Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema Serikali itahakikisha inafanyia kazi mapendekezo na michango iliyotolewa na wabunge wakati wakijadili bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/27, huku akiahidi wamejipanga kufanya kazi.
Ulenga amesema baada ya kufanikiwa kwa mpango wa hatifungani kwenye ujenzi wa barabara utahakikishia mfuko wa barabara fedha na zitajenga barabara kuu za kiuchumi kwa lengo la kupata fedha zaidi kupitia bandari kwa mizigo inayopita.
Ameyasema hayo baada ya wabunge kuchangia mjadala wa bajeti yake kwa siku mbili na kuhitimishwa leo Alhamisi Mei 21, 2026. Bajeti hiyo ya Sh2.56 trilioni imepitishwa na Bunge hilo.
Akijibu hoja za wabunge ambao walilalamikia ubovu na ujenzi wa barabara, Ulega amesema Serikali imepokea mapendekezo yote na ameahidi fedha zote zitatumika kama ilivyopangwa huku akisisitiza wamejipanga kufanya kazi.
Ulega amesema amepokea maoni na ushauri uliotolewa na wabunge na wanakwenda kuyafanyia kazi na kuhakikisha barabara zinajengwa na kukarabatiwa ili wananchi wasipate adha.
Kodi zilipwe tozo mpya hapana
Awali, Mbunge wa Tarime Mjini (CCM), Mwita Waitara amepinga pendekezo la kuchukuliwa asilimia tano kutoka mfuko wa barabara ikafanye kazi nyingine akisisitiza fedha hizo zote ziende kwenye babaraba.
Aidha, Waitara amepinga ushauri wa kuongeza tozo mpya kwa ajili ya kupata fedha za ujenzi na ukarabati wa barabara huku akisema ipo mianya mingi ya kukusanya kodi na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
“Pendekezo la kamati naunga mkono lakini hili la tozo mwenyekiti sasa hivi maisha yamekuwa magumu kuna mambo ya mafuta wananchi wanalalamika hatuwezi kuongeza mambo ya tozo hapa.
“Hata hivyo TRA kwa taarifa zao hawajafikisha asilimia 60 ya makusanyo kwa vyanzo halali hata nyie wabunge ukienda kufanya manunuzi nani anadai risiti? Ulienda kununua simu ya Sh3 au Sh4 milioni hakuna risiti maana yake hapo kodi ya Serikali haipo na inamaanisha kuna mianya mingi ya ukusanyaji wa fedha,” amesema.
Mbunge huyo amesema, “kila mtu alipe kodi na fedha zitumike kama ilivyokusudiwa.
Kiundwe chombo maalumu kusimamia ubora wa barabara.”
Mbunge wa Mbeya Vijijini, (CCM), Patali Shida ameshauri Serikali iunde chombo mahususi kinachojitegemea kwa ajili ya kusimamia ubora wa barabara zinazojengwa.
“Moja ya changamoto tulizonazo ni barabara zetu zinatengenezwa baada ya muda mfupi zinaharibika. Tuondolee jukumu hili la usimamizi Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) yenyewe ibaki na jukumu la utengenezaji barabara ila kuwe na wakala unaojitegemea yenye watumishi wasio na mashaka kwa usimamizi wa ubora,” amesema.
Akiomba barabara za jimboni kwake amesema, uwepo wa barabara kwenye bajeti ni jambo moja hivyo ameomba Serikali kujenga barabara hizo.
Mbunge wa Itigi (CCM), Yohana Msita ameomba wabunge waungane kuiambia Serikali iongeze fedha kwenye wizara ya ujenzi ikiwemo kukata matumizi maeneo mengine.
Mbunge Msita ameyasema hayo wakati alipoonesha wasiwasi wa kutojitosheleza kwa fedha za bajeti ya wizara katika utekelezaji wake kama ujenzi wa barabara na madaraja.
Kwa upande wake, Mbunge wa viti maalumu CCM, Mwanaisha Ulenge ameunga mkono hatua ya Serikali kuja na mpango wa ujenzi wa barabara kupitia hatifungani huku akisema inaelekea kwenye sera ya Serikali ya uchumi shirikishi.
Naye, Mbunge wa Ngara (CCM), Dotto Bahemu amesema anaamini yako maeneo mengine ya kwenda kutafuta fedha za kujenga barabara na si kuongeza tozo zitakazowaumiza kwa wananchi.
“Naungana na wabunge waliochangia juu ya miradi ya PPP, tunaomba kama kuna wawekezaji wanakuja tunaamini zipo barabara umuhimu zikitangazwa kwenye PPP watu wanajitokeza,” amesema.
Pia, Bahemu ameelezea kilio cha barabara za jimbo hilo huku akishukuru kiasi cha Sh1.5 bilioni kilichotengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kilomita 145.
Spika Zungu amwita Nape
Baada ya Bunge kupitisha bajeti hiyo, Spika Zungu amesimama kuzungumza masuala mbalimbali huku akimtaka Mbunge wa Mtama (CCM), kumshukuru Rais kwa kazi.
Haikujulikana kulikuwa na fumbo lipi hata Spika kumtaka Nape Nnauye asimame na kutoa shukurani katika vitu ambavyo ni nadra kutokea.
Baada ya Bunge kukaa kama kamati na kupitisha bajeti hiyo kwa mafungu ya jumla, Spika Zungu amesimama na kueleza namna ambavyo Serikali ya awamu sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ilivyofanya kazi ya kufungua mikoa ya kusini ambako Spika huyo amesema ndiko asili yake.
“Nape naomba usimame hapohapo umshukuru Rais kwa kazi nzuri aliyofanya kwa mikoa ya kusini,” amesema Zungu.
Aliposimama Nape amempongeza Rais Samia akisema amewasaidia watu wa kusini kuanzia kwenye zao la korosho na sasa kwenye barabara kwa jinsi zinavyojengwa.
Kauli ya waziri huyo wa zamani imekinzana na mchango wake alioutoa mapema jana akiwa mchangiaji wa pili kwenye hotuba hiyo aliposema hawezi kuunga mkono hoja ya Wizara ya Ujenzi kwani Mpango wa hatifungani kwenye ujenzi wa barabara ni changa la macho.
Leo Spika amesema muhimu kutumia Mpango wa Miradi ya Ubia (PPP) ambao amesema baadhi ya nchi zilishaanza miaka 20 iliyopita.
Hata hivyo, katika majibu yake, Waziri wa Ujenzi, Ulega amesema hoja zilizotoka kwa wabunge ni nyingi hivyo itakuwa ngumu kujibu zote badala yake wanakwenda kuzifanyia kazi.
Kuhusu mpango wa hatifungani amewataka wasiwe na wasiwasi kwani wamejipanga na hakuna kitakachoshindikana kwa sasa.
