Kituo utafiti wa maendeleo dhidi ya umaskini Afrika chazinduliwaKituo utafiti wa maendeleo dhidi ya umaskini Afrika chazinduliwa

Kibaha. Viongozi wa vyama sita vya ukombozi Kusini mwa Afrika wamekutana Kibaha mkoani Pwani kushuhudia uzinduzi wa Kituo cha Utafiti wa Maendeleo na Mapambano dhidi ya Umaskini kilichopo katika Shule ya Uongozi ya Julius Nyerere.

Kituo hicho kilichozinduliwa leo Mei 20, 2026, kinabeba falsafa za maendeleo za Rais wa China, Xi Jinping na kinatajwa kuwa jukwaa la kujifunza mbinu zilizosaidia China kuwaondoa zaidi ya watu milioni 800 kwenye umaskini kati ya mwaka 2012 na 2021.

Katika kuanza shughuli zake, kituo hicho kimepokea zaidi ya vitabu 200 vinavyoelezea sera na uzoefu wa China katika maendeleo ya vijijini, uwezeshaji wa wananchi na mapambano dhidi ya umaskini.

Picha washiriki wa uzinduzi kituo cha utafiti cha Rais Wa China Kibaha Pwani. Picha na Sanjito Msafiri

Uzinduzi huo umehudhuriwa na viongozi kutoka vyama vya ukombozi vikiwamo Chama cha Mapinduzi (CCM), African National Congress, Swapo, MPLA, Frelimo pamoja na Zanu–PF.

Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Asha-Rose Migiro amesema mshikamano wa vyama vya ukombozi una historia kubwa katika harakati za ukombozi na maendeleo ya wananchi.

“Tunatarajia kituo hiki kitasaidia kubadilishana uzoefu wa maendeleo na kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya umaskini,” amesema Dk Migiro.

Kwa upande wake, Richard Kasesela amesema kituo hicho kitasaidia viongozi wa Afrika kupata maarifa ya utekelezaji wa sera za maendeleo, ikiwemo maendeleo ya vijijini, matumizi ya teknolojia na uwekezaji wa miundombinu.

Mkuu wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Marcelina Chijoriga amesema kituo hicho kitaongeza uwezo wa taasisi hiyo kutoa mafunzo kwa kada mbalimbali zikiwemo sekta ya umma na binafsi.

Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Asha-Rose Migiro

Uzinduzi huo umetajwa kuwa sehemu ya kuimarisha ushirikiano kati ya China na mataifa ya Kusini mwa Afrika katika tafiti, maendeleo na mapambano dhidi ya umaskini.

Vyama vya ukombozi Kusini mwa Afrika vilianza kushirikiana tangu miaka ya 1960 wakati wa harakati za kupigania uhuru dhidi ya ukoloni na ubaguzi wa rangi, huku Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi zilizokuwa mstari wa mbele kusaidia wapigania uhuru wa mataifa mbalimbali ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *