Wataalamu waeleza matumizi sahihi ya AIWataalamu waeleza matumizi sahihi ya AI

Dar es Salaam. Teknolojia ya Akili Unde (AI) imeendelea kutajwa nyenzo muhimu inayorahisisha ujifunzaji, utafiti na uchambuzi wa taarifa, huku wataalamu wakisisitiza umuhimu wa matumizi sahihi ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.

Hayo yamesemwa leo Jumatano, Mei 20, 2026 na Mtaalamu wa teknolojia wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Mahadia Tunga wakati akiwasilisha mada katika wiki ya ubunifu ya chuo hicho.

Amesema AI ni teknolojia inayowezesha kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa kupitia maelekezo sahihi ya mtumiaji, lakini bado hutegemea akili ya kibinadamu katika kutoa majibu na uchambuzi.

“AI inaamini akili ya kibinadamu, nyuma yake kuna akili ya binadamu ambayo kupitia maelekezo sahihi ya mtumiaji ndiyo huisaidia teknolojia hiyo kujua na kutoa kitu ambacho binadamu angefanya,” amesema.

Amesema maendeleo ya mifumo ya kompyuta yameifanya AI kuwa na uwezo mkubwa wa kutafuta na kuchakata taarifa mitandaoni tofauti na mifumo ya zamani, hali iliyopanua matumizi yake katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu na tafiti.

Amebainisha kila teknolojia mpya huwa na mjadala kuhusu athari zake kwa akili ya binadamu, lakini baadaye hukubalika na kuwa sehemu ya maisha ya kawaida.

“Hata vikokotoo vilipoingia walimu waliandamana wakisema vitadumaza akili za wanafunzi kwenye hesabu, lakini baadaye vikakubalika na leo vinatumika kila mahali,” amesema.

Inavyotumika katika utafiti

Katika eneo la utafiti, amesema AI inarahisisha hatua za awali za mtafiti kwa kusaidia kubaini pengo la tafiti zilizofanyika na maeneo ambayo bado hayajafanyiwa kazi.

“Kwa kutumia AI, mtafiti anaokoa muda kwa kupata kazi zilizofanywa katika eneo husika na kujua eneo mahsusi la kufanyia utafiti badala ya kwenda maktaba kusoma kazi kwenye karatasi,” amesema.

Ameongeza teknolojia hiyo pia inasaidia kuchambua tafiti zenye uzito na kufupisha taarifa kutoka vyanzo mbalimbali rasmi, hatua inayorahisisha upatikanaji wa maarifa kwa watumiaji.

Hata hivyo, ameonya matumizi ya AI yanahitaji tahadhari kubwa hasa katika kulinda taarifa binafsi na siri za taasisi, akisema teknolojia hiyo huhifadhi na kusambaza taarifa kirahisi.

“Ukichukua data za siri na kuziingiza kwenye ChatGPT, inaweza kukufanyia uchambuzi lakini pia kuzihifadhi kwa ajili ya kujifunza. Ndiyo maana taarifa nyeti zinahitaji uangalifu mkubwa,” amefichua.

Amesema ili kuepuka kutumia taarifa zisizo rasmi kutokana na yteknolojia hiyo, watumiaji wanapaswa kuhakikisha wanaiomba AI kutaja vyanzo vya taarifa inazotoa ili kujiridhisha na ubora na uhalali wa maudhui hayo.

“Ukipata jibu, ujue pia limetoka wapi kwa kuitaka itaje vyanzo vya taarifa hizo, baadhi ya mifumo ya AI kutumia marejeo ya zamani yasiyoendana na wakati, hali inayoweza kushusha ubora wa maudhui au kusababisha upotoshaji wa taarifa,” amesema.

Pia amesema matumizi yasiyo sahihi ya AI yanaweza kuchangia wizi wa kazi za kitaaluma na ukiukwaji wa haki miliki iwapo watumiaji hawatataja vyanzo vya taarifa walizotumia.

Taasisi ziweke Sera ya AI

Kutokana na hali hiyo, ameshauri taasisi kuweka sera na miongozo maalumu ya matumizi ya AI ili kuhakikisha teknolojia hiyo inatumika kwa manufaa ya kitaaluma bila kuleta madhara.

Tayari baadhi ya taasisi ikiwemo Kampuni ya Mwananchi Communications Limited, iliyotangaza sera yake ya matumizi ya AI hivi karibuni zimeshazindua Sera hiyo, ikiwa ni mkakati wa kwenda na kasi ya maendeleo ya teknolojia bila kuathiri ubunifu na matumizi ya akili ya binadamu katika kulinda misingi ya kitaaluma na kimaadili.

Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Dk Suleiman Ikomba amesema matumizi ya AI hayawezi kuepukika katika dunia ya sasa kutokana na mchango wake katika kurahisisha upatikanaji wa maarifa.

“Hii teknolojia ni nzuri kwa sababu inasaidia kupata maarifa ambayo ni vigumu kuyapata. Kadiri dunia inavyoendelea haya ni mabadiliko yasiyoepukika,” amesema.

Hata hivyo, amesema teknolojia hiyo haipaswi kuua ubunifu wa watumiaji wake, akisisitiza umuhimu wa elimu ya Tehama na upatikanaji wa vifaa kwa jamii ili kuitumia kwa mafanikio.

“Watu hawatakiwi kuwa tegemezi wa AI. Tunahitaji elimu ya matumizi ya teknolojia pamoja na tahadhari ili matumizi yake yasilete madhara,” amesema.

Naye mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (Duce), Baraka Fukwe amesema AI imekuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi katika kutafuta maarifa kwa haraka zaidi.

“Inasaidia sana kutafuta maarifa kwa urahisi. Badala ya kwenda maktaba, siku hizi unaweza kupata kila kitu kirahisi kupitia ChatGPT,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *