Simba, Yanga kwenye mtego wa Nusu Fainali CRDBSimba, Yanga kwenye mtego wa Nusu Fainali CRDB

HUENDA ikashuhudiwa Kariakoo Dabi ya tano msimu huu iwapo Simba na Yanga zitavuka vikwazo vya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho la CRDB, mechi zinazotarajiwa kuchezwa Juni 20 na 21 mwaka huu.

Msimu huu, miamba hiyo miwili tayari imekutana mara nne katika mashindano yote, mbili zilikuwa Ligi Kuu Bara, moja ya Ngao ya Jamii na nyingine fainali ya Kombe la Muungano.

Katika mechi hizo nne, Yanga imeshinda moja Septemba 16, 2025 kwenye Ngao ya Jamii baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Pacome Zouzoua. Mechi mbili za ligi zilimalizika bila ya mbabe, ikianza 0-0, kisha 2-2, huku Simba ikiondoka na heshima ya kutwaa Kombe la Muungano kwa ushindi wa bao 1-0.

Sasa macho yanaelekezwa kwenye nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB, huku kila timu ikiwa na kibarua kizito mbele yake kabla ya kufikia Kariakoo Dabi nyingine katika mchezo wa mwisho wa michuano hiyo kwa msimu huu wa 2025-2026.

Kwa upande wa Simba, itavaana na Coastal Union katika mchezo ambao utakuwa na presha ya aina yake kutokana na mwenendo wa timu hizo kwenye ligi. Mechi hii imepangwa kuchezwa Juni 20, mwaka huu kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.

Coastal imekuwa ikipewa nafasi ndogo mara nyingi lakini imeonyesha uwezo wa kuwasumbua vigogo, ikumbukwe imetinga hatua hiyo baada ya kuing’oa Singida Black Stars kwa penalti 4-2.

Yanga itakuwa na kazi ya kukabiliana na Azam, timu ambayo imeendelea kuwa mwiba kwa vigogo misimu ya hivi karibuni kutokana na ubora wa kikosi chake.

Kinachoongeza uzito wa michezo hiyo ni ukweli timu hizo pia zitakutana katika Ligi Kuu Bara katika kipindi kifupi, hali inayofanya kila mechi kuwa na sura mbili tofauti, mapambano ya ubingwa wa ligi pamoja na vita ya kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB.

Yanga dhidi ya Azam itachezwa Juni 21 mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Kwa Simba, ratiba inaanza kwa mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Coastal Union utakaochezwa Mei 21 mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, kabla ya timu hizo kurudiana tena kwenye nusu fainali ya kombe hilo.

Kwa Yanga wao wataanza kwanza kucheza na Azam kwenye Kombe la Shirikisho la CRDB kabla ya kutifuana katika ligi, Juni 24, 2026.

Hali hiyo inatarajiwa kuongeza presha kwa makocha wa timu hizo ambao watalazimika kupanga vikosi vyao kwa umakini mkubwa ili kuepuka kupoteza uelekeo katika mbio za mataji mawili kwa wakati mmoja.

TAKWIMU ZINAVYOSEMA

Simba na Coastal Union wamekutana jumla ya mechi 26 tangu 2011 hadi 2026, na 25 zikiwa ni Ligi Kuu na moja ya Ngao ya Jamii. Katika rekodi hiyo, Simba imeshinda mechi 17, sare nane na kupoteza mara moja pekee dhidi ya Coastal Union.

Mechi pekee ambayo Simba ilifungwa ni Machi 23, 2014 na Coastal Union iliibuka na ushindi wa bao 1-0. Kwa upande wa mabao, Simba imeifunga Coastal Union jumla ya mabao 44 katika mechi hizo huku ikiruhusu jumla ya mabao 12 katika historia hiyo (2011–2026).

Kwa upande wa Yanga na Azam wamekutana jumla ya mechi 34 tangu 2010 hadi 2026 katika mashindano mbalimbali yakiwemo Ligi Kuu (LKB), Ngao ya Jamii, Kombe la FA na mashindano ya kimataifa.

Katika rekodi hizo, Yanga imeshinda mara 14, Azam ikishinda mara 10 huku mechi 10 zikiisha sare, jambo linaloonyesha ushindani mkubwa kati ya timu hizi mbili kila wanapokutana.

Kwa upande wa mabao, Yanga imeifunga Azam jumla ya mabao 43 huku Azam  ikiwa imeifunga Yanga mabao 35.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *