Wadau wachambua uteuzi majaji tisa Mahakama ya RufaniWadau wachambua uteuzi majaji tisa Mahakama ya Rufani

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan, amewateua majaji tisa wa Mahakama Kuu kuwa majaji wa mahakama ya rufani, huku wataalamu wa sheria wakisema uteuzi huo unaleta ahueni katika mahakama hiyo, japokuwa unaacha pengo walikotoka.

Uteuzi wa majaji hao, utaifanya Mahakama ya Rufani kuwa na jumla ya majaji 49, kutoka 40 waliopo sasa.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka ametangaza uteuzi huo kupitia taarifa ya Ikulu leo Jumatano Mei 20, 2026 iliyotiwa saini na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari Machumu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, walioteuliwa ni Abdi Kagomba, aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Yohane Masara aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha na Immaculata Banzi aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kagera.

Wengine walioteuliwa ni Rabia Mohamed aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Cyprian Mkeha aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara Dar es Salaam na Yose Mlyambina aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi Dar es Salaam.

Pia, wamo Imani Aboud aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mzee Ibrahim aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar na Juliana Masabo aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wateule hao wataapishwa tarehe itakayopangwa baadaye.

Pengo laachwa, lazibwa

Akizungumzia hilo, mwanasheria, August Mramba amesema ingawa uteuzi huo unapunguza upungufu wa majaji uliokuwepo katika Mahakama ya Rufani, kwa upande mwingine unatengeneza pengo katika Mahakama Kuu.

“Huku (Mahakama Kuu) umeacha gap (nafasi) kubwa wakati kule juu (Mahakama ya Rufani) utapunguza gap. Haina tofauti sana na kupandisha mshahara halafu bei ya vitu ikapanda,” amesema.

Amesema kilichofanywa ni kizuri, lakini bado haitakidhi haja ya idadi ya mashauri yaliyopo mahakamani, ukizingatia kila siku yanaongezeka kutokana na kuongezeka kwa uhalifu na watu.

“Idadi ya mashauri ni kubwa mno, inaongezeka kila mwaka. Ujue kuna mahakimu wanastaafu, kuna majaji wanastaafu kila mwezi na wapo wanaofariki. Idadi ya wanaoondoka ofisini ni kubwa kila mwaka,” amesema.

Ameeleza mamlaka ya uteuzi inapaswa kuongeza watumishi wengi kadiri iwezavyo, miundombinu, vitendea kazi na kuwa na tathmini ya idadi ya mashauri yanayofunguliwa kila mwaka.

“Sio kwamba mzigo unapungua, maana ukiangalia wanaostaafu ni wengi hukohuko Mahakama ya Rufani kwa sababu umri wa mwisho kuhudumu ni miaka 65,” amesema.

Hata hivyo, Wakili Sweetbert Nkuba, anaona uteuzi huo utaongeza ufanisi wa utendaji katika mahakama husika, kwa kuwa idadi ya majaji itaongezeka na kuwa haona kama kutaleta upungufu mkubwa.

“Dhamira ya uteuzi huo ni kuongeza ufanisi na hilo litatimia kwa kuwa walioteuliwa wataenda kuongeza idadi ya watumishi kutoka wale waliokuwepo,” amesema.

Alipoulizwa haoni kuwa itapunguza majaji wa Mahakama Kuu, amesema hakuna upungufu mkubwa katika mahakama hiyo, hivyo hakutashuhudiwa uhaba.

“Ukizingatia wale majaji wameteuliwa kutoka kanda tofauti na maeneo mbalimbali, hawakutoka sehemu moja, hivyo itasaidia kuleta ufanisi,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *