Makosa ya kila siku yanayopandisha sukariMakosa ya kila siku yanayopandisha sukari

Watu wengi wanaoishi na kisukari huamini kuwa kiwango cha sukari,  hupanda tu kutokana na kula vyakula vitamu au kutumia sukari nyingi kwenye chai na vyakula.

Hata hivyo, kuna makosa mengi ya kila siku yanayoweza kuongeza sukari kwenye damu bila mtu kutambua mapema.

Baadhi ya tabia hizo zimekuwa sehemu ya maisha ya kawaida kwa watu wengi wenye kisukari, hali inayofanya udhibiti wa ugonjwa huo kuwa changamoto hata kwa wanaojitahidi kufuata ushauri wa kitabibu.

Moja ya makosa yanayotajwa mara nyingi ni kuruka milo, hasa kifungua kinywa.

Watu wengine huamini kuwa kutokula husaidia kushusha sukari, lakini hali hiyo inaweza kuufanya mwili ushindwe kudhibiti kiwango cha sukari vizuri. Baada ya kukaa muda mrefu bila kula, ini huanza kutoa sukari nyingi ili mwili na viungo vingine viendelee kufanya kazi, jambo linaloweza kusababisha sukari kupanda zaidi ya kawaida.

Tatizo jingine ni matumizi ya vinywaji vinavyoonekana kuwa salama kwa wagonjwa wa kisukari.

Baadhi ya juisi za viwandani, vinywaji vya kuongeza nguvu na hata baadhi ya aina za mtindi wenye ladha, vina kiwango kikubwa cha sukari kuliko wengi wanavyodhani.

Wataalamu wa lishe wanashauri watu wenye kisukari kusoma taarifa za virutubisho kwenye vifungashio kabla ya kutumia bidhaa hizo.

Kutofanya mazoezi pia ni sababu kubwa inayochangia kupanda kwa sukari. Maisha ya kukaa muda mrefu ofisini, kwenye magari au kutumia muda mwingi kutazama runinga, huufanya mwili kushindwa kutumia sukari ipasavyo. Hata mazoezi mepesi kama kutembea kwa dakika 30 kila siku yanaweza kusaidia mwili kutumia insulin kwa ufanisi zaidi na kusaidia kuyeyusha sukari pamoja na mafuta mwilini.

Wataalamu pia wanaonya kuhusu msongo wa mawazo. Watu wenye kisukari wanapaswa kufahamu kuwa mawazo mengi, hofu na kukosa utulivu vinaweza kuongeza kiwango cha sukari kwenye damu.

Mwili unapokuwa kwenye hali ya msongo huzalisha homoni zinazochochea kuongezeka kwa sukari kama sehemu ya mwitikio wa mwili dhidi ya presha au hatari.

Aidha, kukosa usingizi wa kutosha ni tatizo jingine linalopuuzwa na wengi. Kulala kwa muda mfupi au kuwa na ratiba mbaya ya usingizi kunaweza kuathiri namna mwili unavyotumia insulin.

Watu wanaokesha mara kwa mara au wanaolala kwa saa chache,  wako kwenye hatari kubwa ya kushindwa kudhibiti sukari vizuri.

Tabia nyingine hatari ni kuamini taarifa zisizo sahihi kutoka mitandaoni au kwa watu wasiokuwa wataalamu wa afya. Baadhi ya wagonjwa huacha au hupunguza matumizi ya dawa bila ushauri wa daktari, wakiamini wanaweza kupona kisukari au kushusha sukari haraka kwa njia nyingine.

Wataalamu wa afya wanaonya kuwa kufanya hivyo kunaweza kuwa hatari na kusababisha sukari kupanda zaidi pamoja na madhara mengine kiafya. Elimu sahihi inabaki kuwa silaha muhimu katika kudhibiti kisukari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *