Takukuru Mtwara yaokoa Sh87 milioni, wakulima walipwaTakukuru Mtwara yaokoa Sh87 milioni, wakulima walipwa

Mtwara. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mtwara, imefanikiwa kuokoa zaidi ya Sh87.3 milioni, fedha ambazo zilikuwa katika hatari ya kupotea kupitia ucheleweshaji wa malipo, ubadhirifu na usimamizi usioridhisha wa miradi ya maendeleo.

Akitoa taarifa ya Januari hadi Machi, kwa waandishi wa habari leo Jumatano Mei 20, 2026, Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mtwara, Mwanakombo Rajabu amesema fedha hizo zimepatikana kupitia ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo, pamoja na uchunguzi wa mifumo ya kiutendaji Serikali, sekta binafsi na kwa wananchi.

Amesema sehemu kubwa ya fedha zilizorejeshwa ni malipo ya wakulima wa korosho yaliyokuwa yamecheleweshwa kwa muda mrefu.

Amesema Takukuru imerejesha Sh40.88 milioni ambazo zilikuwa hazijalipwa kwa wakulima katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mtwara.

Ameeleza kuwa kati ya fedha hizo, Sh34.4 milioni zilikuwa malipo ya wakulima 35 wa korosho kutoka Amcos za Namahonga, Langana, Kuchele, Chimbuko, Madaba na Bahari katika Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba.

“Wakulima hao walikuwa hawajapatiwa fedha zao za mauzo ya korosho za msimu wa 2025/2026 hadi pale Takukuru tulipoingilia kati na kufuatilia suala hilo kupitia vyama vyao vya msingi,” amesema

Katika hatua nyingine, Takukuru imeokoa Sh6.4 milioni zilizokuwa malipo ya wakulima sita wa Muungano Amcos katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara.

Fedha hizo zilikuwa zimecheleweshwa kwa takribani miezi mitatu na kampuni ya Isram Commodities Co. Ltd baada ya kununua korosho kupitia mnada wa soko la awali.

Mbali na sekta ya kilimo, Takukuru pia ilielekeza nguvu zake katika miradi ya maendeleo ya Serikali, hususan sekta ya elimu.

Rajabu amesema taasisi hiyo imefanikiwa kuokoa Sh29.2 milioni kupitia ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi mbalimbali.

Amesema Sh25 milioni ziliokolewa katika Wilaya ya Tandahimba ambapo fedha hizo zilikuwa zimelipwa kwa mzabuni wa vifaa vya ujenzi wa matundu 10 ya vyoo katika Shule ya Msingi Mlanje.

“Mzabuni huyu baada ya kupokea fedha hizo za umma, mzabuni huyu alitoweka na kusababisha mradi kusimama, tukalifuatilia suala hili kwa makini sana,” ameeleza.

Katika Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu, Takukuru pia iliokoa Sh4.2 milioni kupitia mradi wa Shule ya Sekondari Michiga baada ya kubaini kuwa madirisha yaliyowekwa hayakuwa na viwango vilivyoainishwa kwenye BOQ ya mradi huo.

Aidha, katika Halmashauri ya Wilaya ya Newala, ilizuia ubadhirifu wa Sh2.9 milioni zilizokuwa katika mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Uchunguzi ulionyesha baadhi ya maafisa maendeleo ya jamii waliingiza majina ya watu wasiostahili kunufaika na mikopo hiyo katika mfumo wa malipo.

Takukuru ilisimamia kuondolewa kwa majina hayo na kuhakikisha nafasi hizo zinachukuliwa na walengwa halali waliokusudiwa kunufaika na mpango huo.

Sambamba na hilo, Takukuru ilifanikisha kurejeshwa kwa Sh300,000 kupitia ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari Mtunguru wilayani Newala.

“Uchunguzi ulionyesha kuwa kampuni ya GIK Construction Limited haikutozwa faini ya asilimia 0.1 kwa kuchelewesha kukamilisha kazi baada ya mkataba wake kuvunjwa Januari 13, 2025,” ameeleza

Katika tathmini ya jumla ya miradi ya maendeleo, Rajabu amesema Takukuru imefuatilia miradi 32 yenye thamani ya zaidi ya Sh7.8 bilioni na kubaini changamoto mbalimbali ikiwemo matumizi ya vifaa visivyo na ubora, ujenzi usiofuata michoro iliyosanifiwa pamoja na wizi wa vifaa vya ujenzi.

Amesema baadhi ya miradi iliyobainika kuwa na kasoro hizo ipo katika sekta za barabara, afya, elimu, maji, ujenzi na utawala.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *