Wizara ya Viwanda na Biashara Zanzibar yaja na vipaumbele vitatuWizara ya Viwanda na Biashara Zanzibar yaja na vipaumbele vitatu

Unguja. Wizara ya Maendeleo ya Viwanda na Biashara imepanga kutekeleza vipaumbele vitatu vinavyolenga kuimarisha sekta hiyo, kutafuta masoko pamoja na kuimarisha mazingira ya ufanyaji biashara na utoaji huduma.

Akisoma makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti hiyo ya 2026/27 barazani leo Mei 21, 2026, Kaimu Waziri katika wizara hiyo, Shariff Ali Shariff amesema kwa mwaka wa fedha 2026/27 imepangiwa kutumia Sh49.95 bilioni.

Kati ya fedha hizo, Sh2.94 bilioni kwa matumizi ya kazi za kawaida na Sh3.26 bilioni malipo ya mishahara, Sh34.26 bilioni zimetengwa kwa kazi za maendeleo na Sh9.48 bilioni   kwa ajili ya ruzuku ya mishahara na kazi za kawaida kwa taasisi za wizara.

Waziri huyo amesema katika kuimarisha biashara, Wizara imepanga kuendeleza ujenzi wa ukumbi wa matukio wakati wa maonyesho kwenye eneo la maonyesho ya kibiashara Dimani.

 “Ujenzi wa mgahawa katika eneo la maonyesho. Aidha, Wizara itaendelea uratibu wa uandaaji wa upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (Mice) chini ya ufadhili wa Korea Exim Bank,” amesema Shariff.

Amesema katika kuimarisha mazingira ya ufanyaji biashara, wizara imepanga kuandaa mkakati wa urasimishaji biashara pamoja na mwongozo wake na kufanya mapitio ya sheria ya biashara ya mwaka 2013 na kanuni zake ikiwemo ya vyuma chakavu, sheria ya leseni ya mwaka 1983, kanuni za Sheria nambari moja ya mwaka 2025 na sheria ya hakimiliki namba 14 ya mwaka 2003.

Kingine ni kufanya mapitio ya mpango mkakati wa wizara, mpango mkakati wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Utoaji Leseni za Biashara na Mpango mkakati wa Ofisi ya Msajili wa Hakimiliki.

Pia, wataanzisha mfumo wa udhibiti wa bidhaa bandia, kuunganisha mfumo wa TAMS na Mfumo wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa ya Tanzania.

Kingine, watafanya tafiti za malighafi zinazopatikana Zanzibar kwa ajili ya uanzishwaji na uendelezaji wa viwanda vya ndani na tafiti za bidhaa zinazotumiwa na wageni, kutathmini uwezo wa uzalishaji, mahitaji na masoko.

Katika kuendeleza sekta ya viwanda, mwaka wa fedha 2026/27 imepanga kuyaendeleza maeneo ya viwanda Dunga Zuze na Chamanangwe kwa ujenzi wa majengo ya viwanda vidogo na vya kati, Unguja majengo manne na Pemba majengo mawili.

Ujenzi wa uzio kuzunguka maeneo ya viwanda Dunga zuze na Chamanangwe. Ujenzi wa barabara katika maeneo ya viwanda Chamanangwe.

Wizara kupitia Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC) inatarajia kuuza tani 2,964 kwa wastani wa bei ya Dola za Marekani 7,200 kwa moja.

“Shirika linatarajia kununua tani 600 za makonyo 54 makavu kwa wastani wa bei ya Sh2,000 kwa kilo. Shirika linatarajia kuzalisha mafuta ya mimea ya aina mbalimbali, kufanya ujenzi wa maghala kwa ajili ya ukodishaji,” amesema Shariff.

Kamati ya Utalii, Biashara na Kilimo imesema haijaridhika na suala la uingizwaji wa fedha kutoka serikalini katika miradi iliyoingiziwa fedha chini ya asilimia 28.

Mjumbe wa kamati hiyo, Abdulghani Ismail Zubeir amesema wamebaini kasoro hiyo ni sehemu ya changamoto zinayoikumba wizara na kusababisha miradi kutokamilika kwa wakati, hivyo kuitaka Serikali kuwaingiza fedha zote na kwa wakati ili kuiwezesha wizara kutekeleza na kuikamilisha miradi hiyo kama ilivyopangwa.

Katika idara ya maendeleo ya viwanda amesema wamebaini kuna mfanyakazi mmoja kisiwani Pemba ilhali serikali inajinasibu kuifungua Pemba.

“Tutakwendaje kuifungua Pemba katika sekta ya viwanda ikiwa kuna mtumishi mmoja tu katika Idara ya Maendeleo ya Viwanda, kamati inamuomba waziri kuja na taarifa za kulitosheleza baraza lako tukufu kuhusiana na kadhia hii ya upungufu mkubwa wa watumishi,” amesema.

Michango ya wawakilishi

Mwakilishi wa Ole, Seif Hamad Suleiman (ACT Wazalendo) amesema kodi zimekuwa nyingi na zinakwenda kuua biashara hoja iliyochangiwa pia na mwakilishi wa Magomeni, Mahfoudh Abdalla Mohamed (CCM) ambaye amesema kodi hizo zinatakiwa kulipwa sehemu moja badala ya kuwepo na taasisi saba kila moja inahitaji ilipwe kivyake, jambo linalozungusha wafanyabiashara.

Mwakilishi wa Mfenesini, Othman Machano Said (CCM), amesema   kabla ya kuanzisha viwanda ifanyike tafiti kujua soko lilivyo na kutolewa elimu kutumia bidhaa zinazozalishwa Zanzibar.

“Kama kuna vikwazo kwa bidhaa za Zanzibar kwa nini tusiweke masharti kulinda bidhaa zetu za viwanda.”

Naye, mwakilishi wa Pandani, Profesa Omar Fakih Hamad (ACT), amesema suala la ujasirimali halijaeleweka vyema na ndio maana katika bajeti limetengewa kiasi kidogo cha fedha.

 “Bado dhana ya ujasiriamali haijaeleweka, mtu anadhani kumpa kijana bodaboda ndio tayari kawa mjasirimali lakini sio kweli tukumbuke ujasiriamali katika uchumi wa nchi unachangia kwa asilimia 70, lakini kwetu bado hilo halipo,” amesema.

Naye, mwakilishi nafasi za wanawake, Aza Januari Joseph (CCM), amesema zamani Zanzibar ndio ilikuwa na bidhaa kwa bei nafuu lakini kwa sasa imekuwa kinyume chake akitaka kujua sababu ya hali hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *