Unguja. Wafanyabiashara na wataalamu wa mifugo wamesema machinjio yanayotumiwa kwa sasa ya Kisakasaka Mkoa wa Mjini Magharibi hayafai kwa ajili ya usalama na afya za watumiaji, hivyo wameiomba Serikali kujenga machinjio ya kisasa kwa ajili ya usalama wa afya za watumiaji.
Wamesema machinjio hayo hayana vigezo vyovyote kwani mbali na paa la jengo hilo kuvuja, hata mazingira ya kuchinjia yanaiweka hatarini nyama.
Akizungumza katika ziara ya kushtukiza iliyofanywa na Meya wa Jiji la Zanzibar, Kamal Abdulsatar Haji usiku wa kuamkia leo Mei 21, 2026 Mwenyekiti wa machinjio hayo, Idrissa Othman Idd amesema kutokana na machinjio hayo kuwa mabovu wakati wa mvua paa linavuja na nyama wakati mwingine zinalowana.
Ngombe wakiwa wanafungwa na kuangushwa chini kwa ajili ya kuchinjwa katika machinjio ya Kisakasaka Mkoa wa Mjini Magharibi ambayo yanaelezwa kutokuwa salama kwa nyama kutokana na mazingira yake. Picha na Jesse Mikofu
“Kwa hiyo usalama wa nyama unakuwa hatarini kwa sasa tunahitaji soko la kisasa lenye miundombinu mizuri hata kama tukiingiza wanyama wetu kuchinja inakuwa inaridhisha zaidi,” amesema.
Amesema bado wanachinja kienyeji kwa visu vya kawaida kwa kuwaangusha wanyama chini jambo ambalo bado linafanya nyama isiwe katika mazingira mazuri.
“Bado hapa kwetu tunafanya mambo ya kizamani, bado tupo nyuma sana,” amesema.
Amesema umeme ukikatika kunakuwa giza, pia hali huwakosesha maji kwa ajili ya shughuli hiyo maana yanatakiwa kusukumwa kutoka kwenye kisima.
“Kwa hiyo tunaomba tupatiwe umeme wa ziada kama jenereta kusukuma maji kutoka kwenye kisima tofauti na ilivyo sasa ukikatika kazi inasimama,” amesema.
Kauli hiyo imechagizwa zaidi na Ofisa Mifugo Kutoka Wizara ya Kilimo, Maliasili na Mifugo Idara ya mifugo, Zehra Kalimzah ambaye amesema machinjio hayo hayana vigezo.
Amesema kutokana na hali hiyo wana asilimia kubwa kuzalisha nyama ambayo haina vigezo vya usalama na afya ya mlaji kutokana na mazingira yalivyo.
Kalimzah amesema katika uchinjaji kuna mchakato unaotakiwa kufuatwa kabla ng’ombe kuchinjwa, lakini wakati mwingine hazifuatwi kwa sababu hakuna mazingira hayo.
“Kwani ng’ombe anaingia moja kwa moja analazwa chini hapohapo anachinjwa, anachunwa na kutolewa nyama katika mazingira hayohayo. Kwa ufupi Zanzibar hatuna machinjio, tunahitaji mengine,” amesema.
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, ng’ombe wanaopokewa kutoka nje ya Zanzibar wanakaa karantini kwa siku 14 ili kuangaliwa usalama wao kabla hajachinjwa au kupelekwa kwenye maeneo mengine kwa ajili ya kufuga.
Hiyo ni kwa mujibu wa sheria ya mifugo ya 1999 inayosema mnyama yoyote anayetoka nje ya Zanzibar lazima akae karantini siku 14 kabla ya kuingizwa mtaani au kuchinjwa.
Naye Mkuu wa machinjio hayo, Ramadhan Juma Ramadhani amesema wanapopokea ng’ombe hao wanaoshwa kwa ajili ya kuua wadudu ambao wanaweza kusababisha maradhi.
Ngombe wakiwa wanafungwa na kuangushwa chini kwa ajili ya kuchinjwa katika machinjio ya Kisakasaka Mkoa wa Mjini Magharibi ambayo yanaelezwa kutokuwa salama kwa nyama kutokana na mazingira yake. Picha na Jesse Mikofu
Amesema karantini inasaidia magonjwa yasiende katika makazi yao au kuchinjwa wakiwa hawapo katika hali inayoridhisha.
“Kabla ya kuchinjwa mbali na kufanyiwa vipimo, lakini anaangaliwa pia kwa macho, kuna dalili za awali na kisha kupimwa ili kugundua maradhi yake,” amesema.
Naye mlinzi mkuu wa eneo hilo, Makungu Hamad Makungu amesema kuna changamoto mbali ya uchafu katika eneo hilo, lakini wakati mwingine wanakutana na wizi wa mifugo kutokana na mazingira yake, hivyo wanahitaji kuboreshewa miundombinu iliyopo pale.
“Tunaomba mazingira yaboreshwe kwani eneo hili lilivyo kwanza ni pori hata wizi ni rahisi kutokea,” amesema.
Naye Meya wa Jiji la Zanzibar, Kamal Abdulsatar Haji amesema hali hairidhishi kuanzia barabara hadi eneo la machinjio yenyewe.
Amesema sehemu hiyo inahitaji kuboreshwa, hivyo watakaa na wizara husika kuona mipango yao kwa haraka waangalie namna ya kuboresha mazingira hayo.
“Zanzibar ipo mbele kimaendeleo hatuwezi tukawa na eneo kama hili kwa hiyo lazima tupate machinjio mazuri ya kisasa, tunaweza kupata wafadhili kutoka sekta binafsi kusaidia katika hili,” amesema.
Naye Daktari wa Mifugo kutoka idara ya maendeleo ya mifugo, Dk Fatma Said Abdullah amesema wakati wa sikukuu ya kuchinja kutokana na mazingira wameandaa mazingira mengine madogomadogo ambayo watapelekwa wataalamu kwa ajili ya kuangalia mifugo, kabla ya kuchinjwa kama miongozo inavyoelekeza.
