
Dodoma. Ni majira ya jioni jua limepungua mwanga na kukaribisha ubaridi kidogo, lango linafunguliwa na kuruhusu mtu kuingia ndani ya Shule ya Watoto wadogo ya Sherishshcool. Nami naingia kwa kukaribishwa na mwenyeji wangu lakini kwa mbali zinasikika sauti za watoto wachanga.
Sauti inayosikika ni ya mtoto mchanga anayetajwa kwa jina la Naima lakini pembeni yake wamelala Naila na Nilan ingawa wao hawalii kwa wakati huu.
Ninapoingia ndani ya chumba kikubwa chenye hewa ya kutosha, nakutana na mwenyeji wangu Rehema Ally na kabla ya kuketi, anasogea mbele kidogo anainama kwenye kitanda kikubwa na kumbeba mtoto huku akisema “Naima unataka nini mbona kilio,”.
Rehema ni yule mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma ambaye hivi karibuni taarifa zake zilisambaa kuhusu bahati aliyoipata ya kujifungua watoto watatu kwa wakati mmoja wakiwemo watoto wa kike wawili na wa kiume mmoja.
Ujio wangu hasa unalenga kujua maisha ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma hasa linapokuja suala la masomo na ndoa mambo ambayo yametajwa na baadhi ya wanafunzi wenyewe na pengine hata kutoka kwa wananchi majirani na chuo.
Ndani ya simulizi ya Rehema (mama watatu) kuna mshangao hasa linapokuja swali la kwa nini yametokea haya kwa mwanafunzi, lakini nyuma yake kuna funzo ambalo linaweza kuelezeka kwa kutumia msemo wa wahenga kuwa, kuteleza si kuanguka.
Rehema anayesoma kozi ya Maendeleo ya Jamii anakiri kuwa alipata ujauzito kutoka kwa mwanafunzi mwenzake anayesoma kozi ya Sheria wote wakiwa Udom na hata alipomweleza namna ambavyo amekuwa mjamzito, wawili hao kwa pamoja waliweka mkakati kwanza wa kuikubali hali hiyo na kusubiri Mungu awaongoze kuhusu nini kitakachotokea. Mahojiano yangu na yeye yalikuwa hivi:
Swali: Je, hamkujua kuwa ninyi ni wanafunzi na kwa maana hiyo mlipaswa kuachana na mambo mengine ili msome kwanza?
Jibu: Baba mambo hayo sipendi sana kuyasimulia maana ni kama yananiumiza lakini namshukuru Mungu kwamba nilifanikiwa kupiga moyo konde, licha ya changamoto nilizopitia bado naendelea na masomo yangu na Mola wangu ananipigania mwaka huu nitamaliza lakini baba wa watoto hawa yeye atamaliza mwakani.
Swali: Hii kauli ya kwamba Udom wanafunzi wanaishi kama mke na mume na baada ya kumaliza masomo yao ndoa zao huvunjika unaizungumziaje?
Jibu: Hiyo ni ngumu kuisimulia ingawa ipo kwa kiasi fulani maana pale wanasoma watu wazima, lakini sipendi kuisemea kwa undani hasa maisha yanayomhusu mtu mwingine.
Swali: Vipi mapokeo kwa jamii na wazazi wako baada ya kuonekana umekuwa na ujauzito huku ukiendelea na masomo?
Jibu: Kwa jamii yalikuwa maneno kiasi pamoja na wanafunzi wenzangu lakini ‘muziki’ ulikuwa kwa wazazi na hasa mama, nakuambia palichimbika lakini mwishowe ilibidi aikubali hali yangu na akaanza kunitia moyo.
Naamini wazazi waliona nikiumizwa kwa maneno labla ningeweza kupoteza mwelekeo ikiwemo ndoto ya masomo yangu halafu ingekuwa njia mbaya hata kwa watoto wengine wadogo.
Swali: Unawaeleza nini wanafunzi wenzako kuhusu masomo na kujiingiza kwenye uhusiano?
Jibu: Nawashauri mabinti na vijana kokote wanakosoma wasikimbilie uhusiano kabla ya kumaliza masomo yao, hii inawapa ugumu wa kutimiza ndoto zao na wakati mwingine inawafikirisha sana wazazi.
“Vijana wenzangu hasa wasichana waache kudanganyika kwenye mambo mengine nje ya masomo. Uhusiano na mapenzi vipo hasa baada ya kumaliza masomo, hakuna jambo ambalo linapita isipokuwa masomo yana muda wake yakikupita na ukashindwa kumaliza ndiyo basi tena.
Swali: Kwa haya uliyopitia, unatamani kufanya nini?
Jibu: Natamani kuwa balozi mzuri kwa wasichana na wanavyuo, Nafikiria siku za usoni niwe msomi mkubwa lakini mwanaharakati nitakayetenga muda wangu kwa ajili ya kuwapa elimu vijana hasa wasomi wa vyuo vikuu.
Swali: Rehema sasa tuzungumzie malezi ya watoto na ndoto yako kwa siku za usoni
Jibu: Kwanza kama unavyoona, sijawahi kuwa na mawazo ya kukata tamaa, naendelea kupambana na masomo katika kozi yangu na kumshauri baba wa watoto naye asife moyo, kwani tumepata watu wa kutusaidia kuwalea watoto sisi tumebaki na kazi ya kusoma tu.
Nikiwa darasani sifikirii habari za watoto ndani ya vipindi kwani nikifanya mambo mawili kwa wakati mmoja, yanaweza kunipoteza na nisijue cha kufanya.
Swali: Unatengaje muda wako kati ya kuwalea watoto na masomo?
Jibu: Namshukuru Mungu, mama mwenye hiki kituo cha watoto ni mtumishi wa Udom ambaye aliamua kunisaidia kwa kunihifadhi hapa. Anatumia gharama zake kubwa kunisaidia na malezi ya watoto lakini kukubali kunipa wasaidizi wa kuwalea watoto. Kweli namshukuru sana.
