BAADA ya Yanga kumkosa mshambuliaji Moses Shumah wa Power Dynamos ya Zambia, sasa timu hiyo imehamishia hesabu zake kwa Junior Koutiama anayeichezea Polisi Kenya.

Moses Shumah mwenye umri wa miaka 23 amekuwa kwenye kiwango cha juu sana akivunja rekodi katika Ligi Kuu ya Zambia kwa kufunga mabao 20 msimu huu, hatua iliyovutia macho ya mabosi wa Jangwani ambao wameanza harakati za haraka za kumpata lakini wanakutana na kizingiti kigumu.

Hata hivyo, taarifa za hivi karibuni zinaeleza Yanga inapata upinzani mkali kutoka kwa Ama Zulu FC ya Afrika Kusini, ambao nao wameingilia kati dili hili ili kujaribu kumnasa mshambuliaji huyo na hivyo wameamua kubadilisha upepo haraka.

Mpango wa Yanga wa kusaka straika mwingine unatokana na mikakati ya klabu hiyo ya kuimarisha safu ya ushambuliaji na huenda ikaachana na mshambuliaji Laurindo Dilson Maria Aurelio ‘Depu’ ambaye alitua Jangwani dirisha dogo msimu huu akiwa hadi sasa ameshafanikiwa kufunga mabao sita kwenye michezo aliyocheza.

MASHI 01

Yanga kwa sasa bado ipo kwenye wakati mzuri wa kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu Bara ikiwa inaongoza kwenye msimamo kwa kuwa na pointi 60 zikiwa ni mbili mbele ya Simba kwa sasa zikibaki mechi tano kwa kila timu.

HESABU MPYA ZIKO HAPA

Yanga baada ya kukutana na upinzani kwa Moses taarifa zinasema kuwa kwa sasa inapambana kuhakikisha kuwa inampata Koutiama ambaye amekuwa kwenye kiwango bora akiwa na Polisi.

Raia huyo wa Burkina Faso mwenye umri wa miaka 27. Amekuwa kwenye kiwango bora sana tangu alipojiunga na klabu ya Kenya Police FC mwezi Januari mwaka huu akitokea klabu ya USFA ya kwao.

MASHI 02

REKODI ZILIVYOWAVUTA YANGA

Koutiama ambaye amesajiliwa na Polisi kwa mkataba wa miaka mitatu, ndio kwanza ametumika nusu msimu pekee, lakini ameuonyesha ubabe wake kwenye ligi hiyo.

Kilichowavutia Yanga ni rekodi zake ambazo ameziweka ndani ya muda mfupi ambao amecheza, kwani mpaka sasa Polisi Kenya imemaliza ligi ikiwa nafasi ya tatu na pointi 55 huku yeye akicheza mechi 18, amefanikiwa kufunga mabao 10 ndani ya muda mfupi tangu aliposajiliwa huku akichaguliwa kuwa mchezaji bora wa kigeni kwenye ligi hiyo iliyomalizika hivi karibuni.

MASHI 03

YANGA MEZANI

Mwanaspoti linafahamu, Yanga tayari imeshafika mezania na kuzungumza na Polisi kusaka saini ya mshambuliaji huyo ambaye bado ana mkataba mrefu na klabu hiyo, hivyo mazungumzo yanayoendelea ni ya makubaliano kati ya pande hizo mbili kuhusu biashara hiyo.

Taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti, Yanga iko kwenye mazungumzo na Polisi ili kuangalia uwezekano wa kumnunua mchezaji huyo ambaye amewavutia sana mabosi hao.

“Yanga ilidhani Depu atawaka mapema sana, lakini bahati mbaya haijawa hivyo ndio maana wameamua kusaka mashine mpya itakayokuja kuongeza nguvu kwani msimu ujao haitaki mchezo kwenye kila michuano itakayoshiriki.”

Katika nafasi hiyo ya ushambuliaji Yanga ina vyuma vitatu ambavyo ni Depu na Prince Dube, huku mzawa Clement Mzize akiwa anasumbuliwa na majeraha ambayo yamemfanya akae nje msimu mzima.

Hivyo kama Yanga inasaka mshambuliaji maana yake kuna mmoja anaondoka, ambapo inadaiwa kuwa kuna uwezekano mkubwa akawa Depu, ili ipatikane nafasi ya mgeni mmoja.

Msimu huu (2025/2026), mpaka sasa, Dube ameshafunga mabao 09 kwenye ligi akiwa miongoni mwa vinara wa ufungaji wa timu hiyo, huku Depu akiwa nayo sita, kiongozi wa mabao wa timu hiyo ni Allan Okello mwenye 11.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *