Siku 100 za majonzi kwa familia ya mwanamke aliyetoweka ArushaSiku 100 za majonzi kwa familia ya mwanamke aliyetoweka Arusha

Arusha. Huzuni imeendelea kutanda katika familia ya Scola Chuwa (45), mkazi wa mtaa wa Ndarivoi jijini Arusha, baada ya juhudi za kumtafuta kugonga mwamba.

Scola anadaiwa kutoweka Februari 8, 2026 baada ya kuaga nyumbani kwake saa tisa mchana akieleza kuwa anakwenda kwenye msiba wa jirani. Hadi jana, alikuwa ametimiza siku 100 bila kuonekana.

Taarifa za kupotea kwake ziliripotiwa katika Kituo cha Polisi Unga Ltd na kufunguliwa jalada namba UNG/RB/277/26 kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, SACP Justine Masejo, amesema anahitaji muda kufuatilia taarifa hizo kabla ya kutoa ufafanuzi rasmi.

“Naomba muda nifuatilie, kwa sababu bado sina taarifa kamili kuhusu tukio hilo. Nitatoa taarifa endapo kutakuwa na jambo la kufafanua,” amesema.

Akizungumzia tukio hilo, mume wa Scola, Solomon Kivuyo, amesema mke wake aliondoka nyumbani Februari 8, 2026 saa tisa mchana akieleza kuwa anakwenda kushiriki msiba wa jirani, lakini tangu siku hiyo hajarudi tena.

“Tumehangaika kila mahali kumtafuta hadi leo hakuna matumaini yoyote,” amesema.

Baba mdogo wa Scola, Lazaro Chuwa, amesema mara ya mwisho kumuona ndugu yake huyo ilikuwa Januari 2026 alipokwenda Moshi kumuuguza mama yao mzazi.

“Baada ya kukaa kwa miezi miwili kijijini, mume wake alifika Februari 2, 2026 akitaka waondoke pamoja na mama yao kwa ajili ya matibabu zaidi mkoani Arusha,” amesema.

Lazaro amesema awali Scola alikataa kuondoka kijijini, lakini baadaye alikubali kurejea Arusha baada ya kushawishiwa.

Amesema tangu Scola alipoondoka kijijini hawakuwahi kumuona tena hadi walipopata taarifa za kutoweka kwake.

Awali, mume wa Scola alisema siku ya kutoweka kwake aliacha simu yake ya mkononi nyumbani, jambo lililofanya juhudi za kumtafuta kuwa ngumu zaidi.

“Angekuwa na simu tungeweza kufuatilia alipo au kujua kama amepatwa na tatizo au yupo salama,” amesema.

Kwa mujibu wa mume huyo, tukio hilo limewaathiri kisaikolojia wanafamilia wote, hususan watoto wao wanne ambao wameendelea kumuulizia mama yao bila majibu.

“Hali hii imetupa mashaka makubwa sisi wanafamilia, hasa ndugu na watoto wetu. Tunaomba wananchi wenye taarifa zozote zinazoweza kusaidia kumpata mke wangu watoe ushirikiano kwa familia au vyombo vya usalama.

“Na kama yeye mwenyewe atapata taarifa hizi, basi arejee nyumbani, familia yake inaendelea kumsubiri,” ameongeza huku akilia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *