
Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mbeya kimewataka viongozi na makatibu wake kwenda kwa wananchi kusikiliza na kutatua kero zao badala ya kubaki ofisini.
Kauli hiyo imetolewa leo Mei 20, 2026 na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa CCM Mkoa wa Mbeya, Ndele Mwaselela wakati wa kikao na makatibu wa chama hicho kutoka wilaya tano za Mkoa wa Mbeya.
Mwaselela amesema viongozi wa CCM wanapaswa kubadili mfumo wa utendaji kwa kuwa karibu zaidi na wananchi ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu yao.
Amesema chama kimekuwa kikitoa vyombo vya usafiri ikiwemo baiskeli na pikipiki kwa viongozi wa ngazi mbalimbali ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Lengo ni kuwafikia wananchi kwa urahisi katika maeneo mbalimbali, kusikiliza na kutatua kero zao. Nendeni mkatekeleze majukumu yenu kwa vitendo na kueleza yale yaliyofanywa na Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema.
Mwaselela amesema viongozi wa chama wana wajibu wa kuielimisha jamii kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa nchini.
Kwa upande wake, Katibu wa CCM Wilaya ya Mbarali, Malanyingi Matukuta amesema wamepokea maelekezo hayo na watahakikisha wanawafikia wananchi pamoja na kusikiliza changamoto zao.
“Tutaendelea kutekeleza maelekezo haya kwa ufanisi na kutoa mrejesho kwa wakati,” amesema.
Naye kada wa CCM kutoka Kata ya Mbalizi Road, Grace Mapunda amesema maelekezo hayo yataongeza uwajibikaji kwa viongozi wa chama na kusaidia kushughulikia changamoto za wananchi kwa haraka.
Mkazi wa Mbeya, Zainab Hashim amesema viongozi wa chama wanapaswa kuendelea kufanya ziara na mikutano ya hadhara ili kusikiliza wananchi moja kwa moja na kujenga imani zaidi kwa jamii.
