wezi hao.
Baada ya hatua hizo, askari hao walikwenda tena Iringa kwa gari la kukodi akitoa takwimu kwamba, mchakato wote huo wa kuwagharamia askari hao ulikuwa Sh12 milioni na hakuambulia jambo lolote.
“Hadi sasa hamna kitu chochote nilichokipata zaidi ya kupoteza fedha zangu benki na hela zangu ambazo nimepoteza nje, naomba msaada wako Waziri Mkuu, mimi ni mama mjane nalea watoto yatima wanne mamangu mimi mzee namlea,” ameeleza mama huyo.
Magreth amesema changamoto yake ya kuibiwa tayari iliwasilishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Makosa ya Jinai (DCI) lakini hakupata msaada wowote hadi wakati anawasilisha kero hiyo.
Katikati ya misukosuko hiyo, mama huyo akiendelea kusikilizwa na Waziri Mkuu ameeleza ugumu alioupitia kupata nafasi ya kuwasilisha changamoto yake hiyo hata kiongozi huyo alipofika Babati mkoani Manyara kusikiliza kero ya wananchi.
“Waziri Mkuu ulikuja Wilaya ya Babati sikupata muda wa kuongea na wewe, nikakimbia Katesh sikupata muda wa kuongea na wewe.”
Amesema aliposikia yupo mkoani Dodoma alifunga safari na alilala Chemba na hata nauli ya kumfikia aliungaunga.
Baada ya kumsikiliza mama huyo, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu ameelekeza mama huyo asaidiwe na atamuona kabla ya kuondoka.
Akizungumzia kero hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) Tusekelege Mwaikasu amesema kitendo cha kadi ya benki ya mama huyo kutokutwa kwenye mshine ya ATM ilipaswa benki husika kutumia kamera kubaini waliochukua kadi hiyo au kudhibitisha kama kweli mama huyo alikuwa anatoa fedha kupitia mashine ya benki hiyo.
“Kamera ndio ingeonesha mama alitaka kutoa hela haikutoka, kama benki haina udhibitisho wowote kama ile kadi imepotelea kwenye ATM sasa benki itakuwa na ushahidi gani kama kweli alikwenda kwenye ATM husika.”
Hata hivyo, Tusekelege amesema kwa miaka mingi wamekuwa wakiwaelimisha watu wanapokuwa wanaweka namba zao za siri kutoa fedha kuhakikisha wanaficha ili kama kuna mtu ameweka kamera kwalengo la kutaka kuiba asifanikiwe.
“Kuna wezi ambao wanaweka kitu kama ndoano, unaona umeweka kadi alafu unapoandika namba za siri kamera inakuwa kama inaona vile unabonyeza,”amesema.
Kwahiyo kadi yako inaonesha kama haitoki wewe unaona imenasa kumbe kuna mwizi ameweka mtego na aliona namba yako ya siri, sasa unapoondoka anakuja anavuta anaondoka na kadi na mamba yako ya siri.”
Mkurugenzi huyo amesema ushahidi wa kwanza wa wizi wa mama huyo ulipaswa kuanzia kwenye ATM na kama benki itasema kamera zake hazikuwa zinafanya kazi siku hiyo ndipo uwajibikaji wa benki husika unaingia kumlipa mama huyo.
Maelezo ya kanuni
Kulingana na kanuni za mwaka 2019 zilizotangazwa kwenye Gazeti la Serikali na Benki kuu ya Tanzania (BoT) zinatoa wajibu za mabenki na taasisi za kifedha kulinda wateja wake.
Wajibu huo ni benki kutoa taarifa kuhusu njia mbalimbali zinazoweza kusababisha wizi, upotevu au udanganyifu katika fedha za mteja pamoja na kumpatia mteja taarifa kuhusu miamala yake kwa kipindi.
Pia, kanuni hizo zinaruhusu mteja kuwasilisha malalamiko yake Benki Kuu endapo hatapata suluhisho au kutoridhika na utatuzi wa malalamiko yake kutoka kwa Benki au Taasisi ya Kifedha.
