Marekani. Kutangazwa kwa majina ya wanaowania tuzo za BET kumezua mjadala mitandaoni baada ya mashabiki kugundua kuwa staa wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz, hakufanikiwa kupata uteuzi katika orodha ya mwaka huu.
Kutokuwapo kwa Diamond kumewakatisha tamaa mashabiki wake ambao wamekuwa wakiamini kuwa mafanikio yake makubwa barani Afrika na duniani yalitosha kumpatia nafasi kwenye tuzo hizo zinazotambua mchango wa wasanii weusi katika muziki, filamu, televisheni na michezo.
Wakati Diamond akikosekana katika tuzo hizo, rapa Kendrick Lamar ameongoza kwa kupata uteuzi mwingi zaidi baada ya kutajwa katika vipengele vitano tofauti, sambamba na Mariah the Scientist.
Kwa mujibu wa ripoti ya Billboard wasanii wengine waliopata uteuzi katika vipengele vinne ni Doechii, Doja Cat, Clipse, Teyana Taylor pamoja na Latto.
Wengine ambao wamepata uteuzi katika vipengele vitatu ni A$AP Rocky, Bruno Mars, Bryson Tiller, Chris Brown, Jill Scott, Kehlani, Metro Boomin, SZA, Tasha Cobbs Leonard, T.I. pamoja na YK Niece.
Kutokuwapo kwa Diamond kumeibua tena mjadala kuhusu nafasi ya muziki wa Tanzania katika soko la kimataifa, licha ya ukuaji mkubwa wa Bongo Fleva kwenye majukwaa ya kidigitali na ushawishi wake unaozidi kuongezeka ndani na nje ya Afrika.
Baadhi ya wachambuzi wa burudani wanaeleza kuwa changamoto kubwa kwa wasanii wa Tanzania ni ukosefu wa mtandao mpana wa kimataifa, promosheni hafifu katika masoko makubwa ya muziki pamoja na ushirikiano mdogo na kampuni kubwa za muziki duniani.
Hali hiyo ni tofauti na nchi kama Nigeria na South Africa ambazo zimewekeza kwa muda mrefu katika kuusukuma muziki wao kwenye soko la dunia.
Kwa mara nyingine, majina yaliyotawala uteuzi kutoka Afrika yametoka zaidi Nigeria na Afrika Kusini, kutoka kwa mastaa kama Burna Boy, Wizkid, Tems, Asake na Tyla.
Waandaaji wa BET wamesema uteuzi wa mwaka huu unaonyesha ubunifu mkubwa na mafanikio ya watu weusi duniani katika sekta mbalimbali za burudani na michezo.
Hafla ya BET Awards 2026 inatarajiwa kufanyika Juni 28, 2026 jijini Los Angeles, Marekani, huku ikitarajiwa kurushwa mubashara kupitia majukwaa mbalimbali duniani.
