
Dar es Salaam. Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imewatahadharisha wananchi dhidi ya matumizi ya dawa ya binadamu ya Vega-100 inayodaiwa kuuzwa kiholela katika maeneo mbalimbali nchini huku ikipiga marufuku utengenezaji, uingizaji, usambazaji na uuzaji wa dawa ya mifugo ya Hi-tet 120.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa juzi na Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo, mamlaka hiyo inalenga kulinda afya ya jamii dhidi ya matumizi ya dawa ambazo ubora, usalama na ufanisi wake haujathibitishwa.
Inaeleza kuwa, dawa ya Vega-100 haijasajiliwa nchini na imekuwa ikikamatwa mara kwa mara kupitia operesheni na ukaguzi wa kawaida unaofanywa sokoni.
Kwa mujibu wa TMDA uchunguzi wake umebaini kuwapo kwa wafanyabiashara wasio waaminifu, wanaojihusisha na usambazaji na uuzaji wa dawa hiyo katika maeneo mbalimbali nchini.
Inaelezwa kuwa, dawa hiyo ina kiambata hai cha Sildenafil Citrate na lebo zake zinaonesha kuwa, imetengenezwa na Kampuni ya Signature Pharmaceuticals Limited ya India.
Kwa mujibu wa TMDA, dawa hiyo hutumika kuongeza nguvu za kiume kwa wanaume wenye tatizo la kushindwa kusimamisha uume wakati wa tendo la ndoa.
“Tunaonya matumizi holela ya dawa hii yanaweza kusababisha madhara makubwa kiafya ikiwamo kushuka kwa presha, uume kubaki umesimama kwa muda mrefu zaidi ya saa nne, kupoteza uwezo wa kuona ghafla na matatizo ya kusikia yanayoambatana na milio masikioni,” inaeleza.
Madhara mengine yaliyotajwa ni pamoja na kuumwa kichwa, kuona maluelue, pua kujaa makamasi, kiungulia, kushindwa kumeng’enya chakula vizuri pamoja na maumivu ya misuli na mgongo.
“TMDA inapenda kuutahadharisha umma kuwa, dawa tajwa haifai kwa matumizi ya binadamu na ubora, usalama na ufanisi wake haujathibitishwa kwa kuwa haijasajiliwa,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Katika hatua nyingine, mamlaka hiyo imetangaza kupiga marufuku dawa ya mifugo yenye jina la Hi-tet 120 baada ya kubaini kuwapo kwa vitendo vya udanganyifu vinavyohusisha kubadilisha lebo na kufungasha upya dawa hiyo kabla ya kuirudisha sokoni.
TMDA inaeleza kuwa, dawa hiyo yenye kiambata hai cha ‘Oxytetracycline Hydrochloride’ imekuwa ikiuzwa kwa bei ya juu sokoni kuliko dawa nyingine zenye kiambata kama hicho, jambo lililochochea baadhi ya wafanyabiashara kufanya udanganyifu kwa lengo la kujipatia faida isiyo halali.
Kwa mujibu wa TMDA, uchunguzi umeonesha kuwa kifungashio cha dawa hiyo ni rahisi, hali ambayo imeongeza hatari ya kusambazwa kwa dawa zisizo salama kwa matumizi ya mifugo.
Kutokana na changamoto hiyo, TMDA imeeleza kuwa, kuanzia tarehe ya tangazo hilo hakuna mtu au kampuni itakayoruhusiwa kutengeneza, kuingiza, kusambaza au kuuza dawa hiyo ndani ya Tanzania.
Mamlaka hiyo imeonya kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtu au kampuni itakayobainika kuendelea kujihusisha na biashara ya dawa hiyo.
TMDA imewataka wananchi kushirikiana na mamlaka husika kwa kutoa taarifa za watu au kampuni zinazojihusisha na biashara ya dawa bandia, duni au ambazo hazijasajiliwa.
Taarifa hizo zinaweza kutolewa katika vituo vya polisi vilivyo karibu, ofisi za TMDA zilizopo Dodoma, Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Ruvuma, Tabora na Geita.
“Mamlaka pia inawakumbusha wananchi kutotumia dawa bila ushauri wa madaktari, wafamasia au wataalamu wengine wa afya kwa kuwa, dawa ni kemikali zenye sumu zinazoweza kusababisha madhara makubwa, ikiwamo vifo, endapo zitatumiwa vibaya,” inaeleza taarifa hiyo.
