Simu inavyotengeneza kizazi kipya cha wawekezaji nchini  Simu inavyotengeneza kizazi kipya cha wawekezaji nchini  

Katika kipindi cha robo mwaka kilichoishia Machi 31, mauzo ya jumla katika soko la Dar es Salaam (DSE) yalikuwa Sh571.1 bilioni yakiongezeka kutoka Sh135.7 kipindi kama hicho mwaka uliopita huku mauzo ya ndani yakiongoza kwa kuuza Sh553 bilioni.

Jumla ya thamani ya hati fungani zilizouzwa DSE iliongezeka na kufikia Sh1.65 trilioni ikiwa ni ongezeko la asilimia 70.7 ikilinganishwa na mauzo ya Sh966.61 bilioni yaliyofanyika katika kipindi kama hicho mwaka 2025.

Hisa zilizouzwa katika soko hilo zilikuwa milioni 217.3 ikilinganishwa na robo ya kwanza ya mwaka 2025 ambapo hisa milioni 83.2 tu ndizo zilizouzwa, ukuaji wa mwaka hadi mwaka ni asilimia 161.18.

Mtaji wa jumla wa soko (market capitalization) kufikia mwisho wa robo ya kwanza ya mwaka 2026 ulikuwa Sh33.44 trilioni ikiongezeka kutoka Sh19.21 trilioni uliokuwapo kipindi kama hicho mwaka 2025.

Kwa upande wa mtaji wa soko la ndani, kufikia mwisho wa robo ya kwanza ya mwaka 2026 ulikuwa Sh23 trilioni ikilinganishwa na robo ya kwanza ya mwaka 2025 ambapo mtaji wa soko la ndani ulikuwa Sh12.94 trilioni.

Hata hivyo jambo la kutazama hapa ni kuwa hadi Machi 31, 2026, jumla ya akaunti za Mfumo wa Hifadhi ya Kielektroniki wa Hisa (CDS) ziliongezeka na kufikia akaunti 815,838 kutoka akaunti 632,715 zilizokuwapo mwishoni mwa robo ya kwanza ya mwaka 2025.

Ukuaji huo unaonyesha ongezeko la asilimia 12.73 kwa robo hadi robo na asilimia 28.94 kwa mwaka hadi mwaka lakini pia kulikuwa na wa asilimia 244.55 kwa mwaka hadi mwaka kwa upande wa akaunti mpya zilizosajiliwa.

Katika kipindi hicho jumla ya akaunti zilizosajiliwa kwenye mfumo wa biashara ya hisa kwa simu ya mkononi (Mobile Trading Platform – MTP) unaojulikana kama “Hisa Kiganjani” zilifikia akaunti 216,173 zikiongezeka kutoka akaunti 62,740 kipindi kama hicho mwaka jana.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa DSE, Peter Nalitolela anasema ushirikiano wao na watoa huduma za simu umeleta matokeo chanya sokoni hususani kuongeza ushiriki wa wateja wadogo wadogo akisema wanawafikia watu wengi zaidi kwa urahisi akitolea mfano kuwa kupitia jukwa la Mixx by Yas watu zaidi ya 9,000 wamefungua akaunti.

“Kupitia majukwaa kama Hisa Kiganjani na ushirikiano na MNOs kama Mixx, uwekezaji sasa umefika kwa wananchi wengi zaidi kupitia simu zao za mkononi. Mauzo kupitia simu yameongezeka kwa asilimia 656 kufikia Sh106 bilioni jambo ambalo linaonyesha namna gani dijitali ilivyorahisisha,” anasema Nalitolela.

Bosi huyo wa soko pekee la hisa nchini anasema zamani ushiriki wa wawekezaji wadogo ulikuwa mdogo kutokana na changamoto za kuwafikia, elimu na mifumo ya uwekezaji kutokuwa karibu na wananchi wengi. Lakini sasa kupitia simu shiriki umeongezeka kwa kiwango kikubwa.

“Kwa sasa zaidi ya asilimia 98 ya wawekezaji DSE ni wazawa, jambo linaloonyesha kuwa soko limeanza kufikiwa na wananchi wa kawaida zaidi kuliko ilivyokuwa miaka ya nyuma. Pia jumla ya akaunti za CDS zimefikia zaidi ya 740,000, ishara kwamba ushiriki wa wananchi unaendelea kukua kwa kasi.”

Kuhusu aina ya wawekezaji Nalitolela anasema kiasi kikubwa wanaona vijana na watu wa kipato cha kati ndio wanaongoza kutumia zaidi majukwaa ya kidijitali akisema wengi wao wana umri kati ya miaka 18 na 38.

“Kundi kubwa zaidi la wawekezaji wapya ni wenye umri wa kati ya miaka 21 mpaka 30, ambao walichangia zaidi ya asilimia 40 ya akaunti mpya mwaka 2025. Pia kwenye simu karibu asilimia 44 ya watumiaji wote ni vijana wa miaka 20–29. Hii inaonyesha wazi kwamba kizazi cha kidijitali kinaanza kuona uwekezaji kama sehemu ya maisha yao ya kifedha,” Alisema.

Mkuu wa Wateja wa Makampuni na Washirika wa Mixx Justine Lawena anasema kupitia Jukwaa lao la Mixx mwekezaji DSE anapata urahisi kwani tayari ni jukwaa ambalo linatumika kwa maisha ya kila siku kwa miamala hivyo huduma ya kuwekeza inakuwa ni sehemu ya kuongeza urahisi na thamani kwake.

“Lengo letu kubwa ni kufanya uwekezaji uwe rahisi kama kufanya miamala au kulipa bili. Kupitia Mixx Super App, tunataka Mtanzania aweze kupata huduma za uwekezaji ndani ya mfumo mmoja anayoiamini tayari kila siku,” anasema Lawena.

Kuhusu ongezeko la miamala ya DSE kutokana na ushirika wao na Yas Lawena anasema kwao hiyo siyo tu ongezeko la miamala, bali ni ishara kuwa kwamba wananchi wanaanza kuamini zaidi mifumo ya fedha kidijitali.

“Tunapoona thamani ya miamala inaongezeka sisi tunaona kuongezeka kwa imani ya matumizi ya huduma rasmi za kifedha na ushiriki kwenye uchumi rasmi vinaongezeka pia. Hii inaonyesha nguvu ya uchumi wa kidijitali na fursa kubwa ya kuunganisha mfumo ya malipo na uwekezaji katika jukwaa moja,” anasema.

Anasema Mixx ina nafasi kubwa kwenye soko la Tanzania ikiwa na karibu asilimia 29.5 ya huduma za miamala, jambo linalowapa uwezo mkubwa wa kusogeza huduma za uwekezaji karibu zaidi na wananchi wengi zaidi.

Lawena anasema kutokana na ushirika na maboresho wanayoendelea kufanya watumiaji wa Mixx watarajie mfumo mpaka zaidi unaounganisha malipo, biashara, kuweka akiba, uwekezaji, makusanyo, utumaji, bima na huduma nyingine za kidijitali zikiwa sehemu moja.

Anasema kwa sasa dunia inaelekea kwenye “financial super apps,” na kwa mujibu wa GSMA, huduma za miamala kwa simu zimevuka thamani ya Dola za Marekani 2 trilioni kwa mwaka, huku huduma zinazokua kwa kasi zaidi zikiwa ni akiba, mikopo, bima na uwekezaji.

“Mwelekezo wetu ni kutoka kwenye malipo ya kidijitali pekee kwenda kwenye mfumo wa maisha ya dijitali ambapo Mtanzania hataishia kutuma na kupokea fedha pekee, bali pia ataweza kujenga utajiri, kuwekeza, kufanya biashara, na kusimamia maisha yake yote ya kifedha kupitia jukwaa moja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *