Wanafunzi wa Veta waunda simuWanafunzi wa Veta waunda simu

Kibaha. Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi na Huduma (Veta) Mkoa wa Pwani kimeingia hatua za mwisho za kubuni na kutengeneza simu ya mkononi kwa kutumia teknolojia ya ndani.

Akizungumza katika mahafali ya 17 ya chuo hicho yaliyofanyika leo Jumanne Mei 19, 2026, eneo la Kongowe, Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Mashariki, Dk John Mwanja, amesema kuwa simu hiyo tayari inaweza kupiga na kupokea pamoja na kutuma ujumbe mfupi.

Maboresho yanayoendelea, amesema ni kuunganisha huduma za intaneti na mitandao ya kijamii ili kuifanya simu hiyo ikidhi mahitaji ya sasa ya watumiaji.

“Teknolojia hii ni ya kwetu. Tunataka kupunguza utegemezi wa vifaa kutoka nje na kuongeza uzalishaji wa ndani kwa kutumia wataalamu wetu,” amesema.

Dk Mwanja amesema mradi huo umetokana na maelekezo ya Serikali yaliyotolewa mwaka 2025 wakati wa Maonyesho ya Sabasaba, Dar es Salaam, yakihimiza taasisi za elimu ya ufundi kuendeleza ubunifu wa teknolojia za ndani.

Amebainisha kuwa tayari wamejadiliana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kupata namba maalumu za matumizi ya simu hiyo na hatua zilizobaki ni za ukamilishaji kabla ya uzinduzi rasmi.

Mwalimu wa Ufundi wa Veta Kongowe, Hamis Salumu, amesema mradi huo unalenga kupunguza gharama za simu nchini na kuongeza matumizi ya bidhaa zinazotengenezwa na Watanzania.

“Tunataka Watanzania watumie bidhaa zao wenyewe. Hii itasaidia kupunguza gharama na kuimarisha uchumi wa ndani,” amesema Salumu.

Mkuu wa chuo hicho, Crala Kibodya amesema chuo kinakabiliwa na changamoto za miundombinu ikiwamo uhaba wa mabweni, samani na barabara, hali inayoathiri mazingira ya kujifunzia.

Amesema wanahitaji ushirikiano wa wadau ili kuboresha mazingira ya mafunzo na kuongeza ufanisi wa wanafunzi.

Katika risala yao, wahitimu 72 wameiomba Serikali kuongeza mikopo kwa wanafunzi wa Veta ili kuwasaidia kukabiliana na gharama za mafunzo kwa vitendo.

“Tunaomba mikopo iongezwe kwa sababu wakati wa mafunzo kwa vitendo tunakutana na gharama nyingi,” amesema Furaha Boazi kwa niaba ya wahitimu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *