Kauli ya Chatanda yaiponza CCM, Msajili ailima baruaKauli ya Chatanda yaiponza CCM, Msajili ailima barua

Dar es Salaam. Siku chache baada ya Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT), Mary Chatanda kutoa kauli zinazotafsiriwa na baadhi ya wananchi kuchochea chuki na hasira, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imeiandikia barua CCM na kukitaka kijieleze kuhusiana na kauli hizo.

Chatanda alitoa kauli hizo Mei 18, 2026 mkoani Iringa wakati wa kampeni za kumnadi mgombea ubunge kwa tiketi ya chama hicho wa Ismani, Emmanuela Mtatifilokolo, anayewania nafasi iliyoachwa wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, William Lukuvi aliyefariki dunia Machi 25, 2026.

Katika hotuba yake, kauli iliyozua mjadala mtandaoni na kuvuta hisia ya wadau wengi wa demokrasia ni pale aliposema kuwa angekabidhiwa mamlaka ya nchi hata kwa dakika moja, watu aliowaita wanaotumika kutoka nje ya nchi sijui kama wangekuwepo.

Msingi wa kauli yake hiyo aliijenga wakati anakosoa waliopanga matukio ya vurugu yaliyojitokeza wakati na baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025, akisema anasikitishwa na watu waliopoteza maisha kutokana na ghasia hizo.

“Nasema, kama ningekabidhiwa nchi hii hata kwa dakika moja tu! Mama Samia, sijui kama wale watu wangekuwepo. Wamemkuta ndugu yetu mpendwa, Dk Samia, akiwa mpole, mnyenyekevu na msikivu.

“Wakisema jambo, anawasikiliza; mara amewafungulia waliokuwa jela, mara ameenda kunywa nao chai kule Ikulu, halafu wanarudi tena kumtukana. Mimi nisingeweza,” alisema.

Katika maelezo yake Chatanda alienda mbali zaidi akidai anasikia watu hao wanapanga kufanya maandamano ya kumtoa Tundu Lissu huku akisema “unajua unaweza kwenda mjinga kurudi si mjinga tena.”

“Sasa unaangalia hiyo ni siasa ya aina gani, hatujazoea sisi, tumezoea kila mmoja anaeleza jambo lake hapo, mkimaliza mnapiga kura kila mmoja anaondoka aliyepatikana hewala tunasubiri tena hadi miaka mitano,”alisema Chatanda.

Baada ya mjadala na kauli hiyo, leo Jumatano, Mei 20, 2026, Mwananchi limemtafuta Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza ambaye amesema ofisi yake imezipokea video na taarifa za matamshi hayo na tayari imechukua hatua.

“Kuhusu suala la Chatanda, nasi Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa tumetumiwa video na picha hizo, na tumeshaiandikia CCM barua ili wawasilishe maelezo kuhusu suala hilo,” amesema Nyahoza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *