Mlipuko wa Ebola nchini DRC: Bado kuna sintofahamu kuhusu maambukizi yalivyoanza na kusambaa – WHOMlipuko wa Ebola nchini DRC: Bado kuna sintofahamu kuhusu maambukizi yalivyoanza na kusambaa – WHO

Kasi ya kuzuia maambukizi ya virusi vya Bundibugyo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC vinavyosababisha ugonjwa wa Ebola inazidi kuongezeka wakati huu ambapo idadi ya watu wanaoshukiwa kuambukizwa ni zaidi ya 500, wanaoshukiwa kufa ni 130 huku watu waliothibitshwa kufa kwa ugonjwa hu oni 30.

WHO ambalo ni shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani, linasema wanashirikiana na mamlaka za serikali ili kupeleka haraka Mashariki mwa taifa hilo vifaa zaidi vya kupima wagonjwa na kutambua maambukizi ya virusi vya Bundibugyo, ambavyo havina chanjo wala tiba wakati huu ambapo uwezekano wa kuanza kutoa chanjo ya Ervebo ni miezi kadhaa baadaye.

Mwakilishi wa WHO nchini DRC Dkt. Anne Ancia, amesema “tuna hali kubwa ya kutokuwa na uhakika kuhusu idadi ya maambukizi na jinsi virusi vilivyosambaa.”

Akizungumza na waandishi wa habari huko Geneva, Uswisi,  kutoka Bunia mji mkuu wa jimbo la Ituri, ambako wagonjwa wamegunduliwa awali, Dkt. Ancia amesema kuwa mlipuko huo umefika pia jimbo la Kivu Kaskazini, huku wagonjwa waliothibitishwa wakirekodiwa Butembo na Goma jimboni humo. Uganda pia imethibitisha wagonjwa wawili waliowasili kutoka nje ya nchi hiyo.

Jumapili asubuhi, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, alitangaza mlipuko huo kuwa dharura ya afya ya umma ya kimataifa, akieleza wasiwasi kuhusu “ukubwa na kasi ya janga hilo”.

Bado kuna sintofahamu kuhusu jinsi na mahali mlipuko ulipoanza.

“Sidhani kama tumempata ‘mgonjwa wa kwanza’ kwa sasa,” amesema Dkt. Ancia akiongeza kwamba, “tunachojua kwa sasa ni kwamba tarehe 5 Mei, kulikuwa na mtu aliyefariki Bunia. Mwili ulirudishwa Mongbwalu na kuwekwa kwenye jeneza. Kisha familia ikaamua kuwa jeneza hilo halikumfaa marehemu. Kwa hiyo wakabadilisha jeneza. Halafu kulikuwa na mazishi, na hapo ndipo mlipuko ulipoanzia.”

Kilicho wazi ni kwamba hakuna tiba iliyoidhinishwa.

Ugunduzi wa wagonjwa wa awali ulipunguzwa kasi kutokana na ukweli kwamba vipimo vya eneo la Bunia vilionesha matokeo hasi kwa aina ya Ebola ya Zaire. Dalili nyingi tofauti — homa, uchovu, kuhara na kutapika — zilifanya utambuzi wa haraka kuwa mgumu zaidi, pamoja na changamoto ya kwamba kutokwa damu puani, dalili inayohusishwa pia na ugonjwa huo, haikuanza hadi siku ya tano ya maambukizi, afisa huyo wa WHO ameeleza.

Mwisho wa yote, ni kupitia vipimo vilivyofanywa Kinshasa mji mkuu wa DRP, ndipo uwepo wa virusi vya Bundibugyo ulithibitishwa.

Dkt. Ancia amesema kuwa kuna juhudi za kimataifa kuzingatia chanjo au matibabu yanayoweza kusaidia kupambana na mlipuko huo. Kikundi cha ushauri wa kiufundi cha WHO kilitarajiwa kukutana leo Jumanne alasiri “kutoa mapendekezo zaidi kwa WHO na nchi wanachama kuhusu ni chanjo gani inayopaswa kupewa kipaumbele”, alieleza.

Ervebo, chanjo dhidi ya virusi vya Ebola ya Zaire, inazingatiwa,” amesema mwakilishi huyo wa WHO, lakini “itachukua miezi miwili kabla haijapatikana”.

Jamii ndio ina ufunguo wa kudhibiti maambukizi

Ingawa chanjo inaweza kuongeza kinga na ulinzi kwa watu walioathirika, ufunguo wa kudhibiti maambukizi uko katika kazi za kijamii ndani ya jamii ili kuongeza uelewa, kupambana na taarifa potofu na kuhakikisha watu wanafuata hatua za usafi, hasa wakati wa mazishi.

“Ikiwa tutatumia hatua za kulazimisha na wananchi wasikubali, tutaona miili ikitoweka. Tutaona wagonjwa wanaoshukiwa kuwa na maambukizi wakikataa kwenda hospitali na vituo vya afya,” Dkt. Ancia ameonya, akisisitiza ushirikiano endelevu wa wahudumu wa afya na shule, makanisa na viongozi wa jamii.

WHO inaunga mkono mwitikio unaoongozwa na Serikali kwa kuwa na zaidi ya wataalamu 40 wa afya waliopo eneo la tukio pamoja na kupeleka vifaa na uwezo wa ziada wa uchunguzi, katika kile kinachoelezwa kuwa “mazingira magumu sana ya kiafya, kiutendaji na kibinadamu”, yanayoambatana na ukosefu wa usalama na watu kuhama makazi yao.

Hofu kwa wakimbizi – UNHCR

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) nalo limesema leo kuwa majimbo yaliyoathirika ya Ituri na Kivu Kaskazini yana zaidi ya watu milioni mbili waliokimbia makazi yao ndani ya nchi na waliorejea, huku uwezo wa huduma za afya ukiwa umedhoofishwa na migogoro.

Pia kuna wasiwasi kuhusu wakimbizi wanaoishi katika maeneo yaliyoathirika. Huko Ituri, wakimbizi wapatao 11,000 kutoka Sudan Kusini wanahitaji msaada wa kinga dhidi ya ugonjwa huo, huku katika mji mkuu wa Kivu Kaskazini, Goma, unaoshikiliwa na waasi, zaidi ya wakimbizi 2,000 kutoka Rwanda na Burundi wakihitaji vifaa vya usafi.

Ebola ya Zaire

Mlipuko wa hivi karibuni wa virusi vya Ebola ya Zaire nchini DRC ulimalizika Desemba 2025, na athari za kisaikolojia za janga kubwa lililotokea Kivu Kaskazini na Ituri mwaka 2018-19 bado zinaendelea miongoni mwa wananchi.

Dkt. Ancia amesisitiza kuwa ingawa inaweza kuchukua miezi miwili kabla chanjo haijapatikana, “si kwamba mlipuko utaisha ndani ya miezi hiyo miwili. Kumbukeni ule wa awali, ulichukua miaka miwili.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *