Ronaldo aipa Al Nassr ubingwa wa Saudi ArabiaRonaldo aipa Al Nassr ubingwa wa Saudi Arabia

Riyadh, Saudi Arabia. Nahodha wa timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo, ameiongoza Al Nassr kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Saudi Arabia ‘Saudi Pro League’ baada ya timu yake kuifunga Damac mabao 4-1 katika mchezo wa mwisho wa msimu.

Ronaldo amefunga mabao mawili katika ushindi huo ulioipa Al Nassr taji la ligi kwa mara ya kwanza tangu nyota huyo ajiunge na klabu hiyo Januari 2023 akitokea Manchester United.

Huo ni ubingwa wa 11 wa ligi kwa Al Nassr lakini ukiwa wa kwanza ndani ya kipindi cha Ronaldo akiwa klabuni hapo, huku timu hiyo ikimaliza msimu kwa tofauti ya pointi mbili dhidi ya wapinzani wao Al Hilal.

Al Nassr waliingia kwenye mchezo huo wakiwa na presha kubwa baada ya kushindwa kutwaa ubingwa wiki iliyopita kufuatia sare ya 1-1 dhidi ya Al Hilal iliyotokana na makosa ya dakika za mwisho ya golikipa Bento.

Mbali na hilo, timu hiyo pia imetoka kwenye maumivu ya kupoteza fainali ya AFC Champions League Two dhidi ya Gamba Osaka mwishoni mwa wiki iliyopita, ilipokubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Wajapan hao.

Katika mchezo dhidi ya Damac, Sadio Mané alianza kuifungia Al Nassr kabla ya Kingsley Coman kuongeza bao la pili katika kipindi cha pili, huku Ronaldo akihitimisha ushindi huo kwa mabao mawili yaliyoihakikishia timu yake ubingwa.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 41 ameendelea kuwa mhimili mkubwa wa Al Nassr tangu ajiunge na klabu hiyo, akiwa tayari amefikisha zaidi ya mabao 100 ndani ya misimu mitatu aliyocheza Saudi Arabia.

Kwa ubingwa huo, Ronaldo sasa ameandika historia ya kutwaa mataji ya ligi nchini Ureno, England, Hispania, Italia na Saudi Arabia.

Mbali na ubingwa huo, Ronaldo anatarajiwa kuiongoza timu ya taifa ya Ureno katika Kombe la Dunia 2026 litakalokuwa la sita kwake kushiriki mashindano hayo makubwa duniani.

Taji jingine pekee ambalo Ronaldo amewahi kushinda akiwa na Al Nassr ni Kombe la Klabu Bingwa za Kiarabu mwaka 2023, mashindano ambayo hayatambuliwi rasmi na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *